Na BEATUS MAGANJA
-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inashiriki maonesho ya Saba ya Kimataifa ya Swahili International Tourism Expo S!TE yaliyozinduliwa Leo Oktoba 6, 2023 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam
Wanunuzi wa bidhaa za utalii kutoka masoko ya kiutalii ya kimkakati zaidi ya 71, waoneshaji wa kimataifa zaidi ya 150 pamoja na mawakala wa utalii kutoka nchi mbalimbali duniani wanashiriki maonesho haya yenye kauli Mbiu “Utalii Unaowajibika Kwa Maendeleo Jumuishi”
TAWA inatumia maonesho haya kunadi fursa za uwekezaji zinazopatikana katika maeneo yake mapya ya kimkakati ya kiutalii kama vile visiwa vya Lundo vinavyopatikana wilaya ya Nyasa pamoja na eneo la Makuyuni Wildlife Park (Monduli – Arusha) lililokabidhiwa na Serikali kwa taasisi hii tarehe 03 Oktoba, 2023
TAWA inanadi bidhaa zake zake za kipekee za Utalii wa picha zinazopatikana katika Mapori ya Akiba ya Pande (Dar es Salaam), Wamimbiki (Pwani), Mpanga/Kipengere (Njombe na Mbeya), Kijereshi (Simiyu) sanjari na Utalii wa Uwindaji unaofanyika katika maeneo mengi yaliyo chini ya Usimamizi wa taasisi hii nchini
Utalii wa bahari ni mojawapo ya mazao ya kipekee ya utalii kwa taasisi ya TAWA katika ukanda wa Kusini Mashariki ambalo linapigiwa chapuo katika maonesho haya kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na TAWA katika hifadhi urithi wa utamaduni wa dunia, magofu ya kale ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara
Pia, TAWA inauza fursa za utalii wa picha katika maeneo ya uwekezaji mahiri (SWICA) ambayo yametengwa na Serikali kama vile maeneo ya Mapori ya Akiba Selous, Ikorongo Grumet, Maswa, Mkungunero na mengine.
Pamoja na utalii katika maeneo hayo TAWA inatangaza pia fursa za uwekezaji katika eneo jipya la hewa ukaa.
Maonesho haya yanategemea kufikia tamati Oktoba 8, 2023