*SASA ADAIWA KUINGIZA MIZIGO KWA MAGENDO
Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema kuwa haina mfumo wowote mwingine inaouendesha wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo wa Forodha wa TANCIS ambao unatumika kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kutokana na hali hiyo sasa ni wazi inaoneka kugeuka kwa kibao dhidi ya mfanyabishara Emmanuel Gadi ambaye hivi karibuni kupitia video alishusha tuhuma nzito dhidi ya TRA akidai kwamba wametengeza mfumo wa kukusanya mabilioni ya fedha kama ilivyokuwa kwa watumishi wa Tamisemi mkoani Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 12, 2023 Jijini Dar es Salaam na Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Stephen Kauzeni, amesema kuwa taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu malalamiko ya Emmanuel Gadi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Wintech Tanzania Ltd anayedai kuwa, TRA imetengeneza mfumo wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo halali wa Serikali kinyume na Sheria ya Forodha.
Amesema kutokana na uchunguzi wa kina walioufanya TRA wamebaini uwepo wa viashiria vya ukwepaji kodi kwani ni dhahiri kuwa mzigo wake uliingizwa kwa njia za magendo.
“Bwana Emmanuel Gadi alifikisha malalamiko yake kwa njia ya barua tarehe 27 Februari, 2023 akidai kupewa uthibitisho na TRA wa kuingiza mzigo wa vifurushi 471 vya Toner Cartridges kupitia kampuni ya Tosh Logistics Ltd.
“TRA ilifanya Uchunguzi wa kutosha na kuthibitisha kwamba hapakuwa na mzigo wowote ulioingizwa nchini kwa jina la Wintech Tanzania Ltd wa vifurushi 471 vya Toner Cartridges kupitia kadhia yenye namba TZDL – 22-1382193 ya tarehe 18 Agosti 2022 kama anavyodai,” amesema Kauzeni.
Ameongeza kuwa, TRA ilimjibu mhusika kupitia barua yenye kumbukumbu namba CF 8/92/01 ya tarehe 25 Julai 2023 ikimjulisha kuwa, kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa House Bill of Lading na kutoonekana kwa mzigo huo kwenye kadhia iliyowasilishwa na kampuni ya Tosh Logistics Ltd, TRA isingeweza kuthibitisha kuingizwa kwa mzigo huo nchini.
“Kupitia taarifa ya Bwana Emmanuel Gadi aliyoitoa kwenye vyombo vya habari, tumebaini kuwepo kwa viashiria vya ukwepaji kodi kwani ni dhahiri kuwa mzigo wake uliingizwa kwa njia za magendo,” ameeleza Meneja Kauzeni.
Meneja huyo wa Elimu kwa Mlipakodi amemtaka mlalamikaji kuwasilisha nyaraka na uthibitisho wa Kampuni yake kuingiza mzigo huo nchini mara moja ili hatua stahiki zichukuliwe.
Hivi karibuni mfanyabiashara Emmanuel alitoa video kupitia mitandao ya kijamii ambapo amesema “Ndugu zangu wafanyabishara wenzangu natengeneza video hii kama barua wazi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan naomba atusaidie namuonyesha matatizo na ufisadi unaoendelea kwenye forodha TRA.
“Mimi nikiwa mfanyabishara naitwa Mr. Emmanuel Gadi namba yangu ya mlipakodi…. TRA wametengeza mfumo wa uingizaji mzigo nchini kinyume na sheria za forodha tangu mwaka 2018 hili ndilo muhimu kabisa nilitaka Rais Samia Suluhu Hassan alijue mfumo huu umenana kabisa na ule mfumo waliotengeneza wale wafanyakazi wa Tamisemi Mbeya ambao walitengeza mfumo nje ya mfumo wa Serikali.
“Hivyo TRA nao wametengeza mfumo wa kuingiza mizigo nchini, mfumo upo kinyume na sheria za forodha naamini kabisa kwa ajili ya makusudi ya kujikusanyia mapato yao na mabilioni ya hela yanapotea . TRA naacha ushuru wa milioni 400 karibuni kwa ajili ya kujificha makosa yake ananisababishia mimi hasara ya milioni 968 sasa kwa ajili ya kuficha makosa ya TRA tu.
“Kwa nini iwe hivyo TRA imefanya makosa naomba nirekebishiwe niko tayari kulipa ushuru wa milioni 400 nirekebishiwe document zangu (nyaraka)ili kampuni ya Riyadhi Jubilee ikalilipe, nasi tunasubiri document hizo tu tangu mwaka 2018 wametengeneza utaratibu,” amesema Gadi