Home KITAIFA TIRA YASIMAMIA MALIPO WADAI BIMA YA BILIONI 455.80/-

TIRA YASIMAMIA MALIPO WADAI BIMA YA BILIONI 455.80/-

Google search engine

*KAMISHNA DK. SAQWARE ATANGAZA KIAMA KWA KAMPUNI ZITAKAZOVUNJA SHERIA, SASA HATARINI KUFUNGIWA, KUNYANG’ANYWA LESENI

Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk. Baghayo Saqware (kushoto) akikaribishwea na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Erick Mkuti (katikati) na kushoto ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile, leo Septemba 18, 2023 Jijini Dar es Salaam
Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk. Baghayo Saqware, akizungumza na Wahariri katika semina iliyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina leo Septemba 18, 2023
Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Khadija Said, akifafanua baadhi ya hoja kwenye semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari, iliyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina leo Septemba 18, 2023, Jijini Dar es Salaam
Baadhi ya maofisa wa TIRA wakiwa na wadau waliohudhuria semina hiyo leo
Picha mbalimbali za wahariri waliohudhuria semina iliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili leo Septemba 18, 2023 Jijini Dar es Salaam

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

KAMISHNA wa Bima nchini, Dk. Baghayo Saqware amesema kuwa kwa sasa Mamlaa ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), itaendelea kumlinda mteja ikiwa ni pamoja na kuzitaka kampuni za Bima nchini kulipa madeni ya wadai kwa mujibu wa sheria.

Hayo ameyasema leo Septemba 18, 2023, alipokuwa akizungumza kwenye semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini iliyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina nchini, ambapo amesema kuwa bado mamlaka hiyo imeendelea kuzisimamia kampuni za bima kuhakikisha zinalipa madai na fidia stahiki kwa wakati na kwa haki.

“Hadi sasa ulipaji wa madai na fidia stahiki kwa wateja wa bima yamefikia asilimia 95 hivyo kupungua kwa malalamiko. Hata hivyo asilimia 5 ya madai na fidia yana changamoto ambazo TIRA inafuatilia na kutoa suluhisho.

“Kwa mfano, ulipaji wa madai ya bima za kawaida uliongezeka kwa asilimia 10.1 kutoka Shilingi bilioni 301.9 mwaka 2021 hadi shilingi bilioni 332.09 mwaka 2022. Malipo ya madai na mafao ya bima za maisha yaliongezeka kwa asilimia 29.3 kutoka bilioni 95.7 mwaka 2021 hadi bilioni 123.71 mwaka 2022. Na jumla ya kiasi cha madai kilicholipwa mwaka 2022 ni Shilingi bilioni 455.80 hivyo, kupunguza umaskini kwa wanufaika na kufanya biashara kuwa ndelevu.

“Aidha mamlaka inaendelea na uendeshaji wa mikutano ya kupokea na kusikiliza malalamiko ya bima kwa wananchi ambapo hivi karibuni mamlaka imefanikiwa kuandaa mikutano mitano katika kanda zote za mamlaka,” amesema Kamishana huyo Bima

Pamoja na hali bado amezitaka kampuni za Bima kuhakikisha zinalipa wateja wao kwani kufanya hivyo ni kutenda kosa kisheria na wale watakaobainika watakuwa hatarini kufutiwa leseni za utoaji wa huduma za bima nchini.

Akieleza kupanda na kushuka kwa Sekta ya Bima nchini, Dk. Saqware, amesema kuwa wamepitia hatua mbalimbali ambapo kabla kabla na baada ya Uhuru, mwaka 1961 idadi hiyo ilipungua hadi kufikia kampuni 104 kutokana na Serikali kufunga baadhi ya wakala ili kudhibiti utoroshaji wa fedha kwenda nje ya nchi mwaka 1961

Kutokana na hali hiyo, Kamishna ya Bima Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA), Dk. Baghayo Saqware, anasema kuwa katika kuwezesha maendeleo ya sekta ndogo ya bima, mwaka 2009, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifuta Sheria ya Bima namba 18 ya mwaka 1996 na kutunga Sheria ya Bima Sura ya 394 ikiwa na majukumu kadhaa ikiwamo kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima

“Kuandaa na kutoa kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia soko la Bima na kurekebisha Sheria, kutoa elimu ya bima kwa Umma, kulinda haki za mteja wa Bima, kushauri Serikali kuhusu mambo ya Bima,” amesema Saqware

MUUNDO WA MAMLAKA

Dk. Saqware, amesema kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima ni Taasisi ya Muungano chini ya Wizara ya Fedha na inaongozwa na Kamishna wa Bima akisaidiwa na Naibu Kamishna na inasimamiwa na Bodi ya Taifa ya Bima inayoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi.

“Muundo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) uliidhinishwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Septemba 1, 2021. Muundo ulioidhinishwa unajumuisha Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO), Kurugenzi tatu (3), Ofisi ya Zanzibar, Ofisi za Kanda na vitengo saba.

