-ABUJA, Nigeria
RAIS wa Nigeria Bola Tinubu ameiomba Seneti kuidhinisha karibu dola bilioni 8 (Sh trilioni 19.9) katika deni jipya kama sehemu ya mpango wa ukopaji wa nje wa mwaka 2022-24 ili kufadhili ujenzi wa miundombinu, afya, elimu na usalama.
Katika barua kwa Seneti, Tinubu aliomba dola bilioni 7.86 na euro milioni 100 ($105.40 milioni) lakini hakusema pesa hizo zingetoka wapi.
“Kwa kuzingatia hali halisi ya kiuchumi inayoikabili nchi, imekuwa ni lazima kutumia mikopo kutoka nje kuziba pengo la ufadhili ambalo litatumika katika miradi muhimu ya miundombinu ikiwemo umeme, reli, afya miongoni mwa mambo mengine,” alisema Tinubu.
Serikali imesema inataka kuhimiza uwekezaji badala ya kutegemea kukopa ili kutengeneza ajira na kujenga miundombinu.