Serikali ya Msumbiji inasema wanajeshi wake wamemuua kiongozi wa kundi la wanajihadi lenye uhusiano na Islamic State ambalo linapigana kaskazini mwa nchi hiyo.
Wizara ya ulinzi ilisema Bonomade Machude Omar – ambaye pia anajulikana kama Ibn Omar – alikuwa ameongoza waasi tangu kuanza kwa vita mwaka 2017.
Taarifa ilisema aliuawa pamoja na viongozi wengine wawili wakuu.
Hakujawa na uthibitisho huru wa vifo hivyo.
Miaka miwili iliyopita, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilimtangaza Omar kuwa kiongozi wa magaidi, ikimlaumu kwa mashambulizi katika jimbo la Cabo Delgado, yakiwemo mauaji ya makumi ya watu katika hoteli moja mjini Palma.
Mwezi mmoja kabla ya hapo, jeshi la Msumbiji lilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya wapiganaji hao kwa msaada wa mamia ya wanajeshi kutoka Rwanda na nchi kadhaa za kusini mwa Afrika.
Kwa mujibu wa serikali, Omar na washirika wake wawili kutoka kundi lenye uhusiano na Islamic State waliuawa katika msitu wa Macomia katika operesheni iliyotekelezwa na washirika wa kigeni wa jeshi hilo.
Chanzo: BBC