Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM
BANDARI ya Dar es Salaam ndio lango kuu ya uchumi nchini Tanzania, haitoi huduma kwa Tanzania pekee, kutokana na umuhimu wake pia inahudumia nchi jirani zisizo na bahari zinatumia bandari hiyo kama Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.
Kwa mujibu wa taarifa zinaeleza kuwa watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam, wameongezeka ndani ya mwaka mmoja ambapo wanahudumia magari kati ya 250,000 hadi 300,000 na asilimia 60 ya magari hayo, ni ya nchi Jirani.
Kwa mujibu wa tovuti ya bandari hiyo, asilimia 95 ya biashara za kimataifa za Tanzania, zinahudumiwa na Bandari Dar es Salaam. Bandari hiyo inaunganisha Mashariki ya Kati, Mashariki ya Kati, Ulaya na Marekani.
Mwaka 2019/2020 makusanyo ya Bandari ya Dar es Salaam, yalikuwa shilingi bilioni 901, mwaka 2020/2021 ilikusanya shilingi bilioni 896, na mwaka 2021/2022 katika robo ya kwanza ilikusanya shilingi bilioni 980 hadi mwisho wa mwaka.
Hadi hapo mambo yanaonekana kwenda vizuri. Ila upande mwingine wa shilingi, bandari hii ina changamoto zake vilevile – nyingine ni za muda mrefu. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kila wakati amekuwa akizungumzia matatizo ya Bandari ya Dar es Salaam hasa kutokana na kukosekana kwa ufanisi kwenye eneo la usheleweshaji wa mizigo na ukosefu wa teknolojia za kisasa ambazo zitakuwa zimeunganishwa na mamlaka nyingine badala ya kuwepo na usumbufu kwa wateja kuhangaika kwenye kila idara.
“Siridhishwi kabisa na kasi za bandari, siasa zilizoko, longolongo zilizoko, mabandari yanaendeshwa kwa kasi kubwa duniani, na biashara zinakuwa kwa kasi kubwa kupitia bandari, sisi bado tunasuasua. Wawekezaji wanakuja, wanazungushwa mwanzo mwisho,” Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Julai 4, 2022.
Katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita takribani wakurugenzi sita wa bandari ya Dar es Salaam, wameteuliwa na kutumbuliwa, kwa sababu mbali mbali – ukiwemo utendaji mbovu na ubadhirifu wa fedha.
Ripoti ya Takukuru iliyotolewa Machi mwaka 2023, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Kamishna Salum Hamduni alisema kutosomana kwa mifumo ya mamlaka ya bandari (TPA) na mamlaka ya mapato (TRA), ni moja ya viashiria vya rushwa.
“Tatizo la mifumo katika bandari limekuwepo kwa siku nyingi. Bandari ni lango kubwa la uchumi lenye uwezo wa kuchangia hata nusu ya bajeti ya serikali, lakini inashangaza pato lake haliinuki,” alisema Rais Samia katika hafla ya kupokea ripoti hiyo.
Changamoto za Bandari ya Dar es Salaam
Taarifa ya utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam imeonesha kutofikiwa malengo ya kiutendaji katika maeneo ya shehena inayohudumiwa na mapato yanayokusanywa. Kutofikiwa kwa malengo hayo kunasababishwa na changamoto mbalimbali zikiwemo, kutokuwepo kwa Gati za Kutosha
Bandari ya Dar Es Salaam kwa sasa ina jumla ya gati 12 za kuhudumia shehena ya magari, mzigo mchanganyiko na makasha pamoja na gati mbili za mafuta na kituo kimoja baharini cha kupokelea shehena ya mafuta. Gati hizo 12 za Bandari ya Dar es Salaam zina uwezo wa kupokea hadi meli 10 kwa wakati mmoja na wastani wa meli nyingine 16 zikisubiri nangani (outer anchorage) kupatikana kwa nafasi gatini.
