Home BIASHARA Dirisha la Ufadhili NMB Nuru Yangu 2023/24 lafunguliwa

Dirisha la Ufadhili NMB Nuru Yangu 2023/24 lafunguliwa

Google search engine
Meneja Mkuu wa NMB Foundation, Nelson Karumuna (kushoto), akizindua rasmi dirisha la pili la Ufadhili wa Masomo kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu ‘NMB Nuru Yangu Scholarship’ uliofanyika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam leo Septemba 15, 2023. Katikati akishuhudia ni Mwenyekiti wa Bodi ya NMB Foundation inayofadhili wanafunzi hao, Ruth Zaipuna na kulia ni Mjumbe wa Bodi ya NMB Foundation, Gladness Deogratias. (Na Mpiga Picha Wetu).

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB, imefungua rasmi dirisha la pili wa Ufadhili wa Masomo na Usimamizi mwaka 2023/24, kwa wanafunzi wanaojiunga Vyuo Vikuu kupitia Programu ya NMB Nuru Yangu Scholarship and Mentorship, ambako itafadhili wanachuo 65 kwa kiasi cha Sh. Bilioni 1 gharama zinazojumuisha ufadhili wa wateule 65 wa dirisha la kwanza. Nakufanya idadi ya wanufaika kufika 130.

Ufadhili huo unatolewa kupitia Asasi ya Kiraia ya NMB Foundation, ambayo inajikita katika kusimamia na kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Sekta za Kilimo, Elimu, Afya, Mazingira na Ujasiriamali, ambapo mwaka jana ilifadhili wanafunzi 65, ambao wanaendelea na masomo katika vyuo vikuu mbalimbali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo unaoanza Septemba 15 hadi Oktoba 8, 2023, Meneja Mkuu wa NMB Foundation, Nelson Karumuna, alitaja sifa za waombaji kuwa ni ufaulu wa Kidato cha Sita wa Daraja la Kwanza pointi 3 hadi Daraja la Kwanza pointi 7, kwa wanafunzi wenye mazingira magumu na wenye changamoto.

“Ufadhili huu ambao unaenda katika maeneo ya ada, nauli, posho, stationary, mafunzo ‘field’ na laptop, unatolewa kwa wanafunzi wanaojiunga chuo katika fani za Hesabu na Takwimu, Biashara, Uchumi, Teknolojia, Habari na Mawasiliano, Uhasibu, Uhandisi, Mafuta na Gesi, Sayansi pamoja na Udaktari.

“Mwaka huu tutafadhili wanafunzi 65, hivyo kuifanya NMB Foundation kuwa na wanafunzi 130 hadi Mwaka wa Masomo wa 2023/24 utakapoanza. Programu hii pia inatoa usimamizi maalum ‘mentorship’ kuwawezesha wateule kupata ushauri, tukitarajia kuibua vipaji na kuwasaidia vijana hao kutimiza ndoto zao kielimu.

“Tunawahamasisha Watanzania wote kufikisha taarifa hizi kwa wanafunzi waliomaliza ‘form six’ mwaka huu, ambao wanajiandaa kujiunga na vyuo vikuu, kutembelea tovuti yetu ya www.foundation.nmbbank.co.tz, wajaze fomu kwa usahihi ili kuepuka makosa yanayoweza kuwatoa kwenye mchakato wasomi wenye vigezo,” alisema Karumuna.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NMB Foundation, Bi. Ruth Zaipuna, aliweka msisitizo kauli ya Meneja Mkuu wake akiwataka waombaji wahakikishe wanajaza fomu zao kwa usahihi, ili kuepuka makosa kama yaliyochangia kutopata wanafunzi 100 waliowahitaji mwaka jana, badala yake wakapata 65 tu.

“Mwaka jana tulitoa nafasi 100, lakini hadi dirisha la usajili linafungwa, tulipata wanafunzi wenye sifa 65 tu, kutokana na wengi kufanya makosa katika ujazaji wa fomu, tukajikuta wapo wanafunzi wenye sifa wameondolewa kwenye mchakato wakati walikuwa wanastahili ufadhili wetu, tunaomba makosa hayo yasijirudie.

“Watanzania watusaidie kuzifikisha taarifa hizi kwa vijana wetu, lakini tuwaombe pia wajaze fomu kwa usahihi ili tupate wanafunzi wote 65 tunaohitaji kuwafadhili mwaka huu, isijirudie makosa ya mwaka jana.

“Nia yetu sisi NMB Foundation ni kuendelea kuweka alama kwa jamii inayotuzunguka, ndio maana tunatafuta wadau zaidi wa kuungana nasi katika kufanikisha ufadhili huu kwa idadi kubwa ya wanafunzi na wanachuo wetu. Tunawaomba wadau wajitokeze kutusapoti kuwabeba vijana wetu, kwani mahitaji ni makubwa.

“Nia yetu kubwa ni kuwa chachu ya maendeleo endelevu ya vijana wa Kitanzania na jamii kwa ujumla. Pamoja na ufadhili huu wa masomo tunaowapa, NMB Foundation tutaendelea kuwatafutia wateule wetu nafasi za mafunzo kwa vitendo, sio tu hapa NMB, bali pia kwa taasisi washirika watakaoungana nasi.

“Mwisho kabisa, niwahakikishie vijana watakaoomba na Watanzania kwa ujumla, kwamba mchakato huu utakuwa wa huru, wenye usawa, haki, uwazi na umakini, ili kupata vijana wanaostahili. Tutafanikisha mchakato huu kupitia matawi yetu 230 yaliyoko kote nchini na Serikali za Mitaa,” alibainisha Zaipuna.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here