Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
MKOA wa Dar es Salaam umezindua rasmi program ya kukagawa vyandarua zaidi ya 700,000 katika shule zote za msingi huku Mkuu wa mkoa huo, Albert Chalamila akitoa maelekezo kwa sekta ya afya kuhakikisha wanapuliza dawa ya kuua mbu katika maeneo yote lengo likiwa kukabiliana na ugonjwa wa Malaria.
Uzinduzi wa program ya kugawa vyandarua umefanyika leo Oktoba 18,2023 jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na wadau mbalimbali wa mkoa huo wakiwemo wataalam kutoka sekta ya afya ngazi ya Wilaya, Mkoa na Wizara na ugawaji wa vyandarua hivyo utafanywa na Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam kuanzisha kesho.
Akizungumza Oktoba 18,2023 wakati wa uzinduzi ugawaji vyandarua kwa shule za msingi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema Taifa lolote linalojiandaa kukua kiuchumi hujidhatiti lisipate madhara katika rasilimali watu.
“Leo Tanzania tunazungumzia malaria, lakini historia inaonesha nchi kama Marekani mgonjwa wa mwisho kuumwa malaria ilikuwa mwaka 1950 lakini zaidi pia hapa kwetu Tanzania Bara na Zanzibar tumeshapishana sana katika udhibiti wa malaria kwani Zanzibar wamejitahidi kudhibiti Malaria.
“Nitoe maelekezo na mwito wangu kwa wataaam wote wa sekta ya afya na wadau kuhakikisha wanaendelea na dhamira ya kugawa vyandarua lakini wakati huo huo kuongeza kasi ya kudhibiti mbu kabla ya kufikia hatua ya kupevuka.
“Wakati tukiendelea na jitihada hizi tunafahamu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuita wawekezaji kuja kuwekeza na miongoni mwa wawekezaji hao tunao wenzetu kutoka Cuba ambao wamewekeza kaika kiwanda cha kutengeneza dawa ya viua dudu.
“Hivyo tunaweza kununua na kupuliza maeneo yote na sasa hivi tuna program ya kuipendezesha Dar es Salaam na tunaelezwa kuwa mpaka kufika mwaka 20250 Jiji hili litakuwa moja ya majiji makubwa saba katika Afrika.
“Itakuwa aibu katika Jiji ambalo linawekwa katika orodha ya majiji saba makubwa halafu watu wake wanaugua na kufariki dunia kwasababu ya malaria.Niombe watalaam wa afya tusaidiane na huu ndio muda wa kusema Dar es Salaam na Tanzania bila malaria inawezekana.”
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dk. Rashid Mfaume amesema ugonjwa wa Malaria bado ni tatizo katika nchi yetu na hata yale maeneo ambao wanaona kabisa ni ya maambukizi yako chini ya asilimia 3.5 lakini kuna baadhi ya maeneo hali ya maambukizi yako juu.
“Upande wa Dar es Salaam tumeona maeneo ya Luhanga na Tungi Songani maambukizi yako juu.Kwa hiyo ni wajibu wetu kufahamu malaria bado ni tatizo lakini kuna maeneo mahususi ambayo ni kero kubwa kwa Malaria.
“Hakuna mdudu anayeishi muda mfupi kama mbu kwani mbu mpevu haishi zaidi ya wiki mbili lakini ukimsubiria mbu apevuke hasa mbu wa kike anaweza kutaga mayai 100 mpaka 200, hiyo ndio shida yake.Hivyo hii ya kugawa vyandarua ni afua mojawapo lakini tunahamasisha na afua nyingine za kupambana na malaria kama kusafisha mazingira.
“Hata hivyo tukisubiria mbu awe mpevu itakuwa changamoto , hivyo tutokomeze mapema.Nitoe maelekezo kwa wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam kwenda kupuliza dawa katika mazalia ya mbu na lengo la kufanya hivyo ni kupambana na mbu katika hatua za awali kabisa kabla hajakuwa mpevu.
Dk. Mfaume amesema kuna haja wakati wa kuandaa bajeti ya fedha kuwa na bajeti kwa ajili ya afua ya kupambana na malaria kwa kutokomeza mbu lakini viongozi wa dini wasaidie kuhamasisha utumiaji vyandarua katika kaya hasa kwa watoto ambao ndio walengwa wa vyandarua hivyo.
Awali Frank Mpembeni ambaye alimwakilisha Meneja wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam, amesema usambazaji vyandarua katika mkoa wa Dar es Salaam utafanyika katika wilaya zote tano Ubungo,Kigamboni, Temeke, Kinondoni na Ilala huku akifafanua kazi ya MSD katika program hiyo ni kupokea vyandarua , kutunza na kusambaza.
Aidha amefafanua Ubungo watagawa vyandarua 122,116 katika shule 194, Wilaya ya Kigamboni vyandarua 44,311 katika shule 77, Wilaya ya Temeke vyandarua 180,843 katika shule 152, Wilaya ya Kinondoni vyandarua 106,123 katika shule 175 wakati Ilala itapewa vyandarua 255,725 katika shule 280 na hivyo kufanya jumla ya vyandarua vitakavyogawiwa ni 709,118.
“Katika usambazaji tutatumia magari makubwa ya kuanzia tani tano, 10 na tani 15, pia tutatumia magari madogo kwenye maeneo ambayo magari makubwa hayawezi kufika kwa urahisi.Hivyo tunatarajia kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wote kuanzia ofisi ya Mkuu wa mkoa mpaka wakuu wa shule,” amesema