Hali hiyo husababisha kuwa na msongamano mkubwa wa meli nje ya bandari zikisubiri nafasi ya kuingia bandarini hivyo bandari yetu kuwa ghali katika gharama za usafirishaji (freight costs) kwa sababu wenye mzigo hulazimika kulipia pia tozo ya adhabu ya meli kuchelewa gatini (demurage charges) inayotozwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).
Ni wazi kwamba Mpango Mkakati wa Tatu wa TPA wa kipindi cha mwaka 2016/17 hadi 2020/21, ulilenga kufanya kuimarisha na kuboresha kina cha gati namba 1 hadi 7 pamoja na ujenzi wa gati ya magari (RoRo), ujenzi wa gati namba 12-13 na kuchimba pamoja na kutanua lango la kuingia na kugeuzia meli.
Aidha, katika kipindi hicho, miradi hiyo iliyopangwa haikuweza kutekelezeka kutokana na rasilimali fedha za kutosha. Upungufu wa magati uliopo kwa sasa ni kama inavyoonekana kwenye
Uhaba wa Mitambo ya Kisasa
Hali ya kutokuwepo kwa mitambo ya kutosha na ya kisasa imekuwa changamoto ya muda mrefu kwa Bandari ya Dar es Salaam.
Licha ya jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali katika kuhakikisha bandari zetu zinakuwa na vifaa vya kutosha, bado kuna uhitaji mkubwa katika kuhakikisha kunakuwepo na mitambo inayotumika kutoa huduma kwa meli na shehena ili kufikia malengo ya utendaji yaliyowekwa.
Ambapo ikilinganishwa na bandari nyingine au Kitengo cha Makasha kilichopo Gati Na. 8 -11, Bandari ya Dar es Salaam haina mitambo ya kutosha ambayo ingewezesha utoaji huduma kwa tija na kupunguza msongamano wa meli gatini pamoja na nangani.
Kutokuwepo kwa Mifumo ya Kisasa ya TEHAMA
Shughuli za bandari zinajumuisha huduma kwa meli na shehena mbalimbali ambapo kwa upande wa shehena, TPA hutoa huduma za kupakua, kupakia, kupokea, kuhifadhi na kukabidhi shehena kwa wateja. Utoaji wa huduma hizo unaambatana na ushirikishaji wa wadau mbalimbali wa Serikali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na wadau wa Sekta Binafsi wakiwemo Mawakala wa Meli na Forodha.
Hata hivyo, TPA inakosa Mfumo mahsusi wa TEHAMA unaounganisha mifumo mbalimbali ya utoaji wa huduma bandarini (Terminal Operating System and Port Community System) katika kutoa huduma za bandari na kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza ufanisi.
Ili kuwa na huduma zenye ufanisi kwa wateja ambazo zitapunguza muda wa kutoa huduma bora, unahitajika mfumo mmoja wa kisasa wa TEHAMA utakaoratibu shughuli zote za huduma kwa wadau wa bandari, meli, shehena na utawala. Kwa sasa, huduma za bandari nchini zinahusisha wadau wa Serikali na Sekta Binafsi zaidi ya 30 ambao mifumo yao haijaunganika na mifumo ya bandari pamoja na ya forodha.
Kutofikiwa Viwango vya Kimataifa Huduma za Bandari
Kama ilivyoonesha hapo juu, tija kwa bandari zetu hususan Bandari ya Dar es Salaam haijafikia viwango vya kimataifa ambavyo vinaweza kuvutia zaidi meli na shehena kubwa kuhudumiwa na bandari zetu.
Viwango hivyo vinajumuisha muda wa meli kukaa gatini na kusubiri nangani ambapo meli hutumia wastani wa siku 9.5 tangu kuingia bandarini, kupata gati, kupakia/kupakua na kuondoka, muda wa mzigo kuhudumiwa bandarini hadi kumfikia mteja ambao kwa kasha moja kwa sasa ni wastani wa siku 9.3 na hivyo kuongeza gharama kwa wateja katika kutumia Bandari ya Dar es Salaam.
