*Afunga mafunzo ya wajariamali Stanbic Biashara Incubator
Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, amesema kuwa Serikali itakikisha Watanzania wananufaika na fursa rasilimali zilizopo nchini na kupitia Mpango wa Tatu wa maendeleo FYDP III.
Hayo amesema mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam, katika mahafali ya wajasiriamali 100 walioshiriki mafunzo ya Program ya Supplier Development inayoratibiwa na Benki ya Stanbic Tanzania chini ya mpango wa Stanbic Biashara Incubator.
Kutokana na hilo Zungu, ameipongeza Benki ya Stanbic kwa kuratibu vema mpang huo wenye manufaa katika kuinua vijana na kuwafanya wajiajiri huku akiwataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri kwa jamii has kutokana na umuhimu wa program hiyo ambayo inakwenda kuakisi falsafa ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan
“Tumejikita katika kukabiliana na changamoto zote zinazowakabili wajasiriamali na kuweka mifumo endelevu utakayowezesha kufikia malengo ya sera za Taifa za ushiriki wa watanzania (local content) katika kujenga uchumi,” amesema Naibu Spika Zungu
Aidha ametoa rai kwa wahitimu kwenda kufanya kazi kwa mtazamo mpya wa kukabiliana na changamoto za jamii na kila mmoja akatimize wajibu wake.
“Tukiwa ni kiungo muhimu katika kukuza uchumi wetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko, tunaweza kuinua jamii zinazotuzunguka na kuhakikisha tunakuwa na maendeleo jumuishi katika nchi yetu,” amesema Zungu
Awali akizungumza katika mahafali hyo, Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Stanbic Tanzania, Fred Max amesema mpango huo wa Stanbic Biashara Incubator sio programu tu bali ni kujitolea kwa hisani na kukuza mafanikio ya miradi ya ujasiriamali.
Amesema kupitia mfumo huo na mpango wa rasilimali na huduma za usaidizi wa biashara, tunalenga kuharakisha ukuaji wa kampuni hizi, tukiwapa zana wanazohitaji ili kustawi.
“Mheshimiwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, katika mpango huu kuna vipengele ambavyo ni pamoja na anuwai ya rasilimali za usaidizi kama vile nafasi halisi, ujumuishaji wa mtaji, mafunzo na mwongozo, huduma za kawaida, na muhimu zaidi, ufikiaji wa mtandao muhimu wa miunganisho,” amesema Max
Ameongeza kuwa kupitia mpango huo ambao umelenga kwa wajasiriamali wa kati SME’s ambao wanachangaia maendeleo ya kimkakati ndani ya nchi.
“Macho yetu yameelekezwa kwenye sekta ambazo zina jukumu muhimu katika ukuaji wa Taifa letu ambazo ni Kilimo na uzalishaji vifungashio na vifaa vya ujenzi pamoja na kazi za kira na malighafi.
“…nyingine kuwa ni usafiri, upishi na masuala ya hoteli pamoja na wazalishaji wa bidhaa za watumiaji zinazoenda haraka (zinazojumuisha vifaa vya kusindikia vyakula na dawa. Pamoja na huduma za biashara ikiwa ni pamoja na sheria, elimu, fedha, kufundishaji na Mawasiliano na Teknolojia,” amesema Max
Akifafanua zaidi kuhusu lengo ya mradi huo, Max amesema malengo ya benki yao yapo wazi na yenye kuleta mabadiliko kwa jamii kupitia Stanbic Biashara Incubator ambayo imelenga kukuza maudhui ya ndani kwa kuimarisha biashara za ndani na kunaziwezesha kupata kandarasi na kampuni za kimataifa.
“Pia kuboresha na kupitia sera ya uchumi wa ndani kwa kiwango cha kimataifa pamoja na kushughulikia mahitaji na kupunguza msururu wa ugavi (ununuzi) kupitia mpango huu sambamba na kukusanya taarifa,” amesema