KICHWA kipya cha treni ya umeme chenye namba ya usajili E6800-01 kilichoundwa na Kampuni ya ‘Hyundai Rotem Company’ (HRC) kimewasili nchini Tanzania kutoka nchini Korea Kusini.
–
Kichwa hicho cha umeme ni miongoni mwa vichwa 17 vilivyoagizwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa ajili ya kuanza kwa safari za treni ya Kisasa ya Standard Gauge (SGR).
–
Kampuni ya Hyundai Rotem Company (HRC) ya nchini Korea Kusini ndio ilipewa jukumu la kutengeneza vichwa hivyo kuanzia namba E6800-01 hadi E6800-17 na sasa bado vichwa 16.
–
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha TRC, Jamila Mbarouk amesema kuwa mfumo wa uendeshaji unaotumika katika kichwa hicho ni nishati ya umeme wenye msongo wa Kilovoti (KV) 25 na kitakuwa na nguvu ya Kilowati 5,000 sawa na nguvu ya 6,800 kwa kipimo cha ‘Horse Power’.
–
“Kichwa kitakuwa na uwezo wa kutembea mwendokasi wa Kilometa 160 kwa saa (160km/h), kuvuta na kupeleka umeme kwenye mabehewa yasiyozidi 14 ya abiria kwa wakati mmoja,” amesema Mbarouk.
Pia amesema kuwa majaribio ya kichwa cha treni kitakachotumika katika reli ya kiwango cha kimataifa, yatafanyika kati ya Dar es Salaam na Morogoro na baadaye Dar es Salaam hadi Dodoma.