Kutokuwepo kwa Maeneo ya Kutosha Ndani na Nje ya Bandari ya Kuhifadhi Shehena Pamoja na Maegesho ya Meli
Kwa sasa wastani wa meli kwa siku zinazosubiri kuingia bandarini kuhudumiwa (outer Anchorage) ni meli 16 na wastani wa gati zilizopo kwa sasa kuhudumia meli ni meli 10 kwa wakati mmoja. Hivyo, kwa kuzingatia ongezeko la shehena na idadi ya meli zinazokuja nchini upo uhitaji mkubwa wa kuongeza maeneo ya bandari kwa ajili ya kuhudumia meli na kuhifadhi shehena ndani na nje ya bandari.
Endapo Tanzania haitaridhia Mkataba huo ni nchi kupoteza fursa ya uwekezaji katika uendeshaji na uendelezaji wa bandari nchini ikiwemo ununuzi wa mitambo kuhudumia shehena, mifumo ya TEHAMA na kuunganisha mnyororo wa usafirishaji. Historia inaonesha kuwa, ushiriki wa Sekta Binafsi huleta tija na ufanisi katika shughuli za kibandari ndani na nje ya nchi.
Mathalan, ushirikishwaji wa Kampuni ya TICTS katika uendeshaji wa Gati la Makontena Na. 8 – 11 katika Bandari ya Dar es Salaam ulileta tija na mafanikio katika kuhudumia shehena ya makontena ikilinganishwa na mafanikio hafifu katika Gati Na. 5 – 7 la Makontena ambalo linaendeshwa na TPA. Aidha, sekta ndogo ya bandari ni kichocheo kikubwa kwa ajili ya ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi.
Hivyo, kutoshirikisha Sekta Binafsi katika uwekezaji wa shughuli za kibandari ni kuzinyima sekta nyingine za kiuchumi kukua na kuchangia katika pato la Taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla
Kuongeza Ufanisi katika utoaji wa huduma
Sekta Binafsi ina utaalam wa uendeshaji wa shughuli za bandari unaotokana na uzoefu wa kufanya shughuli hizo katika maeneo mbalimbali duniani.
Kupitia uzoefu huo, teknolojia na utaalam, Sekta Binafsi inaweza kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za bandari pale ambapo inapewa fursa ya kufanya hivyo, kwa mfano, uwekezaji uliofanywa na DPW katika Bandari ya Dakar, nchini Senegal umefanikiwa kuboresha ufanisi wa bandari katika viwango vya utendaji kazi kama vile kupunguza muda wa meli kusubiri nje ya bandari kutoka saa 35 hadi saa moja (1), kupunguza muda wa malori unaotumiwa ndani ya bandari kutoka dakika 152 hadi dakika 22, kuongeza idadi ya mizunguko ya mashine ya kupakua na kupakia makasha kutoka mizunguko 10 hadi 31 kwa saa moja.
Majumuisho ya viwango vya utendaji wa Bandari ya Dakar vilivyoimarika ni kama inavyoonekana kwenye
Kupunguza gharama za kupitisha Mizigo Bandarini
Gharama za usafirishaji wa mzigo kutoka kwa mzalishaji (producer) kwenda kwa mlaji (consumer) zimegawanyika katika makundi makubwa matatu yafuatayo;
i.Gharama ambazo zinahusisha kutoa mzigo nje ya nchi hadi kuufikisha bandarini (sea-side freight costs);
ii.Gharama ambazo zinahusisha huduma za bandari (port charges); na
iii.Gharama ambazo zinahusisha kutoa mzigo kwenye eneo la bandari baada ya kukamilisha taratibu za forodha kwenda kwenye masoko au mlaji wa mwisho (land-side transport costs). Bandari inapokuwa na ufanisi mdogo, gharama ambazo zinahusisha kuutoa mzigo nje ya nchi huwa kubwa ili kufidia gharama ambayo mtoa huduma ya usafirishaji (shipping line or agent) ataingia pale ambapo atafikisha meli yake katika bandari yenye ufanisi mdogo ambao humlazimu kutumia muda mrefu katika bandari hiyo.
