*Mazingira ya Uwekezaji Sekta ya Madini kuboreshwa
Na MWANDISHI WETU
Wizara ya Madini imeweka Mipango ya kuhakikisha Sekta Madini inafungamanishwa na mipango ya taifa ili kuwa na Matumizi yenye tija katika rasilimali za nchi hususan katika Sekta ya Madini.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 4, 2023 na Waziri wa Madini Anthony Mavunde alipokutana na Waziri Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wakati wa kikao kifupi kilicholenga kujenga uhusiano mzuri ya uwekezaji nchini Ofisi za Wizara ya Madini Jijini Dodoma.
Amesema ushirikiano wa Wizara hizo mbili utaimarishwa ili Sekta ya Madini iweze kuingizwa katika mipango yenye tija kwa taifa na hatimaye kukuza uchumi wa madini.
Mavunde amesisitiza kuwa madini ni sayansi hivyo Sekta ya Madini itahakikisha inafanya utafiti wa madini nchini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kuvutia wawekezaji nchini.
“Lazima tupate taarifa sahihi za madini yaliyopo nchini hususan kwenye mahitaji makubwa ya madini muhimu na madini mkakati ili madini hayo tuyachimbe kwa kiasi kikubwa nchini,” amesema Waziri Mavunde.
Kwa upande wake Profesa Kitila Mkumbo, amesema Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji inaratibu na kuweka mazingira mazuri yanayoratibika kwa uwekezaji katika Taasisi za Umma
Kuhusu madini muhimu na madini mkakati, Prof. Kitila amesisitiza mahitaji ya madini hayo duniani iwe chachu kwa Tanzania kutumia fursa hiyo katika kujenga mazingira bora ya kiuchumi ikiwa pamoja na kuibua maeneo mapya ya uwekezaji.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini, Angelo Haule amesema mapendekezo ya Vipaumbele kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 ni kuendelea kufanya utafiti wa jiofizikia kwa kutumia ndege (High Resolution Airborne Geophysical Survey) na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji maduhuli na utoaji wa leseni.
“Tutaimarisha uwekezaji na Teknolojia katika Sekta ya Madini ili kuendeleza madini muhimu na madini mkakati katika kuhamasisha uwekezaji, biashara na uongezaji thamani Madini,” amesisitiza Haule.
Naye Mtendaji Mkuu wa GST, Dk. Mussa Budeba amesema kuwa kama Dira 2030 ya Wizara Madini ni Maisha na Utajiri Sekta ya Madini itafanya utafiti ili kufikia maeneo mengi nchini na kuwawezesha wachimbaji wadogo kuchimba kwa tija badala ya kubahatisha.
Kikao pia kimehudhuriwa na watendaji mbalimbali kutoka wizara hizo mbili na kwa pamoja wameahidi kushirikiana ili kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini.