Na MWANDISHI WETU
-SONGWE
JUMLA ya Shilingi milioni 56,362,000 kutoka Benki ya NMB Kanda Nyanda za Juu zimewezesha shule 7 zilizopo katika Wilaya za Mbozi na Mji wa Tunduma mkoani Songwe.
Fedha hizo zilizotolewa kupitia msaada wa Mabati 420 na Madawati 491 zitasaidia shule hizo saba kupunguza adha ya kuketi sakafuni kwa kutoa madawati na kuepuka kunyeshewa na mvua kwa kukabidhiwa bati.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya makabidhiano kwenye Ofisi za Mkuu wa mkoa wa Songwe, Meneja wa NMB Kanda Nyanda za Juu Straton Chilongola alisema msaada huo umetokana na maombi maalumu ya kuchangia elimu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na Mamlaka ya Mji wa Tunduma kutokana na mahitaji ya Madawati na Mabati.
Alisema shule zilizonufaika na msaada huo ni Vwawa Day Sekondari(mabati 200) na Tanganyika Primary School (Mabati 240) zenye thamani ya Jumla ya Shilingi Mil 17,728,000.
Chilongola alitaja msaada mwingine ni wa madawati 491 kwa shule ya sekondari Mlowo na shule za msingi za Chiwezi,Mkombozi,Mahenje na Nansele na Nansele waliokabidhiwa Madawati yenye thamani ya shilingi Mil 27,170,000.
Chilongola alisema Benki ya NMB itaendelea kusimama mstari wa mbele kusaidia na kuchangia huduma za afya elimu na majanga ili kuunga mkono jitihada za serikali kwenye kuchangia huduma za elimu,Afya na majanga.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk. Francis Michael mbali na kuipongeza Benki ya NMB kuchangia Elimu na huduma zingine za kijamii mkoani Songwe msaada huo umefika kwa wakati muafaka kutokana na mahitaji katika shule hizo.
Alisema kuwa msaada huo utapunguza tatizo la madawati na mabati ikiwa ni moja katika ya mahitaji mengi yanayohitajika kwenye sekta za elimu afya na huduma zingine za kijamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Abdallah Nandonde alisema Halmashauri ya Mbozi ina mahitaji mengi kwenye sekta ya elimu na afya ambayo serikali pekee haiwezi kukidhi mahitaji hivyo msaada huo utapunguza sehemu ya mahitaji ambayo serikali ilipaswa kuchangia.
Nandonde aliziomba taasisi zingine za kifedha kuiga mfano wa Benki ya NMB ambayo imekuwa ikijitoa kwa hali kurejesha sehemu ya faida yake kwa kuchangia huduma za kijamii.