Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, LINDI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amendika historia mpya katika sekta ya uvuvi baada ya kuweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambayo haijawahi kuwepo tangu nchi ya Tanzania ipate uhuru.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe hilo la msingi leo Septemba 19, 2023 kuashiria ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa katika tukio lililofanyika Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Kukamilika kwa bandari hiyo kutawezesha meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Pia, uwepo wa bandari ya uvuvi utachochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi. Hivyo, uwekezaji huu, unaenda kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kutoka tani 40,721.53 zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 249.54 hadi tani 52,937.99 na kuchangia takriban asilimia 10 katika pato la Taifa ifikapo mwaka 2036.
Aidha, Bandari hiyo inatarajiwa kutengeneza ajira kwa watanzania takriban 30,000 huku katika hatua za awali za ujenzi, jumla ya ajira za muda mfupi 278 zimetolewa ambapo kati ya hizo ajira 106 sawa na asilimia 38 zimetolewa kwa wakazi wa wilaya za Mkoa wa Lindi.
Pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya Uvuvi, Rais Samia pia amegawa boti 34 kati ya boti 160 ambazo zinatolewa nchi nzima. Boti hizi kwa ukanda wa bahari ya Hindi zipo 92 zikihusisha wavuvi na wakulima wa mwani.
“Serikali imejipanga kuhakikisha mazingira ya wavuvi na wakuzaji viumbe maji yanaimarika ndio maana leo nimegawa boti za kisasa zikiwa na kifaa cha kuonyesha upatikanaji wa samaki na uhifadhi wa samaki”, alisema Mhe. Dkt. Samia
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amemshukuru Rais Samia kwa namna ambavyo ameiwezesha sekta ya Mifugo na Uvuvi kwa kuiongezea bajeti.
Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kuamua kutekeleza ujenzi wa mradi huo ambao utakuwa na tija kwa wananchi wa Kilwa na Tanzania kwa ujumla.
Ulega amesema ujenzi huo wa bandari ambao unagharimu zaidi ya bilioni 266 unakwenda kujibu changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi, lakini pia kuleta fursa za ajira zisizopungua 30,000. Ujenzi huu utawezesha ujenzi wa Viwanda vya kuchakata samaki, karakana ya kutengeneza meli, sehemu ya kuhifadhi samaki na uzalishaji wa barafu.