NA MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
Benki ya NMB imetunukiwa tena tuzo na jukwaa la kufadhili ujasiriamali duniani (SME Finance Forum) kutokana na huduma zake wezeshi na ufadhili wake wa kuendeleza biashara za wafanyabiashara wadogo na wakati nchini.
Ushindi iliyoupata benki hiyo kwenye tuzo za mwaka huu za ufadhili wa ujasiriamali duniani (Global Finance Awards 2023 – GSMEFF 2023) ni wa Mfadhili wa Ujasiriamali wa Mwaka upande wa Afrika uliyoipa tuzo ya fedha.
Washindi wa tuzo za mwaka huu walitangazwa wakati wa mkutano wa jukwaa hilo uliofanyika kati ya Septemba 12 na 14 huko Mumbai, India.
Kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake, tuzo za GSMEFF 2023 zinatambua dhamira na mafanikio ya taasisi za fedha na kampuni zinazojihusisha na teknolojia za huduma za kifedha (fintech) katika kuwahudumia wateja wao ambao ni wajasiriamali wadogo na wakati.
Ujumbe wa kauli mbiu ya tuzo za mwaka huu, ambayo ni “Mifumo ya Kidijitali na Mustakabali wa Ufadhili wa SMEs,” uliendana na dhamira ya NMB ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wakati kwani ulizingatia jinsi mifumo ya kidijitali inavyogusa mabadiliko ya ukuaji wa uchumi duniani.
Akizungumzia ushindi wa tuzo ya mwaka huu, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema heshima hiyo ni ushahidi mwingine wa juhudi za dhati za benki hiyo za kuziba pengo la kuwafadhili wajasiriamali nchini.
“Tuzo hii kimsingi inathamini mchango na ushiriki wa benki yetu katika kuwafadhili wajasiriamali na uwekezaji inaoufanya katika uvumbuzi wa kidijitali,” ameongeza.
NMB inazingatia maendeleo ya wafanyabiashara haa kutokana na mchango wao mkubwa katika ujenzi wa taifa kwa kutengeneza ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha mapato ya wananchi.
“Tuzo hizi na heshima tuliyopata ni ushahidi wa mwendelezo wa ubora wa huduma zetu na dhamira ya dhati ya ubunifu ya NMB,” Zaipuna alisema katika taarifa ya kuutangazia umma mafanikio hayo.
Huu ukiwa mwaka wake wa sita, tuzo za ufadhili wa ujasiriamali zilianzishwa mwaka 2018 na SME Finance Forum ambao ni mtandao wa taasisi za fedha wa kusaidia kuzikwamua kifedha biashara ndogo na za kati duniani.
Katika pongezi zake kwa washindi, Afisa Mtendaji Mkuu Matthew Gamser, amesema ushindani wa mwaka huu ulikuwa mkubwa kutokana na washiriki kuwa wengi wakitoka katika nchi nyingi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Kwa upande wake, mtu anayetarajiwa kumrithi, Qamar Saleem, amesema kuwafadhili wajasiriamali ni zaidi ya kuwasaidia kifedha kwani kufanya hivyo pia kunabadilisha maisha ya watu wengi.
SME Finance Forum, inayoratibiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) la Benki ya Dunia, ilianzishwa mwaka 2012 na nchi 20 tajiri duniani (G20) chini ya mwamvuli wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ujumuishaji wa Kifedha (GPFI).
Majukumu yake makubwa ni pamoja na kusimamia wanachama wake kubadilishana maarifa, kuchochea ubunifu na kukuza ukuaji wa wajasiriamali.