Na MWANDISHI WETU
-LINDI
KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema, amewasihi Watanzania kutunza amani ya nchi pamoja na kulinda tunu za Taifa.
Ameyasema hayo Oktoba 17, 2023 alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Kata Sudi, Lindi Vijijini mkoani hapa, ambapo amesema kuwa Watanzania wana wajibu wa kuimarisha umoja na mshikamano.
“Amani ya nchi tuitunze ndugu zangu, kuna nchi nyingine mtoto anazaliwa hadi anazeeka ni milio ya mitutu tu, maendeleo yanapatikana katika amani,” amesema Mjema.
Mjema ambaye alikuwa mkoani Lindi kuendesha mafunzo ya falsafa, itikadi na sera za CCM kwa viongozi na watendaji wa CCM, amesema demokrasia itumike kuimarisha amani.
Amesema fursa ya demokrasia nchini inatokana na uongozi makini wa CCM, na kimekuwa kikiitekeleza ndani ya chama kwa vitendo.
Amewataka wananchi kuchuja maneno wanayoambiwa au kuyasikia kutoka katika majukwaa ya siasa.
Amesema wako wanasiasa wanasema uongo na kuwataka wananchi waachane nao.
Kutokana na hali hiyo, wananchi ni mashahidi kwamba chini ya uongozi mahiri wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, nchi inasonga mbele katika maendeleo.
Amesema katika kipindi kifupi, tangu amekuwa Rais, maendeleo makubwa katika kila sekta yamepatikana.
“Vituo vya afya, shule, maji, barabara, umeme, taja chochote, hakuna kilichosimama, mabilioni ya fedha yanashuka hadi vitongojini,” amesema.
Mjema amesema katika uchaguzi mkuu wa 2020, CCM iliahidi maendeleo kwa Watanzania na sasa inatekeleza.
“Usidanganywe na mtu, CCM imeahidi imetekeleza na kazi inaendelea,” amesema na kuongeza kwamba “mtu ukimpa nafasi akakudanganya, maana yake anakudharau.”