Home KITAIFA CEO NMB akabidhi misaada ya milioni 10/- New Hope for Girls

CEO NMB akabidhi misaada ya milioni 10/- New Hope for Girls

Google search engine
Mkuu wa Idara ya Biashara na huduma za Serikali wa Benki ya NMB, Vicky Bishubo(kulia) akimkabidhi vifaa mbalimbali Mkurugenzi wa kituo cha New Hope for Girls, Dk Consoler Eliya (kushoto) vilivyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna ikiwa ni msaada kwa kituo hicho kutoka kwenye zawadi ya Malkia wa nguvu aliyotunukiwa mnamo mwezi wa tatu.
Mkuu wa Idara ya Biashara na huduma za Serikali wa Benki ya NMB, Vicky Bishubo(kulia) akimkabidhi vifaa mbalimbali Mkurugenzi wa kituo cha New Hope for Girls, Dk Consoler Eliya (kushoto) vilivyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna ikiwa ni msaada kwa kituo hicho kutoka kwenye zawadi ya Malkia wa nguvu aliyotunukiwa mnamonmwezi wa tatu. Kulia ni mkuu wa idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya NMB, Rahma Mwapachu

NA MWANDISHI WETU

MIEZI mitano tangu alipotunukiwa Tuzo ya Malkia wa Nguvu (wa Sekta Binafsi Tanzania), Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, ameitoa zawadi iliyoambatana na tuzo hiyo kwa Dk. Consoler Eliya wa New Hope for Girls Foundation, aliyemkabidhi misaada ya vifaa vya malazi, shule na chakula vyenye thamani ya Sh. Mil. 10, kwa ajili ya wasichana 60 wa familia hiyo.

Machi 25 mwaka huu, Clouds Media Group ilimtunukia CEO Zaipuna tuzo hiyo, kutokana na mafanikio ya NMB chini ya uongozi wake, alikosimamia nyanja za Ubunifu wa Huduma Suluhishi za Kifedha, Uwekezaji wa Kiteknolojia na Mapinduzi ya Mifumo ya Kidigitali, ikiwa na zawadi ya pesa Sh milioni tatu, ambazo ameziongeza na kufikia Sh milioni 10 na kununulia vifaa alivyokabidhi kwa familia ya New Hope for Girls ya Kimara Stop Over, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya CEO Zaipuna, Mkuu wa Idara ya Huduma za Serikali wa NMB, Vicky Bishubo, aliishukuru Clouds Media sio tu kwa tuzo waliyompa, bali kuwashirikisha katika jambo la baraka la kuiwezesha familia ya Dk. Consoler, mwanamke aliyekidhi vigezo vyake yeye vya kutunukiwa tuzo ya Malkia wa Nguvu kutokana na mchango wake kwa jamii.

“Niko hapa kwa niaba ya CEO Zaipuna, ambaye ametingwa na shughuli za kiofisi na kunituma kumuwakilisha kukabidhi misaada hii yenye thamani ya Sh. Milioni 7 na Sh. Milioni 3 nyingine zimewekwa kwenye akaunti ya familia hii, hivyo kufanya thamani ya jumla ya msaada kuwa Sh. Milioni 10, nyongeza ikitokana na pesa zake binafsi, pamoja na utaratibu benki kupitia Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI – zamani CSR).

“CEO Zaipuna ametoa vifaa vya malazi, vifaa vya shule na chakula, ambavyo ni magodoro, mashuka, mchele, mafuta ya kupikia, tambi, unga wa ngano, sembe, madaftari, ‘rim paper,’ ‘calculator,’ vitambaa na sare za shule, hii ni katika kumuunga mkono Dk. Consoler na mumewe wanaoishi na wasichana hawa,” alisema Bishubo mbele ya wanahabari.

Kwa upande wake, Dk. Consoler alimshukuru CEO Zaipuna kwa moyo ya kujali aliouonesha kwake na familia yake hiyo ya watoto 60, wakiwemo wawili aliowazaa yeye na mumewe Eliya na watoto wa kulea wapatao 58, msukumo wa kuwalea mabinti hao ukitokana na changamoto alizopitia akiwa mdogo, kiasi cha kuweka ahadi kwa Mungu ya kuja kuwasaidia wengine watakaopitia Mazingira magumu.

“Nina miaka 18 ya kutoa huduma ya ulezi wa wasichana hawa, miaka mitatu kabla ya kuolewa kwangu na miaka 15 baada ya ndoa yangu na Bwana Eliya, ambaye amekuwa bega kwa bega na mimi katika matunzo na malezi ya wasichana hawa. New Hope for Girls ilianza kama kaulimbiu ambayo matamanio yangu ni kuiona ikiwa ya kitaifa, itakayowezesha watoto wote kuwa na kwao na sio kwenye Vituo.

“Naamini Tanzania ina Wananchi wengi wenye wanaoweza kugawana watoto wenye uhitaji kwa kushirikiana na wadau kama NMB, ili kuhakikisha watoto wanakuwa na kwao, pamoja na kuwapunguzia mzigo wachache waliojitolea kuwatunza. Kiu yangu na mume wangu ni kuona vinavyoitwa Vituo vya Watoto (yatima na wanaoishi kwenye Mazingira magumu), vinageuka kuwa familia zao na kuishi kifamilia,” alibainisha Dk. Consoler.

Alisisitiza kuwa siri ya mafanikio yake katika malezi na matunzo ya wasichana hao walio kwenye ngazi za chekechea hadi vyuo vikuu, ni kuwalea katika misingi ya dini, ambako mabinti hao wanafundishwa kumjua na kumtegemea Mungu na kwamba tangu aanze amekaa na wasichana 150, kati ya hao tisa waliolewa wakiwa mikononi mwake na kupata wajukuu 12, ambapo licha ya kuihama familia hiyo baada ya ndoa zao, wanawatembelea waliopo.

“Tunamshukuru CEO Zaipuna kwa msaada huu mkubwa alioutoa, tunaishukuru pia NMB kwa kututambua na kuchagua kusaidia kulea na sisi. Mmefanya jambo kubwa kwangu Binafsi na familia yangu kwa ujumla,” alimalizia Dk. Consoler, huku Ushindi Charles, binti wa miaka 23, akitoa neno la shukrani na kushukuru kwa msaada huo, uliokabidhiwa mbele ya Lilian Kisamba, ambaye ni Meneja wa Benki ya NMB wa huduma za kurejesha kwa jamii.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here