Na MWANDISHI MAALUM
– BUDAPEST, HUNGARY
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango ametoa wito kwa mataifa kutambua umuhimu kuweka mkazo katika taasisi ya familia ya kiutamaduni ili kuifanya kuwa kiini cha maendeleo ulimwenguni.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati leo Septemba 14, 2023, wakati akihutubia kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Tano wa Idadi ya Watu (5th Budapest Demographic Summit) unaofanyika Jijini Budapest nchini Hungary.
Amesema inahitajika nguvu ya pamoja kimataifa katika kuimarisha ustawi wa familia ikiwemo kuzingatia kanuni na desturi za kiutamaduni pamoja na kuunga mkono mafundisho ya dini ambayo yanakuza maadili ya familia na kulinda usalama na mwendelezo wa familia.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Mpango, ametoa wito kwa serikali ulimwenguni kutengeneza na kutekeleza sera, programu na sheria zitakazohakikisha usalama na uendelevu wa familia.
Aidha ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana na Bara la Afrika katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na ongezeko la idadi ya watu zikiwemo uhitaji wa huduma za afya na elimu, ukosefu wa ajira, upungufu wa chakula na uhamiaji haramu.
Akitoa mfano wa Tanzania katika mkutano huo wenye kauli mbiu ya “Familia Msingi wa Usalama” Makamu wa Rais amesema nchini Tanzania familia inatambuliwa kama msingi imara na muhimu ambayo ni mwanzo wa ujenzi wa mtandao wa mahusiano ya jamii nzima.
Hata hivyo amesema kuwa Tanzania familia inahusisha muunganiko wa ndoa ya watu wa jinsia mbili tofauti,watoto wao pamoja na ndugu au wategemezi wao ambapo pamoja na mambo mengine, familia hutumika kuimarisha utaratibu na utulivu katika jamii na pia husaidia katika uwezo wa kufanya maamuzi na utatuzi wa matatizo pamoja na utulivu wa kifedha, utoaji wa elimu na huduma za afya kwa wanafamilia na malezi.
Makamu wa Rais amesema pamoja na kuendelea kusisitiza na kuimarisha ustawi wa familia, serikali ya Tanzania imeendelea kuwekeza katika kujenga uchumi na kuboresha miundombinu ya kijamii kwa maendeleo ya watu ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji, umeme, elimu pamoja na utoaji wa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari.
Ameongeza kwamba serikali imeongeza jitihada katika kuwavutia vijana ambao ni idadi kubwa iliopo nchini kushiriki katika kilimo biashara kwa kuanzisha programu maalum ya Jenga Kesho iliyobora (BBT).
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema sababu za kiuchumi na migogoro zinazopelekea ongezeko la wahamiaji ndizo zinazopelekea athari ya mienendo ya idadi ya watu Barani Afrika. Amesema Tanzania imekuwa ikihifadhi wakimbizi zaidi ya laki nne kutoka mataifa Jirani ambao wamekua wakitafuta amani na ustawi wa maisha yao.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa kwa nchi na mataifa kuiunga mkono Tanzania katika kuwahudumia wakimbizi ambapo uwepo wao huongeza mahitaji kama vile ya ardhi, maji, huduma za kijamii na miundombinu.
Pia ametoa wito wa kuboresha usalama wa kitaifa na kikanda, kuzuia migogoro, kuimarisha na kulinda amani pamoja na kuongeza juhudi katika kuzuia na kupambana na ugaidi.
“Tanzania inathamini ushirikiano na Jamhuri ya Hungary katika nyanja ya Elimu na kuinua ujuzi. Serikali imedhamiria kuimarisha uhusiano na nchi ya Hungary katika ukuzaji wa ujuzi kwa vijana, uwekezaji hususani katika kilimo na biashara ya kilimo, uongezaji wa thamani, utengenezaji wa bidhaa, utalii na teknolojia,” amesema Dk. Mpango
Mkutano huo wa siku mbili unahudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa mbalimbali, watunga sera, viongozi wa taasisi na mashirika ya kimataifa, viongozi wa dini na wanataaluma.