Home KITAIFA UWEKEZAJI WA BANDARI UTALETA FURSA LUKUKI KWA TAIFA LETU

UWEKEZAJI WA BANDARI UTALETA FURSA LUKUKI KWA TAIFA LETU

Google search engine

Na MWANDISHI WETU

-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM

MJADALA wa uwekezaji wa Bandari yetu umekuwa ni wenye afya kwa Taifa letu, lakini kila upande ukiangazia fursa badala ya hasara.

Kutokana na hali hiyo yapo maeneo kadhaa ambayo kwa Taifa tumeshindwa kupata toja zaidi ya kunufaika na lawama hasa kwa bandari shindani ambao kila mara wamekuwa wakitumia hali hiyo kama njia ya kutaka kukwamisha mchakato wa Serikali katika kuona namna bora ya uwekezaji katika eneo hilo nyeti ambalo pia ni lango la uchumi kwa nchi yetu.

Licha ya hali hiyo kila mara ahadi ya Serikali imekuwa ni kuhakikisha kutodharau maoni na ushari wa suala la uwekezaji wa Bandari kwani Serikali imejidhatiti kuhakikisha bandari inakuwa na ufanisi unaoendana na mahitaji ya sasa na kwa kuzingatia manufaa ya kijiografia ya nchi yetu.

Pamona na hali hiyo lakini kila mara Serikali imekuwa ikitoka hadharabi na kusisitizwa kwamba Bandari haijauzwa, bali Serikali inataka kubadilisha mwekezaji ili iweze kuendeshwa kwa ufanisi na tija zaidi.

Ni kweli licha ya maboresho yaliyofanyika, hali ya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda. Kwa mfano, wastani wa meli kusubiri nangani kwa Bandari ya Dar es salaam ni siku tano ikilinganishwa na wastani siku moja na nusu kwa Bandari za Mombasa na Durban.

Udhaifu huo uliopo katika bandari hiyo unasababisha meli kusubiri muda mrefu nangani na hivyo kuongeza  gharama, kwa siku moja ni takriban Dola za Marekani 25,000, sawa na takriban Shilingi milioni 58 kwa siku.

Kitendo cha meli kutumia muda mrefu kupakia na kupakua shehena gatini kwa wastani wa siku tano ikilinganishwa na siku moja inayokubalika kimataifa kinasababisha meli kubwa kutokuja katika Bandari ya Dar es Salaam.

Ni wazi kwamba hali hiyo huikosesha nchi mapato ambayo yangeweza kutumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini ambayo ingesaidia kukuza uchumi na kuboresha huduma za wananchi.

Ili kutatua changamoto za bandari zilizopo na kuongeza ufanisi katika mapato, ajira na kuchagiza sekta nyingine za kiuchumi, Serikali ilifanya maamuzi ya kutafuta wawekezaji wapya wanao endana na dhima ya Serikali.

Juni 10, 2023 Bunge liliridhia mkataba unaohusu makubaliano ya mahusiano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai (IGA) ili kuwezesha majadiliano ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, ambapo miradi hiyo ni pamoja na ya uendelezaji na uboreshaji wa huduma za bandari nchini.

“Kilichofanyika sasa ni kuwezesha tu baadaye kuwa na mikataba ya maeneo maalum ambayo itazingatia maslahi ya nchi kisheria na kibiashara bila kuathiri usalama Taifa,” kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Juni 20, 2023 mkoani Arusha

Pia, Waziri Mkuu Majaliwa amesema wakati wa kuingia mikataba utakapofika wataalamu wa uchumi nchini wataishauri Serikali kuhusu muda wa uendeshaji wa uwekezaji huo, hivyo amewataka wananchi waendelee kuwa na subira.

Akifafanua kuhusu makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia kampuni ya DP World, Waziri Mkuu amesema “Ili mradi mmesema mkataba uzingatie maslahi ya Taifa, tutahakikisha mkataba huo unazingatia maslahi ya Taifa, Mmekuwa na hofu na ajira, hakuna atakayepoteza ajira.

“Mmekuwa na hofu na ardhi, kwamba anayekuja atachukua ardhi, siyo kweli. Hakuna mwekezaji aliyepewa ardhi kwa sababu hata kwenye sheria za uwekezaji, mwekezaji hapewi ardhi bali anapata kibali cha kukaa juu ya ardhi, na analipa kodi.

“Hofu nyingine ni muda wa mkataba, mmesema atakaa miaka 100. Hapana, haijatamkwa popote ila akija tutakubaliana miaka ya kukaa na kufanya tathmini kadri tunavyoona ukaaji huo utakuwa na maslahi ya Watanzania,” Julai 7, 2023 mkoani Mtwara

Ni kweli usiopingika kwamba Kampuni ya DP World imewekeza kwenye nchi nyingi duniani na imejenga Bandari kavu nchini Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Mwekezaji huyo anahudumia bandari zaidi ya 168 duniani, ana meli zaidi ya 400. Meli hizo zitaleta mizigo kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam, jambo ambalo ni wazi kama Taifa tunatakiwa kumwamini na kusimama na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kufungua lango la uchumi kwa nchi yetu.

