Na Mwandishi Wetu
Asasi ya NMB Foundation na shirika la Save the Children International zimeunganisha nguvu kusaidia kuboresha maisha nchini kwa kuingia makubaliano ya kushirikiana kuchangia juhudi za utekelezaji wa haki za watoto, vijana na makundi mengine yenye hali duni.
Mashirika hayo mawili ya kibinadamu yalitia saini mkataba wa ushirikiano kwenye shughuli za ustawi wa jamii Ijumaa jijini Dar es Salaam katika makao makuu ya Benki ya NMB.
Wakati NMB Foundation ni asasi ya kiraia ya NMB, Save the Children ni shirika la kimataifa linaloongoza katika kusimamia haki za watoto ambalo pia linajihusisha na masuala ya vijana na watu wengine wenye changamoto za kimaisha.
Akizungumza kabla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Meneja Mkuu wa NMB Foundation, Nelson Karumuna, amesema kimsingi ushirikiano huo unalenga kuendeleza mshikamano na uwekezaji katika ustawi na maendeleo ya jamii.
“Tunaingia makubaliano ya kihistoria kati yetu NMB Foundation na wenzetu wa Save the Children yenye lengo la kuimarisha utekelezaji wa haki za watoto, vijana na wanawake nchini Tanzania,” kiongozi huyo alibainisha.
“Ushirikiano huu ni muhimu kwa kuleta mabadiliko chanya na ya kudumu katika maisha ya Watanzania. Kwa kutumia utaalamu wetu, rasilimali zetu, na ubunifu wetu, tunaweza kuziwezesha jamii kwa zana na maarifa yanayohitajika ili kuweza kujitegemea,” aliongeza.
Huku akisisitiza kuwa NMB Foundation itatumia zaidi uzoefu wa miaka mingi wa Save the Children katika shughuli za kibinadamu, Bw Karumuna amesema ushirikiano huo utazingatia zaidi maeneo matano ambayo ni elimu, afya, mabadiliko ya tabianchi na ulinzi wa mtoto.
Shirika hilo lisilo la kiserikali, ambalo lengo lake kuu ni kuhakikisha watoto sio tu wanaishi, bali pia wanastawi, lipo nchini tangu mwaka 1986.
“Ushirikiano huu na kuunganisha nguvu kati yetu, ni hatua muhimu kuelekea kutimiza lengo moja ambalo ni kuleta matokeo chanya katika maisha ya watoto, vijana na makundi mengine ya watu wenye hali duni katika jamii zetu,” mkurugenzi wake nchini, Anjela Kauleni, amesema.
Aidha, aliongeza kuwa uamuzi ya NMB Foundation kushirikiana na Save the Children ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuchangia kuboresha maisha ya jamii zinazoishi katika mazingira magumu.
Bi Kauleni amesema moja ya faida kubwa za ushirikiano huo ni pamoja na taasisi hizo kuweza kuimarisha programu za shughuli zao na kupanua wigo wa manufaa yatakayopatikana.
“Uwepo wa Benki ya NMB ambayo ni mlezi wa Asasi ya NMB foundation katika sehemu nyingi nchini na utaalamu wake wa kibiashara utatuwezesha kuyafikia hata maeneo yaliyo pembezoni kabisa mwa nchi yetu,” alifafanua huku akisisitiza mchango wa ubunifu wa benki hiyo na uzoefu wa shirika hilo katika ushirikiano wao.
Utiaji wa saini ya makubaliano hayo ulishuhudiwa na mkurugenzi wa eneo la Afrika Mashariki na Kusini wa Save the Children, Ian Vale, aliyesema ushirikiano huo ni fursa nzuri ya wao kufanya kazi na sekta binafsi kusaidia kuboresha maisha.