Home KITAIFA MAJALIWA AZUIA KAMPUNI BINAFSI UPIMAJI ARDHI DODOMA

MAJALIWA AZUIA KAMPUNI BINAFSI UPIMAJI ARDHI DODOMA

Google search engine

*AAGIZA VIBARUA WENYE NYARAKA ZA JIJI WAKAMATWE, WACHUKULIWE HATUA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jery Silaa, akiwa na viongozo wa wizara yake katika kikoa hicho

Na MWANDISHI WETU

-DODOMA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kampuni zote zilizopewa kazi za upimaji wa viwanja kwenye Jiji la Dodoma na zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo, ziwe zilikuwa na mikataba ama hazikuwa na mikataba zichukuliwe hatua kali za kisheria.

Agizo hilo amelitoa leo Oktoba 6, 2023 kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo na kutafuta suluhisho.

“Moja kati ya hatua hizo, ni kuziblacklist kwa sababu makampuni hayo yapo, tutumie makampuni ambayo yana uaminifu badala ya kutumia makampuni ambayo yanatuzalishia migogoro.

“Tunatambua makampuni mengi hapa Dodoma ni ya watumishi wenyewe kama ambavyo imeelezwa kwenye ripoti. Mkurugenzi alikuwa na kampuni mbili, Mhasibu wake ana kampuni yake na wanazitumia kupima maeneo, kwa hiyo ni miradi yao,” amesema Majaliwa

Kutokana na hali hiyo Waziri Mkuu, aliwaagiza wakuu wa mikoa wahakikishe kuwa Kamishna Msaidizi wa Mkoa, maofisa Mipango Miji wa Majiji, Halmashauri na Manispaa hawana sababu ya kuchukua watumishi wa muda kufanya kazi ya upimaji bali wafanye wao ili kuepusha mianya ya rushwa.

Pia aligiza watafutwe na kukamatwa vibarua ambao wanatembea na nyaraka za Serikali na kuuza viwanja kwa niaba ya maofisa wa Jiji.

“Bwana Justin Albert, Freddy Mathias, Elias na Magige watafutwe, wachunguzwe na vyombo vya dola kuhusu nyaraka za Serikali walizonazo, na wazirejeshe nyaraka za Serikali wanazozitumia vibaya kwa kuendelea kuuza viwanja maeneo ya Jiji ya Ukanda wa Kijani, Mkonze, Ndachi, Chinyika, Ng’ong’ona na Mkalama.

“Hawa ni vibarua, lakini wana ramani na wanavijua viwanja vyote. Wao wanachofanya ni kufanya mauzo halafu wanapeleka kwa watu wao pale Jiji na hati zinatoka. Kwa hiyo, watafutwe na wanyang’anywe zile nyaraka ili wasiendelee kuuza viwanja,” aliagiza.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here