*Awataka watoe ushirikiano kwa wawekezaji wanaoonesha nia ya kuwekeza nchini
Na MWANDISHI WETU
-ITALIA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania walioshiriki katika Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia wahakikishe wanatumia vizuri fursa walizozipata kutoka kwenye jukwaa hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na wafanyabiashara walioonesha nia ya kuja kuwekeza nchini.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeondoa tozo na urasimu uliokuwepo awali kwa lengo la kurahisisha shughuli za biashara na uwekezaji nchini.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi wahakikishe Taifa linanufaika kwa kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vya uwekezaji pamoja na kuwashawishi wawekezaji kutoka katika nchi wanazoishi waje kuwekeza Tanzania.
Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Oktoba 20, 2023) katika hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Benki ya NMB kwa lengo la kuwatambua wafadhili na washiriki wa Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia.
Waziri Mkuu ambaye yuko Italia akimuwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023, Rome nchini Italia, aliwasisitiza Watanzania waheshimu sheria za nchi husika.
Mheshimiwa Majaliwa alisema kupitia jukwaa hilo wafanyabiashara na wawekezaji wengi kutoka nchini Italia wameonesha nia ya kuja Tanzania kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, hivyo amewataka viongozi na watendaji wa wizara zinazohusika na masuala ya uwekezaji kuchangamkia fursa hiyo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wafugaji nchini wakubali kubadilika na wafuge kwa kutumia teknolijia ya kisasa ili waweze kujinufaisha zaidi na shughuli hiyo. “Tubadilike tupate manufaa zaidi, ufugaji ni uchumi, ufugaji ni maisha na ufugaji ni kazi, hivyo tubadili mfumo wa ufugaji wetu kwa ajili ya kujiongezea kipato zaidi.”