Home KITAIFA JOKATE MBIONI KUJA NA MWELEKEO MPYA UWT

JOKATE MBIONI KUJA NA MWELEKEO MPYA UWT

Google search engine

AOMBA USHIRIKIANO WA WANAWAKE, ASIMULIA SAFARI YAKE KISIASA

Katibu Mkuu wa UWT, Jokate Mwegelo, akisindikizwa na wanachama wa jumuiya hiyo mara baada ya kuwasilisi katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba Jijini Dar es Salaam. Wa mbele ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT, Asha Feruzi
Katibu Mkuu wa UWT, Jokate Mwegelo, akilakiwa na wanachama na viongozi mbalimbali wa jumuiya hiyo leo

NA MWANDISHI WETU

-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu mpya wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT), Jokate Mwegelo, amesema kuwa kwa sasa anajipanga na muda mfupi ujao ataeleza mwelekeo wa UWT kwa Watanzania.

Kutokana na hali hiyo amesema kuwa kwa sasa anaingia kwenye UWT ambayo ina inaongozwa na kina mama shupavu Mary Chatanda na Makamu wake Zainabu Shomari ambao wamekuwa wakichanja mbuga kutokana na hostiria yao iliyotukuka ndani ya CCM.

Jokate anakuwa Mtendaji Mkuu wa nane wa umoja huo wa wanawake, ambapo tangu ilipoanzishwa kwake ambapo makatibu wakuu waliotangulia kuongoza jumuiya hiyo muhimu ya CCM ni Leah Lupembe, Kate Kamba, Halima Mamuya, Hasna Mwilima, Amina Makilagi, Mwal. Queen Mlozi, Dk. Philis Nyimbi na sasa Jokate Mwegelo.

Akizungumza leo Oktoba 4, 2023 wakati wa hafla ya mapokezi yaliyoandaliwa kwa ajili yake, yaliyofanyika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM Lumumba, jijini Dar es Salaam, Jokate, amesema kuwa anaamini kazi yake itakuwa nyepesi kutokana na viongozi wake kwa namna walivyofanyakazi za kuijenga UWT nchini.

“Jumuiya hii kipindi hiki imepata bahati ya kuongozwa na kinamama shupavu, Mama yetu Marry Chatanda na Makamu wake Zainabu Shomari wanachanja mbuga kwelikweli na wote hawa wana historia za utumishi ndani ya chama na kwenye Jamhuri kwahiyo mimi nina imani kazi yangu itakuwa nyepesi sana kwasababu naingia kwenye Jumuiya ambayo imejipanga, imejidhatiti na imejipambanua, kwahiyo sisi kwa pamoja ndio askari wake ambao tunakuwa na nguvu na kasi ya kuhakikisha kwenye chaguzi zinazokuja tunamuheshimiwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Sasa leo nilipita tu kwenye ofisi zetu hapa kwa ajili ya kuchukua barua za uteuzi ili niridhie kupokea jukumu hili ambalo nimepatiwa lakini kama alivyosema Naibu Katibu Mkuu wetu kutakuwa na mapokezi rasmi ambayo yatafanyika wiki ijayo Oktoba 12.2023 kwenye makao makuu ya nchi lakini Makao Makuu ya chama (Dodoma).

“… nadhani tukiwa kule tutaweza kuongea kwa kirefu lakini pia nitaweza kuongea zaidi baada ya kukabidhiwa Ofisi rasmi na kuweza kupitia mipango mbalimbali, namimi nitakuwa na uwezo sasa wa kuja kwenu na kueleza muelekeo wa UWT utakuwa ni upi,” amesema Jokate

Katibu Mkuu huyo mpya wa UWT, ametumia mkutano huo kueleza kwamba yeye ni zao la CCM ikiwamo kusomeshwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Mimi ni zao la Chama cha Mapinduzi (CCM) lakini pia nimesomeshwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hapa namaanisha uwezo wangu wa kusoma umetokana na sera nzuri zilizowekwa na CCM ambazo zimeniwezesha kupata elimu ambayo naitumia sasa hivi kuwatumikia Watanzania wenzangu. Niko hapa kwa niaba yenu siko hapa kwaniaba yangu binafsi.

“Nilivyokuwa Pwani kuna msemo walikuwa wanausema zilongwa mbali zitendwa mbali na walikuwa wananiona kadogo kadogo lakini nilivyoenda Korogwe kwa Wasambaa walikuwa na msemo wao mmoja ambao ulikuwa unamaanisha ukienda kwenye ngoma ucheze vizuri kwa maana wenzako wanakuona kwa hiyo naishukuru Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu kwa kuniona na nadhani nilicheza vizuri.

“Kwa maana hata ninyi kuwepo hapa wengi ambao nimefanyanao kazi kuanzia Kisarawe, Temeke, Korogwe na kwingine kote nadhani tuliishi vizuri ndio maana mmefika hapa, lakini zaidi nitumie fursa hii kuwashukuru saana kwa malezi yenu, mngeamua kunikunjia nisingeweza kufanya yale ambayo nimeyafanya mngeamua tu nisingefanikiwa hapa.

“… lakini kwa sababu ya ushirikiano ambao mmenipatia iliniwezesha mimi kuwa na wepesi wa kutekeleza majukumu yangu na dhamana ambazo nimepetiwa na nchi yetu basi mafanikio yangu na ninyi mna sehemu kubwa kwelikweli,” amesema

Kutokana na hali hiyo Katibu Mkuu huyo wa UWT, amechukua mikoba ya Dk. Philis Nyimbi, ameelza wazi matumaini yake hasa kutokana na ushirikiano walionao wanawake ndani ya CCM.

“Kwa hiyo kikubwa ndugu zangu ninachoomba kutoka kwenu, unaweza kuwa na maono mazuri lakini ukikosa ushirikiano ni kazi bure lakini mimi kwenye hilo sina shaka maana ninyi wote ni mashahidi jumuiya hii kipindi hiki imepata bahati ya kuongozwa na wakinamama shupavu wenye historia njema kwenye utumishi ndani ya chama na kwenye Jamhuri,” amesma Jokate

Hatua hiyo ya kupewa Jokate kama mtendaji mkuu wa jumuiya hiyo inatarajiwa kwenda kuifanya jumuiya kuwa na mchanganyiko ambao huenda ikasaidia kuwa mvuto machoni mwa watanzania kwa kuonekana inamchanganyiko wa wanawake wa kila rika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba Mosi, 2023 na Katibu Wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Sophia Edward Mjema, ilieleza kuwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyokutana katika kikao chake maalum, Oktoba 1, 2023, jijini Dar es Salaam, imefanya uteuzi wa makatibu wakuu wa Jumuiya za Umoja wa Wanawake (UWT) na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Katika kikao hicho, Kamati Kuu kimemteua, Jokate Mwegelo, kuwa Katibu Mkuu wa UWT, kabla ya uteuzi huo, Mwegelo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here