Na MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya maboresho makubwa katika mifumo ya TEHAMA kwa lengo kuongeza ufanisi, uwajibikaji, uwazi pamoja na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Miongoni mwa maeneo ambayo yamefanyiwa maboresho hayo ni katika stempu za Kodi za kieletroniki (ETS).
Kutokana na maboresho hayo yanayofanywa na TRA hivi karibuni timu maalum ya ukaguzi iliyoongozwa na Meneja wa ETS Ayubu Tweve iliitembelea Kampuni ya Double Diamond Holdings Limited inayomilikiwa na Pardeep Singh Sindhu iliyopo Njiro katika mkoa wa kikodi wa Arusha.
Kampuni hiyo inayojihusisha na uzalishaji wa Pombe kali aina ya the The Ace of Diamond Gin na The Ace of Diamond Pineable na katika ukaguzi huo ilibainika kulikuwa na katoni 666 zikiwa zimebandikwa stamp zinazodhaniwa kuwa za kughushi pamoja na reel moja ya stamp inazodhaniwa kuwa ni ya kughushi.
Aidha timu maalum ya ukaguzi libaini pia kulikuwa na katoni 995 zikiwa zimezalishwa muda mrefu lakini hazijabandikwa stamp kinyume na utaratibu.Tayari mtuhumiwa amefikishwa katika vyombo vya usalama kwa hatua zaidi
Akizungumzia maboresho hayo Meneja Mfumo Eva Raphael amesema
mfumo huo wa stempu za kielektroniki umeunganishwa na mifumo ya TRA ili kupata takwimu sahihi za uzalishaji/uagizwaji kwa maana ya idadi, ujazo pamoja na ubora na viwango vya bidhaa.
Aidha TRA imewafahamisha wananchi wanaotumia bidhaa hizo kushiriki kulinda afya zao kwa kutambua bidhaa halisi na halali kwa matumizi yao.
Pia kutokana na wakusanya kodi kukabiliwa na changamoto ya kujua viwango vya kweli vya kodi kwa uzalishaji uliopo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilifikiria kutafuta njia nyingine ya kisasa na sahihi ili kukabiliana na changamoto hiyo.