Na MWANDISHI WETU
-TANGA
BENKI ya NMB rasmi imezindua msimu wa tano wa promosheni yake kabambe ya MastaBata chini ya kauli mbiu ‘MastaBata Halipoi’ inayolenga kuwazawadia wateja wa benki hiyo kwa uaminifu na imani yao kwa benki hiyo
Katika promosheni hiyo ya miezi mitatu ambayo itafikia kilele Januari 25, 2023, wateja wa Benki ya NMB watajishindia zaidi za fedha taslimu za shilingi milioni 350 pamoja na safari zilizolipiwa kila kitu za kula bata katika ‘full moon party’ huko Kendwa Rocks visiwani Zanzibar na safari za kwenda hadi jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini wakati wa droo ya mwisho.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Tanga mwishoni mwa wiki, Mkuu wa idara ya Biashara ya Kadi wa Benki ya NMB, Philbert Casmir alisema kampeni hiyo sio tu inaendana na malengo ya Tanzania ya kuwa na uchumi usio wa matumizi ya fedha tasalimu bali ni hatua muhimu katika kuongeza kasi ya ushirikishwaji wa kifedha.
“Hi promosheni yetu inalenga kuchochea matumizi ya malipo ya kidijitali ambayo yameonekana kuwa rahisi zaidi, ya haraka na salama. Pamoja na aina mbalimbali za malipo ya kidigitali zinazopatikana kwa urahisi kwetu, ninawahimiza sana wateja wetu kutumia NMB MasterCard kulipia bidhaa au huduma kupitia mashine za mauzo (POS), Msimbo wa QR au mamunuzi ya mtandao ili kujiwekea nafasi nzuri ya kujishindia pesa taslimu na safari zilizolipiwa kila kitu wakati wa kampeni,” Casmir alisema.
Casmir alibainisha kuwa promosheni hiyo ni njia ya kuwazawadia wateja waaminifu wa benki hiyo kwa kuendelea kuwaunga mkono kwa muda mrefu na kuongeza kuwa benki ya NMB imeweza kupiga hatua kubwa katika miaka yake 25 ya utendaji kazi wake kutokana ina imani ya wateja.
Alibainisha kuwa promosheni hiyo itakuwa na droo za wiki ambapo washindi 100 wataondoka na shilingi 100,000/ kila mmoja, droo za mwezi ambapo washindi 30 wataondoka na shilingi 500,000 kila mmoja, washindi 10 ambao watajishindia safari za kula bata katika ‘full moon party’ huko Kendwa Rock visiwani Zanzibar na zawadi kuu ikiwa ni safari ya kwenda Cape Town ambapo jumla ya washindi sababa watakaobahatika watasafiti kwa siku tano na watashindikizwa na wenza wao au rafiki baada ya droo ya mwisho kufanyika.
“Tofauti na mwaka jana, promosheni ya mwaka huu inatoa pesa taslimu na safari zilizolipiwa kila kitu kwa washindi watakaobahatika na ni maalum kwa wateja wote wa Benki ya NMB. Tunapomaliza mwaka, tunataka kuwazawadia wateja wetu ambao wamekuwa bega kwa bega nasi katika safari yetu ya kujenga jamii inayotumia malipo ya kidigitali. Natumia fursa hii kuwaomba wateja wetu wote kutumia kadi zao na njia nyinginezo za malipo ya kidijitali zinazotolewa na Benki ya NMB kulipia manunuzi yao ya kila siku na ukibahatika unaweza kujishindia shilingi 50,000/- papo hapo iwapo utatambuliwa na bwana wetu wa NMB MastaBata.”
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba wakati wa hafla hiyo aliipongeza Benki ya NMB kwa jitihada zake za kuongeza kasi ya ujumuishaji wa fedha nchini Tanzania kupitia utoaji wa suluhu mbalimbali za malipo ya kidijitali.
“Malipo ya fedha taslimu yana changamoto mbalimbali ikiwamo ya usalama. Kama nchi, tunatumia pesa nyingi kuchapisha tena noti zilizochakaa na ndiyo maana Serikali inasisitiza matumizi ya kidigitali. Kwa benki, gharama kubwa sana zinatumika kusafirisha fedha kutoka sehemu moja kwenda yingine. Ili kupunguza gharama hizo zisizo zalazima, hatuna budi kutumia malipo ya kidigitali,” aliongeza Kindamba.
Aliipongeza benki hiyo kwa kuendela kuunga mkono mipango mbalimbali ya maendeleo inayoongozwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta muhimu ikiwemo elimu, afya na mazingira.