*MKURUGENZI MKUU ATAJA VILIVYOPO BAHARINI, NCHI KAVU
*SASA WAJIPANGA KUTAFITI NA KUENDELEA KUCHIMBA GESI ASILIA NCHINI, KUUZWA KWENYE MASOKO YA NJE
Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DAR ES SALAM
MKURUGENZI wa Mamlaka Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, amesema licha ya mafanikio kadhaa yaliyopatikana nchini ikiwamo suala la utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia nchini ambapo kwa sasa jumla ya visima vya utafutaji wa mafuta vilivyochimbwa ni 96 ambapo kati ya hivyo visima 59 vipo maeneo ya nchi kavu na visima 37 vipo maeneo ya baharini.
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa shughuli ya utafutaji wa gesi asilia nchini ilianza miaka ya 1950 ambapo wamefanya utafiti katika visima 96 ambapo kati ya hivyo 44 vimegundulika kuwa na gesi na 52 vimekutwa havina gesi..
Kwa mujibu wa twkimu hizo za PURA imeelezwa kuwa visima 16 vilichimbwa nchi kavu na 28 vilichimbwa baharini.
Akizungumza na wahariri wa vyombo habari katika kikazi kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina leo Novemba 6, 2023 Jijini Dar es Salaam, amesema kuwa pamoja na hali hiyo pia gesi asilia imegunduliwa katika maeneo ya Songo Songo, Mnazi bay, Mkuranga mwaka 2007, Kiliwani Kaskazini mwaka 2008, Ntorya mwaka 2012, Ruvu na Kina Kirefu cha Baharikuanzia miaka ya 2010.
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa gesi asilia iliyogunduliwa nchi kavu na kina kirefu cha bahari ni futi za ujazo Trilioni 57.54 sambapo kati ya hizo nchi kavu Trilioni 10.41 na Baharini Trilioni 47.13.
“Uzalishaji wa gesi asilia ulianza mwaka 2004 kwa upande wa Songo Songo na mwaka 2006 kwa upande wa Mnazi Bay. Ugunduzi na uzalishaji wa gesi asilia iliyogunduliwa umewezesha itumike maeneo mbalimbali, hususan kwa kuzalisha umeme, kutumika viwandani, majumbani na kwenye magari. Hadi sasa kiasi cha gesi kinachozalishwa kinachangia karibu asilimia 70 ya umeme unaozalishwa hapa nchini.
“Hadi sasa kwa kupitia usimamizi wa PURA maeneo ambayo yamefanyiwa tafiti ni kiasi cha kilomita za mraba 534,000 ambapo kati ya hizo kilomita za mraba 394,000 ni nchi kavu na km 140,000 baharini, hata hivyo maeneo mengi yameshafanyiwa tafiti za awali ambapo data, taarifa na takwimu zake zipo (Gravity/Magnetic and 2D seismic);
“Kuimarika kwa mifumo ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi nchini, ambapo kumekuwa na Sheria ya Peroli ya mwaka 1980, Sera ya Nishati ya mwaka 2015, Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, na Sheria ya Udhibiti wa Mapato ya Mafuta na Gesi ya mwaka 2015. Mifumo ambayo imewezesha kuanzishwa kwa PURA na EWURA.
“Katika kipindi chote hicho Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha shughuli hizi zinafanyika kwa ufanisi ili kuwezesha upatikanaji wa rasilimali hii muhimu kwa maendeleo endelevu ya nchi. Kati ya hatua muhimu ambazo Serikali imeendelea kuchukuwa ni kuimarisha mifumo ya Kisheria, Kitaasisi na udhibiti wa shughuli hizo,” amesema Mhandisi Sangweni
Mkurugenzi huyo wa PURA, amesema kuwa hatua hiyo imesaidia kuwepo kwa Sheria ya Petroli ya mwaka 1980, mikataba kifani ya ugawanaji mapato (Model PSA) kwa nyakati mbalimbali, Kanuni na miongozo mbalimbali na Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, ambayo kutokana na Sheria hiyo Taasisi ya PURA ilianzishwa.
SHUGHULI ZA MKONDO WA JUU
Akielezea kuhusu Taasisi ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Sangweni amesema kuwa ilianzishwa mwaka 2015, kupitia Sheria ya petroli ya mwaka 2015 ambapo ilianza shughuli zake rasmi mwezi Februari 2016 kupitia Kamati Maalumu iliyoundwa na Watumishi kutoka iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini na kutoka TPDC.
Amesema kamati hiyo, ilikuwa ikitekeleza majukumu ya Kisheria ya taasisi huku ikiendelea na maandalizi ya nyaraka mbalimbali za kuwezesha taasisi kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
MIAKA MINANE YA PURA
Mhandisi Sangweni, amesema kuwa kwa sasa PURA ina miaka minane na inatekeleza majukumu yake kama yalivyoaisnishwa kwenye Sheria ya Patroli 2015, kifungu cha 12.