“Ili kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake na kusogeza huduma kwa wananchi, mamlaka hadi kufikia sasa ina ofisi zifuatazo, Makao Makuu Dodoma, Ofisi ya Zanzibar, Ofisi ya Dar es Salaam, Kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Njombe, Rukwa, Iringa naSongwe).

“Kanda ya Ziwa (Mwanza, Mara, Shinyanga, Kagera, Simiyu na Geita), Kanda ya Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro na Tanga), Kanda ya Kati (Dodoma, Singida na Manyara) na Kanda ya Kusini (Lindi, Mtwara, na Ruvuma),” amesema Kamishna Dk. Saqware

Kutokana na hali hiyo Kamishna Saqware, amesema kuwa Soko la Bima linaongozwa kwa sheria, kanuni, miongozo na taratibu mbalimbali.

Amesema kuwa kati ya mwaka 2022 na 2023 Mamlaka kwa kushirikiana na wadau wa bima wamefanikiwa kuandaa Miongozo mbalimbali kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza soko la bima.

Dk. Saqware amesema kuwa miongozo hiyo ni pamoja na mwongozo wa usimamizi wa ubakizaji wa Bima na Bima Mtawanyo, mwongozo wa Bima ya Afya na usajili wa Watoa Huduma za Afya, mwongozo wa utoaji wa Ithibati kwa warekebishaji na watengenezaji wa vyombo vya moto katika sekta ya Bima.

“Mwongozo wa Uendeshaji huduma za Takaful, mwongozo wa Utoaji Huduma za Bima Kidijitali, mwongozo wa maofisa wauza Bima, mwongozo wa utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya taarifa ya kifedha kuhusu mikataba ya Bima (IFRS 17).

“Mwongozo wa Uwekezaji na Usimamizi wa Ukwasi, mwongozo wa kushughulikia madai ya Bima, mwongozo wa Uendeshaji wa Biasharaya Benki Wakala, Mwongozo wa viwango elekezi vya fidia ya Bima kwa madai ya majeraha ya mwili na vifo kwa mtu wa tatu kutokana na ajali,” amesema Kamishna Saqware

UTOAJI WA ELIMU KWA UMMA

Kamishna Dk. Saqware, amesema kuwa mamlaka inaendelea na mkakati wake wa utoaji wa elimu kwa umma kwa kushirikisha wadau wote kwenye sekta. Lengo ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania wote wenye umri wa miaka zaidi ya 18 ifikapo mwaka 2030.

Aidha mamlaka inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa utoaji elimu na uhamasishaji kwa wizara na taasisi za umma kutekeleza Sheria ya Bima Sura Na. 394 ya mwaka 2009 na Sheria ya Manunuzi Na. 7 ya mwaka 2011.

Amesema lengo mkakati ni utoaji elimu ya bima na uhamasishaji wa Serikali, Idara, Taasisi za Umma ili ziweze kuzingatia Sheria ya Bima Sura 394, kif.133 (1) hadi (3), kif.140 na Sheria ya Umma Na. 7 ya mwaka 2011, kif. 4 (2) (b).

Kamishna huyo wa Bima nchini, anasema kuwa hadi Julai 2023, Mamlaka imezitembelea Wizara za Kilimo,  Wizara ya Nishati na Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi na TAMISEMI.

KUISHAURI SERIKALI KUHUSU BIMA

Licha ya hilo lakini pia Mamlaka imeendelea kuishauri Serikali katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la ukatiaji wa bima za lazima, ukatiaji wa bima kwa mali za serikali na Bima ya Afya kwa wote.

UKUAJI WA SEKTA YA BIMA

Akieleza kuhusu ukuaji wa Sekta ya Bima nchini, amesema kuwa imekua kwa wastani wa asilimia 12.8 kwa mwaka ambapo kwa kipindi cha miaka mitano mauzo ghafi ya bima yameongezeka kutoka Sh bilioni 691.9 mwaka 2018 hadi kufikia takribani Trilion 1.2 mwaka 2022.

MCHANGO SEKTA YA BIMA KWENYE PATO

Amesema kuwa mchango wa sekta hiyo unazidi kuongezeka kutoka asilimia 0.56 kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 1.68 kwa mwaka 2021.

GAWIO

Mamlaka imeendelea kuongeza gawio Serikalini ambapo kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 TIRA imeweza kulipa gawio kwa Serikali la jumla ya Sh bilioni 2.9.

AJIRA

Sekta ya bima imechangia kwenye ajira kwa vijana ambapo hadi Septemba 2022 imetoa ajira za kudumu kwa Watanzania 4, 173.

UTEKELEZAJI WA MIRADI

Amesema mamlaka hiyo, ina mradi wa TIRAMIS na TIRA-ORS TIRAMIS na TIRA-ORS ni kifupi cha TIRA Management Information System na TIRA Online Registration System.

