Na Beatus Maganja
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, Dk. Rashid Chuachua amesema shughuli za uhifadhi na Utalii hususani Uwindaji wa Kitalii zinazofanywa na kusimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) zina faida kubwa wilayani humo.
Ameyasema hayo Oktoba 24, 2023 katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa jamii iliyofanywa na TAWA wilayani Kaliua.
“TAWA katika wilaya ya kaliua wameisha tujengea madarasa mawili yenye thamani ya Shilingi millioni 50 katika shule ya msingi Usinge, lakini TAWA wameshawahi kutoa fedha kule mwendakulima ambapo walichangia bati 205 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa” amesema
Sambamba na hilo TAWA wameweza pia kukamilisha nyumba ya mganga katika kata ya Zugimlole, haya ni baadhi tu ya mambo ambayo TAWA wamekuwa wakiyafanya” ameongeza
Dr. Chuachua amewataka wananchi kutii Sheria kwa kuacha kufanya shughuli zozote ndani ya hifadhi kama Sheria zinavyotaka
Naye Mkuu wa divisheni ya mipango, uratibu na ufuatiliaji ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa H/W Kaliua Bw. Emmanuel Kishimbo amesema uwepo wa TAWA katika Halmashauri hiyo umekuwa na manufaa makubwa kwani katika nyakati tofauti wamekuwa wakipata mapato ambayo yamewasaidia kukamilisha miradi mingi ikiwemo kituo cha afya cha Usinge ambacho kwasasa kinatoa huduma pamoja na ujenzi wa kituo cha afya cha Ukumbi Siganga ambacho bado kinaendelea kujengwa.
Afisa Ujirani Mwema kutoka TAWA Kanda ya Magharibi Magreth James amesema wananchi wanaoishi Jirani na vitalu vya Uwindaji wa kitalii wamekuwa wakinufaika moja kwa moja na gawio la Dola 5,000 kutokana na shughuli za uwindaji wa kitalii zinazofanyika jirani na vijiji vyao ambazo zimekuwa zikitumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema Halmashauri za Wilaya huwa zinapata gawio la asilimia 25 ya fedha za uwindaji wa kitalii kutoka TAWA kutokana na idadi ya Wanyamapori waliowindwa katika kitalu husika Jirani na kijiji ambapo asilimia 40 ya mapato yaliyopatikana huelekezwa katika shughuli za uhifadhi na asilimia 60 huelekezwa katika miradi ya maendeleo