Home KITAIFA DK. HUSSEIN MWINYI AENDESHA HARAMBEE KUWEZESHA MPANGO WA BBT

DK. HUSSEIN MWINYI AENDESHA HARAMBEE KUWEZESHA MPANGO WA BBT

Google search engine
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza leo Septemba 07, 2023 katika mkutano wa pembeni katika Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika  linaloendelea kufanyika katika ukumbi wa kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, wakati wa mjadala kuhusu mchango wa BBT kwa vijana nchini leo jijini Dar es Salaam
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akizungumza leo Septemba 07, 2023 katika mkutano wa pembeni katika jukwaa la mifumo ya chakula Afrika  linaloendelea kufanyika katika ukumbi wa kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Mmoja wa wachokoza mada katika mkutano huo
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wakifuatilia hoja mbalimbali

NA MWANDISHI WETU

-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Husein Ali Mwinyi leo Septemba 7, 2023, ameongoza harambee kwa washiriki mbalimbali wa ndani na nje ya nje kuchangia utekelezaji wa Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).

Dk. Mwinyi, aliongoza harambee hiyo iliyofanyika kwenye mkutano wa pembeni wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaoendelea kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaa, ambao umewakutanisha wadau na viongozi kutoka mataifa mbalimbali ya Bara la Afrika.

Akizungumza wakati wa harambee hiyo, Dk. Mwinyi amesema kuwa kumekuwa na utashi wa kisiasa unaokua kwa kasi barani Afrika hususani Tanzania unaolenga kuwawezesha vijana na wanawake kupitia kilimo biashara.

Amesema, utashi huo unaonekana kutokana na uwepo wa juhudi za makusudi zinazofanywa Serikali ikiwamo kupitishwa mikataba ya tamko la mpango wa utekelezaji wa vijana, kunzishwa kwa dawati la vijana katika mpango mpya wa ushirikiano wa pamoja na uwezeshaji mpango huo wa BBT.

Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, amesema kuwa serikali imeandaa mikakati shirikishi na kutekeleza mipango ya kusaidia vijana na wanawake katika sekta ya kilimo biashara katika hatua za uwezeshaji wa mradi wa BBT utaongeza ajira kupitia mfumo wa chakula.

Dk. Mwinyi, amesema kutokana na kukua kwa mifumo ya kidigitali inayosimamia mabadiliko ya uchumi wa dunia kumekuwa na ongezeko la kasi kwa vijana kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi Afrika kupitia kilimo.

“Bado kuna changamoto ya ushiriki mdogo wa vijana na wanawake katika sekta za kilimo na uvuvi kutokana na upatikanaji mdogo wa rasilimali za uzalishaji, ujuzi na ukosefu wa mitaji,” amesema Rais Dk. Mwinyi

Akizungumzia kuhusiana na vijana, amesema vijana wana hamu ya kuwekeza sehemu zenye matokeo ya haraka.

Kutokana na hali hiyo Rais Dk. Mwinyi, amesema ili kufikia mafanikio yapo maeneo yanahitaji ufumbuzi ikiwemo upatikanaji wa huduma za kijamii vijijini ili kupunguza wimbi la vijana ambao wanao uwezo wa kushiriki katika kilimo kuhamia mjini.

“Ni muhimu sana kumaliza tatizo la kukosekana kwa masoko, vikwazo vya kimazingira na mabadilioo ya tabia nchi, kukosekana kwa miundombinu ya uzalishaji na kutafuta ufumbuzi katika uwekezaji wa teknolojia,” amesema

Akizungumzia uwezeshaji wa vijana na wanawake katika sekta ya kilimo amesema ufunguo wa milango ya ajira ni kilimo ambacho kinaweza kuwa chanzo cha kupunguza umaskini na matokeo ya uzalishaji wa chakula na kujiongezea la thamani.

Ili kufikia malengo ya vijana na wanawake katika nchi za Afrika, Rais Dk. Mwinyi, amesema Serikali ya Tanzania imejidhatiti katika kuwawezesha vijana na wanawake kufikia malengo yao, ikiwemo kuwepo kwa mazingira wezeshi katika kilimo biashara.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema, lengo la serikali ni kukusanya zaidi ya dola bilioni 2 kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa BBT unaoisha mwaka 2030.

Amesema, hatua hiyo itawezesha ukuaji wa uchumi kwa kuwa kilimo kinachangia asilimi 25 ya Pato la Taifa huku asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, kinatoa  asilimia 75 ya ajira na kuchangia mauzo ya nje ya nchi kwa asilimia 85.

Mradi wa BBT unalengo la kujumuisha vijana zaidi ya milioni 16 katika mfumo rasmi wa kiuchumi kupitia kilimo biashara kwa kuwapa elimu na uwezeshaji.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here