*SASA MBIONI KUTENGEZA FAIDA, KILA WILAYA KUUNGANISHWA MKONGO WA TAIFA
NA MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limetangaza mageuzi makubwa ikiwamo kutengeza faida pamoja na kuhakikisha wanafikisha huduma ya mtandao kupitia Mkongo wa Taifa.
Akizungumza leo Alhamis Agosti 24, 2023 Jijini Dar es Salaam, katika mkutano ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wahariri wa vyombo vya habari Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Peter Ulanga amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili hadi mitatu iliyopita hali ya shirika hilo haikuwa nzuri kifedha na ingawa bado linaendelea kujiendesha.
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa kwa mwaka wa Fedha 2022/23 tayari kuna dalili za kufanya vizuri kwa shirika hilo hilo nyeti la mawasiliano.
“Katika hesabu zetu miwili hadi matatu hakufanya vizuri sana na mwaka 2021/22 tulipata hasara lakini kwa mwaka 2022/23 tunakwenda vizuri na sasa tunasubiri hesabu zetu kwa wahasibu pamoja na kupata maoni ya Mkaguzi lakini mwelekeo si mbaya na tunaelekea kutengeneza faida itakayofikia kiasi cha Shilingi Bilioni mbili hivyo hali ya mwekeleo wetu kwa maana hesabu tunakwenda vizuri sana,” amesema Ulanga
Akizungumzia mkakati wa shirika hilo, Ulanga amesema kwa sasa wanaendelea kufanya mageuzi ndani ya shirika hilo ikiwamo kulifanya kuwa kitovu cha mawasiliano wa Taifa kuelekea uchumi wa kidigitali.
“Mizania yetu ipo vizuri kwa sasa kwenye vitabu ambapo kwa mwaka 2022 inaonyesha tupo na mtaji wa Shilingi Bilioni 300.7 na tunatarajia mizania yetu itapanda na kufikia hadi Sh trilioni moja kwa upande wa ukwasi hatupo vibaya. Kutokana na mipango yetu tuna uwezo wa kwenda nje ya mipaka.
“Ukwasi wa watumishi tunao 1200 kutokana na kazi yetu japo yapo makapuni ya simu yanafanyakazi 300 na hawa kwa asili ya kazi yetu wamekuwa wakijituma zaidi,” amesema
Amesema mara baada ya kuanza safari ya mageuzi Bodi ya Wakurugenzi iliitaka menejimenti kuonyesha uwezo ambapo mwaka 2022 walifikisha huduma za mtandao wa TTCL katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa TTCL amesema kuwa kwa sasa uendeshaji wa shirika hilo unategemea ruzuku ya Serikali kwa asilimia 100 ingawa katika mkakati wao wa hivi karibuni TTCL itaanza kujitegemea kutokana na mapato yake.
“Moja kati ya mageuzi makubwa ambayo tumeyafanya ndani ya TTCL ni kuhakikisha tunajenga minara 4000 ambayo yote tunaunganisha na mtandao wa Faiba ambapo sasa tunataka kupeleka huduma hii katika kila nyumba nchini kama njia ya kuimarisha mkakati wa matumizi wa mtandao kupitia Mkongo wa Taifa ambao upo chini ya shirika hili muhimu la Taifa.
“Wateja wetu wakubwa ni kampuni karibu zote za simu kama Vodacom, Tigo, Zantel ambao hawa wote wanatumia huduma za mkongo wa Taifa pamoja na makabenki yote. Pia yapo mashirika ya umma, Uhamiaji, Tanesco, TRA, TPA. TAA, TCAA pamoja na hospitali zote za Serikali ambao hawa kwa asilimia 100 wanategemea huduma kutoka TTCL ambapo kote huko tumejenga miundombinu yetu inayowawezesha kupata huduma zetu za mtandao,” amesema Ulanga
Amesema katika kuhakikisha wanaendelea kujiimarisha Shirika hilo la Mawasialino nchini, limekuwa likitoa huduma katika nchi za jirani kama Malawi, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Zambia, Kenya na Tanzania yenyewe ambapo Kampuni za Halotel, Zantel, Airtel, Tigo, Liquid, Vodacom na Wananchi wanatumia huduma za TTCL.
“Ndani ya nchi tuna mikakati na sasa tunajivunia na kujisikia faraja TTCL kama shirika la umma limekuwa tegemeo hata kwa nchi jirani katika kutoa huduma kupitia Mkongo wa Taifa. Lakini pia tumeendelea kujenga minara ya simu 150 ambapo huko hakuna huduma za minara za mtandao wowote wa simu na kama tutazima zaidi ya wananchi 200,000 watakosa mawasiliano,” amesema
WILAYA KUUNGANISHWA MKONGO
Ulanga, amesema kuwa kabla ya Januari 2024 TTCL itakuwa imefika katika wilaya zaidi ya 90 na ifikapo Desemba 2024 makao makuu ya wilaya zote yataunganishwa na huduma hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Ufundi, Mhandisi Cecil Francis, amesema kuwa wilaya 100 tayari zimeunganishwa na Mkongo wa Taifa na kufikia Desemba 2023 wataongeza wigo na kufikia kuwa na wilaya 139 ambazo zitapata huduma hiyo.
Naye Mkuu wa T-Pesa, Lulu Mkudde, amesema kuwa Shirika la Mawasiliano limejinga kuhakikisha inakuwa nguzo muhimu ya miamala ya kifedha kwa njia ya kielektoniki katika kuhakikisha wanafanya utekelezaji wa kubuni na kuanzisha miradi mbalimbali yenye uwezo wa kujiendesha.
“Katika kufanikisha hili T-Pesa kupitia mpango kazi wake wa miaka minne 2022/26 imewekwa wazi utekelezwaji wa na uanzishwaji wa miradi mbalimbali na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za mapinduzi ya Kidigitali ikwamo pamoja na maendeleo ya huduma za kijiditali katika masuala ya fedha, afya, elimu, utawala wa umma na taarifa za soko kama ilivyoelekekezwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (NFYDP III).
“Kampuni imepanga kusajili wateja kutoka milioni 1.2 hadi kufikia milioni tatu. Kuongeza wigo wa matumiziya Internet kufikia asilimia 20 ya malengo yake pamoja na kuongeza huduma za lipa kwa T-Pesa hadi kufikia 36,000 nchi nzima.
“…kuongeza mahusiano na washirika wetu pamoja na kuongeza wigo wa matumizi ya huduma za kijiditali nchini,” amesema Mkudde