Akifafanua kuhusu majukumu hayo, amesema kuwa yamegawanyika katika makundi makuu matatu ambayo ni pamoja na Kuishauri Serikali kupitia Waziri mwenye dhamana ya nishati hususani mafuta na gesi juu ya masuala yanayohusu shughuli za mkondo wa juu wa petroli, Kudhibiti na kusimamia shughuli zote za mkondo wa juu wa petrol na kusimamia miradi ya kubadili gesi kuwa katika hali ya kimiminika (Liquified Natural Gas – LNG).
“Hapo awali shughuli hizi zilikuwa zikitekelezwa na TPDC baada ya kukasimishwa na Kamishna wa Mafuta na Gesi. Shughuli hizi za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi nchini zinatekelezwa kwa kupitia mikataba ya ugawanaji mapato yaani Production Sharing Agreements – PSA, ambapo Kampuni kubwa za mafuta duniani huingia mkataba na Serikari na kuwekeza katika nyanja hiyo,” amesema
KAMPUNI ZENYE MIKATABA
Mhandisi Sangweni, amesema kuwa kwa sasa kuna Kampuni zipatazo nane ambapo mikataba iliyopo ni kumi na moja (11); kati ya mikataba hiyo, mitatu ipo katika hatua ya uzalishaji na uendelezaji wa gesi asilia wakati iliyobaki bado ipo katika hatua ya utafutaji.
“Kwa upande mwingine katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, PURA katika kutekeleza majukumu yake imewezesha kupatikana kwa mafanikio kadhaa.
“Kuimarika kwa shughuli za Kaguzi za Gharama katika Mikataba ya Uzalishaji na Ugawanaji Mapato (PSA Audit), iliyopelekea kuokoa fedha kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 189 kwa kurudishwa kwenye mfuko wa ugawanaji wa mapato kati ya Serikali na Waendeshaji wa Vitalu husika
“Kuimarika na kuongezeka kwa ushiriki wa Wazawa katika miradi ya utafutaji
na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini. Wastani wa ushiriki wa Wazawa katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli kupitia ajira ni asilimia 85, kushauri Serikali na kufanikisha kuongezwa kwa muda wa leseni ya utafutaji katika Vitalu vya Tanga, Ruvu, Mtwara na vitalu Namba 1, 2 na 4 vilivyopo baharini.
“…kushauri Serikali na kufanikisha utiaji saini kwa mkataba wa nyongeza wa uzalishaji na ugawanaji mapato ya gesi iliyogundulika Ntorya katika kitalu cha Ruvuma. Mkataba huo ambao utekelezaji wake utawezesha kuendeleza gesi asilia ya Kitalu hicho ya takriban Futi za Ujazo Trilioni 1.6 ulisainiwa baina ya Wizara ya Nishati, TPDC na Kampuni ya ARA (Oman),” amesema Mhandisi Sangweni
Licha ya hali hiyo pia amesema kuwa hatua ya kuongezeka kwa wastani wa uzalishaji wa gesi asilia kufikia futi za ujazo Bilioni 53.19 kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Februari 2023 ukilinganisha na futi za ujazo Bilioni 46.96 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2021/22, sawa na ongezeko la asilimia 14.
“Kukamilika kwa maandalizi ya rasimu ya Ramani ya Kidijitali (Interactive Digital Petroleum Reference Map) kwenye Mfumo wa Taarifa wa Kijiografia (Geographical Information System – GIS) inayotoa taarifa za Vitalu vya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini,” amesema
Amesema moja kati ya mkakati wa PURA ni kuhakikisha wanachmba gesi asilia nchini ambayo itakuwa na uwezo wa kupakiwa vizuri na Kwenda kuuzwa katika nchi mbalimbali duniani.
Mhandisi Shangweni, amesema mkakati huo ni kuhakikisha wanashika soko hilo katika nchi za Japan Korea.
CHANGAMOTO
Akizungumzia kuhusu changamoto, amesema kuwa tangu kupata uhuru Tanzania imepitia changamoto mbalimbali katika eneo la utafutaji wa mafuta na gesi.
Kutokana na hali amesema kutokana na hali hiyo bado changamoto zilizojitokeza zilipatiwa ufumbuzi na hatimaye kufikia hatua tuliyopo ambapo kumefanyika ugunduzi wa gesi asilia nyingi ambayo matumizi yake yana manufaa makubwa kwa Taifa na hasa hasa kwenye kuinua uchumi wetu.
“Kipekee kabisa nachukua nafasi hii kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mazungumzo ya utekelezaji wa mradi wa usindikaji wa gesi asilia kuwa katika hali ya kimiminika (yaani LNG project), mradi ambao utaliletea Taifa manufaa makubwa kwa kuanzia fedha, ajira, uanzishwaji wa viwanda vinavyotumia gesi kama malighafi pamoja na uuzaji wa bidhaa mbalimbali.
“Nachukua nafasi hii kwa mara nyingine kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa miongozo na maelekezo ambayo yamewezesha ustawi wa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini. Aidha, naishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Kwa upande mwingine shukrani zangu ziende kwa viongozi na watumishi wa Wizara ya Nishati, ambayo inaongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko, kwa miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyowezesha utekelezaji wa majukumu yetu ipasavyo,” amesema