Manufaa 12 ya uwekezaji wa DP World katika Bandari

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolwa na Wizara ya Uchukuzi inachambua kwa kina faida 12 kubwa ambazo Tanzania inatarajia kuzipata kutoka na uwekezaji wa kampuni ya DP World kwenye bandari ya Dar es Salaam:

1. Kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 kwa sasa mpaka masaa 24 tu.

2. Kuongeza idadi ya meli zitakazokuja Bandari ya Dar es Salaam kutoka meli 1,569 zilizohudumiwa mwaka 2021/22 hadi kufikia takriban meli 2,950 ifikapo mwaka 2032/33;

3. Kupunguza muda wa ushushaji wa makontena kutoka wastani wa siku 4.5 mpaka siku 2

4. Kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka masaa 12 mpaka saa 1 tu kutokana na uboreshaji wa mifumo yạ TEHAMA;

5. Kupunguza gharama ya usafirishaji wa shehena kutoka nchi za nje kwenda nchi za jirani, kutoka USD 12,000 mpaka kati ya USD 6,000 na USD 7,000 kwa kasha

6. Kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.41 kwa mwaka 2021/22 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka 2032/33

7. Kuongezeka kwa mapato ya serikali yatokanayo na kodi ya forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka Shilingi trilioni 7.76 kwa mwaka 2021/22 hadi Shilingi trilioni 26.70 kwa mwaka 2032/33

8. Kuongezeka kwa ajira zinazotokana na shughuli za bandari kutoka 28,990 kwa mwaka 2021/22 hadi 71,907 ifikapo mwaka 2032/33

9. Maboresho ya magati ya kuhudumia majahazi na abiria ikiwa ni pamoja na kushawishi uingiaji wa meli kubwa za kitali (cruise ships) zitakazo ongeza idadi ya watalii nchini na kuongeza pato la taifa

10. Mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TPA katika Bandari zote (knowledge and skills transfer)

11. Uanzishaji wa maeneo huru ya kiuchumi na kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi zikiwemo: sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi; utali; viwanda na biashara

12. Kuchagiza ukuaji wa sekta ndogo za usafirishaji kwa njia ya reli (SGR, TAZARA na MGR) na barabara; na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia.

Katika baadhi ya ibara ya azimio la Bunge lililoridhiwa Juni 10, 2023 kiwamo;

vi. Ibara ya 9 – Motisha za Uwekezaji: Ibara hii inaeleza kuwa, uwekezaji wa DP World utakuwa mkubwa na utaleta manufaa ya kiuchumi na kijamii hivyo utahitaji kutolewa motisha za uwekezaji.

Hivyo, pande mbili zilikubaliana kutoa motisha za uwekezaji kwa kuzingatia Sheria za nchi na taratibu mahsusi za Tanzania kama itakavyoainishwa zaidi katika Mikataba ya nchi mwenyeji.

vii. Ibara ya 12 – Ulinzi na Usalama: Ibara hii inaeleza kuwa utekelezaji wa shughuli za miradi hautaathiri au kukiuka masuala ya ulinzi na usalama ikiwemo: Ardhi ya Mradi, mifumo, miundombinu ya juu na chini ya eneo la bandari, mitambo iliyosimikwa pamoja na masuala mengine ya usalama ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama yatakavyokubaliwa chini ya Mkataba wa Nchi Mwenyeji.

viii. Ibara ya 13 – Ushirikishaji wa Wazawa, Ajira na Majukumu kwa Jamii: Ibara hii inaeleza kuwa, mikataba itakayosainiwa ya utekelezaji wa mradi ni lazima iainishe: mpango wa ushirikishaji wa wazawa katika utekelezaji wa mradi husika, majukumu kwa jamii, undelezaji wa ajira zilizopo, kutoa ajira mpya kwa watanzania na kuwapatia mafunzo kuhusiana na utekelezaji wa miradi husika.

ix. Ibara ya 18 – Kodi, Tozo na Ushuru Nyinginezo: Ibara hii inaeleza kuwa kodi, ushuru na tozo nyinginezo zitakusanywa katika utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia Sheria za Kodi zilizopo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, Ibara hii inaeleza kuwa Motisha za Uwekezaji, misamaha ya kodi ama tozo nyinginezo zitatolewa kwa kuzingatia msingi wa sheria za kodi zilizopo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kama itakavyokubaliwa katika Mkataba wa Nchi Mwenyeji na Mikataba ya Utekelezaji wa Miradi kwa kuzingatia Sheria za Nchi.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here