Kwa mantiki hiyo, gharama zote ambazo mnunuzi wa mzigo au bidhaa atazilipa hadi kufikisha mzigo bandarini zitabebwa na mnunuzi au mlaji wa mwisho wa bidhaa husika. Kwa mfano, Bandari ya Dar es Salaam ambayo meli za makasha zinasubiri kwa wastani wa siku 10 kabla ya kuingia bandarini, kampuni zinazoleta meli zake zinaingia gharama ya ziada ya uendeshaji wa meli hizo kutokana na ufanisi mdogo wa Bandari.
Kupitia ushirikishaji wa Sekta Binafsi, ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam utaongezeka na kupunguza muda wa meli kusubiri nje na hivyo kupunguza gharama za kuleta mzigo nchini na kuokoa fedha ambazo zinalipwa na mlaji wa mwisho ambazo zilikuwa zinaliwa juu ya gharama halisi za bidhaa kutokana na ufanisi mdogo wa bandari.
Kuchochea shughuli za sekta nyingine, kukuza Uchumi (Economic Multiplier Effect)
Ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndio lango kuu la biashara nchini na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi, DR Congo, Zambia na Malawi unachochea shughuli za sekta nyingine za kiuchumi zikiwemo viwanda, biashara, kilimo, usafirishaji kwa njia ya barabara na reli na utalii.
Kupitia kuishirikisha Sekta Binafsi, TPA inalenga kuwa na bandari yenye ufanisi ambao utavutia watumiaji wengi zaidi kutumia kusafirisha mizigo mingi zaidi itakayochochea shughuli za uchumi wa nchi na nchi za jirani zinazotumia bandari ya Dar es Salaam.
Ambapo ongezeko la shughuli za kiuchumi, Mamlaka na Wakala nyingine za Serikali zitakusanya mapato, tozo na ada mbalimbali zinazotokana na ongezeko na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini.
Kupunguza mzigo kwa Serikali
Hasa katika kugharamia mitambo na vifaa vya utoaji wa huduma za Bandari nchini, ambapo katika vipindi tofauti Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia vifaa na mitambo ya utoaji huduma kupitia miradi mbalimbali, fedha ambazo zingeweza kutumika katika shughuli nyingine za kiuchumi.
Mathalan, katika miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2019/20 hadi 2021/22, Serikali ilitoa jumla ya Shilingi Trilioni 1.638 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Endapo Serikali ingeshirikisha Sekta Binafsi katika kutekeleza miradi hiyo, fedha hizo zingetumika katika shughuli nyingine za maendelo na utoaji huduma kwa jamii
Manufaa tarajiwa baada ya kushirikisha sekta binafsi
Mapato makadirio ya ongezeko la shehena na mapato ya Kodi inayokusanywa na TRA kutokana na mzigo unaopitishwa Bandari ya Dar es Salaam yamefanyika kwa kuangalia namna ambayo mzigo huo umekuwa ukiongezeka kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita na kwa kuzingatia uwekezaji unaotarajiwa kufanyika kama inayoelelezwa kwenye sehemu ifuatayo;
Ukuaji wa Shehena kipindi cha Miaka 10 iliyopita na matarajio ya miaka 10 ijayo
Ambapo bila mwekezaji Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kuanzia mwaka 2012/13 hadi mwaka 2021/22, shehena iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 5.14 kwa mwaka. Ongezeko hilo ni kutoka tani milioni 12.55 za mwaka 2012/13 hadi tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22.
Katika kupata maoteo, kiwango cha ukuaji wa shehena kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita cha asilimia 5.14, kimetumiwa kupata matarajio ya shehena kwa kipindi kijacho cha miaka 10 kuanzia mwaka 2022/23 hadi mwaka 2032/33. Katika kipindi hicho, shehena inatarajiwa kuongezeka kutoka tani milioni 18.41 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 33.44 ifikapo mwaka 2032/33.
TUTAENDELEA NA UCHAMBUZI HUU KUHUSU BANDARI