“Mamlaka, kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2019/2020 hadi 2021/2022, imetekeleza miradi miwili ya Mifumo ya TEHAMA (TIRAMIS na TIRA-ORS), mifumo hii yote imejengwa na watumishi wa umma. Mifumo yote miwili inafanya kazi na imesaidia kuleta manufaa kadhaa kwenye soko ikiwa ni pamoja na kurahisisha huduma za utumaji na upokeaji wa taarifa za kibima miongoni mwa wadau;

“Kurahisisha usimamizi wa biashara ya bima nchini, kuharakisha uchambuzi wa takwimu na utaoji wa taarifa,” amesema Kamishna

MAFANIKIO YALIYOPATIKANA

Amesema katika kipindi cha mwaka wa Fedha wa 2022/2023 Mamlaka imepata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na uanzishaji wa Konsotia ya Bima ya Kilimo  kama njia ya  kutekeleza skimu ya bima ya Kilimo Tanzania kwa ufanisi, Julai 1, 2023, kulizinduliwa Konsotia ya Bima ya kilimo (Agriculture Insurance Consortium).

“…uzinduzi huo ulifanyika Mkoani Tabora ambapo ulifanywa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe katika kilele cha Siku ya Ushirika Duniani (SUD). Konsotia ya Bima ya Kilimo imeanzishwa ili kuweka ufanisi katika utekelezaji wa Skimu ya Taifa ya Bima ya Kilimo (TAIS) na kuongeza uwezo wa kimtaji wa soko la bima nchini kwa ajili ya kukinga majanga kwenye sekta ya kilimo,” amesema

Dk. Saqware, amesema kuwa uanzishaji wa Konsotia ya Bima ya Mafuta na Gesi Tanzania, ambayo ilizduliwa Novemba 16, 2022 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Hamad H. Chande.

“Vihatarishi vyote vya nishati vinavyotoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama vile vihatarishi kutoka kwa mradi wa LNG vitakatiwa bima kupitia Konsotia ya bima ya nishati ya mafuta na gesi Tanzania

“Mantiki ya kuanzisha konsotia ni kuhakikisha miradi yote ya gesi na mafuta inabakiza sio chini ya asilimia 45 ada zitokanazo na gesi na mafuta kutokana na kutokuwa na uwezo wa soko la ndani, vihatarishi vya nishati, vilielekezwa nje ya nchi kwa asilimia 100, jambo ambalo sio na lisilo na tija kwenye uchumi wa nchi.

Kuanzishwa kwa miradi mikubwa ya nishati kama vile bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ni fursa kwenye sekta ya bima kujipanga kwa ajili ya kuongeza tija, uchumi na ajira nchini.

“Malengo ya kuanzisha konsotia ni kutoa fursa kampuni za bima za ndani kushiriki na kuandika vihatarishi vya nishati ya Gesi na Mafuta ndani ya nchi, kushiriki katika bima ya mradi wa LNG, unaokadiriwa kuwa na gharama ya uwekezaji wa Dola za Kimarekani Shilingi Bilioni 40,” amesema

UTEKELEZAJI WA KONSOTIA HADI SASA

Dk. Saqware, amesema kuwa Kampuni 22 za Bima zimesaini Mkataba wa Muungano huo wa Bima ya Nishati ya Mafuta na Gesi Tanzania zenye jumla ya laini (hisa) 238;

Hata hivyo anazidi kuweka wazi kwamba kila laini (hisa) ina thamani ya Dola za Kimarekani (USD) 25,000 ambayo ni jumla ya uwezo wa muungano wa kiasi cha mtaji cha wa Dola za Marekani 6,000,000;

“Konsotia itasimamiwa na kampuni ya bima Mtawanyo ya Tanzania Reinsurance Company Limited (Tan Re); Kampuni ya Bima ya Phoenix ya Tanzania ni kampuni Kiongozi (leader) wa konsotia, Kamati ya Kiufundi ya Konsotia imeundwa na wanachama kutoka makampuni 10 ya bima (yaani Phoenix, Shirika la Bima la Taifa (NIC), Jubilee, Britam, Heritage, Reliance, UAP, Alliance Insurance Corporation, Tanzania, na Shirika la Bima la Taifa (ZIC);

“…wajumbe wa kamati wana idadi ya laini (hisa) kuanzia 5 mpaka 95 katika muungano wao. Ambapo faida za moja kwa moja za Konsotia kwa nchi yetu pamoja na kuhakikisha miradi yote ya gesi na mafuta inabakiza sio chini ya asilimia 45 ada zitokanazo na gesi na mafuta,” amesema Dk. Saqware

MIPANGO IJAYO YA MAMLAKA 2025/26

Kamishna huyo amesema kuwa TIRA kwa kushirikiana na wadau wa Bima inaendelea na utekelezaji wa mipango na mikakati ya Taifa ambayo ni pamoja na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa (FYDPII-2020-2025), Mpango Mkuu wa Taifa wa kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini (FSDMP 2020-2030), Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025), Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar pamoja na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan wakati akilihutubia Bunge mwezi April 2021.

Licha ya hilo pia kupokea na kufanyia kazi maelekezo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi

TAKWIMU BIMA

Kuunganisha mifumo ya kidigitali na Taasisi mbalimbali za umma ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, LATRA, NIDA, TASAC, TRA, PTA, ZRA.

Amesema lengo ni kuongeza usimamizi na maendeleo ya soko la Bima na kuendelea na utoaji wa elimu ya bima kwa umma na wadau mbalimbali.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here