Na MWANDISHI WETU
-MTWARA
Benki ya NMB Kanda ya kusini imetoa vifaa vya kuezekea katika zahanati ya polisi iliyopo mkoani hapa vyenye thamani ya Sh17 milioni.
Vifaa hivyo ambavyo vitamalizia jengo la mama na mtoto katika zahanati hiyo ni pamoja na bati, mbao, misumari na mabati na kofia za bati.
Meneja wa benki ya NMB Kanda ya Kusini, Faraja Raphael Ngingo alisema kuwa changamoto za sekta ya afya nchini ni jambo la msingi kwa benki ya NMB.
Amesema pamoja na makubwa na mengi yanayofanywa na serikali katika sekta ya afya lakini NMB kama wadau wanao wajibu wa kuunga mkono juhudi hizo.
“Tulipopata maombi haya ya kuchangia sekta ya afya tulifarijika na kuamua mara moja vifaa hivi ni moja ya ushiriki wetu katika maendeleo ya jamii, tunao wajibu wa kuhakikisha jamii inayotuzunguka inafaidika na faida tunayoipata” amesema Faraja
Amesema wanatambua kuwa kupitia jamii ndipo wateja wanapotoka. Hata hivyo alisema NMB imekuwa ikipokea maombi mengi sana lakini imejikita katika afya, elimu na misaada ya majanga. Kwa miaka saba mfululizo sasa NMB imekuwa ikitoa asilimia moja ya faida yake kwa jamii.
Mganga mkuu wa zahanati ya polisi, ambaye pia ni mkuu wa kikosi cha afya mkoani Mtwara, Dk. Stephen Kisaka alisema zahanati hiyo ni moja kati ya vituo 18 vya kutolea huduma za afya mkoani Mtwara na ni moja kati ya vituo 37 vya jeshi la polisi.
Huduma zinazotolewa katika zahanati hiyo ni pamoja na wagonjwa wa nje, mama na mtoto na wenye maambukizi ya ukimwi na kwa mwezi huudumia wagonjwa 2500 mpaka 3000 na wenye bima ya afya 800 hadi 1000
Vile vile wanahudumia wagonjwa wa msahama, wazee na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo alisema kuwa kituo hiko ambacho wagonjwa wanaohudumiwa asilimia 80 ni raia kilianza kwa wazo kutoka kwa askari polisi wenyewe na baadaye wakapata msaada kutoka kwa wadau.
“Tunataka ifikapo mwaka 2025 tuwe na kituo kamili cha afya kwa hiyo msaada huu utarahisisha njia ya kufika katika kituo cha afya kabla ya kufika mwaka 2025” alisema RPC Katembo.
Mmoja wa wagonjwa aliyefika hospitalini hapo kupata huduma, Rachel Thobias, alisema wanaishukuru zahanati ya polisi kwani huduma wanapokelewa na kuwapatia huduma nzuri kwa upande wa mama wajawazito, watoto na hata wagonjwa wa nje.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Mukunda alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kuwa karibu na jeshi la polisi.
“Kama asilimia themanini ya wagonjwa wanaokuja hapa ni raia maana yake mko karibu nao na mnatoa huduma bora” amesema Mkuu wa wilaya.