Home KITAIFA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YAKAGUA MRADI WA...

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YAKAGUA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI LA AFRIKA MASHARIKI (EACOP)

Google search engine
Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka (aliyemwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati) akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kukagua  Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) unaoendelea katika kata ya Chongoleani -Tanga 
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk. David Mathayo akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kukagua ujenzi wa  Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) unaoendelea katika kata ya  Chongoleani -Tanga 
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. David Mathayo (wa nne kushoto) pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka (wa sita kulia) wakipatiwa maelezo ya ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) na Meneja wa Mradi, Mhandisi Mathieu Fayet huko Chongoleani, Tanga.
 
 
Mwonekano wa eneo la ujenzi wa bandari ya kituo kikuu cha kupokea mafuta  ghafi kwenye Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) ikiendelea na ujenzi. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefika na kujionea maendeleo ya ujenzi wa mradi huo katika eneo la Chongoleani, jijini Tanga 

Na Theresia Lugwisha

– Tanga

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea kituo Bandari Chongoleani cha Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) na kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.

Kamati hiyo imetembelea Novemba 13, 2023 na kufanya ukaguzi wa mradi huo katika kituo kikuu cha kupokea na kuhifadhi mafuta ghafi Chongoleani, jijini Tanga.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. David Mathayo, ameongoza kamati katika ziara hiyo huku ikionesha kufurahishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa EACOP kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, jijini Tanga.

“Lengo la kamati ni kutembelea  mradi huu na kujionea kasi ya ujenzi na kwa kweli tumefurahishwa sana na kasi ya ujenzi. Tulikuja mwaka jana tukajionea maendeleo, lakini leo tumekuta mambo tofauti kabisa, maendeleo ya ujenzi yamekua kwa kasi kubwa sana,” amesema Dk. Mathayo.

Amewataka wananchi kuchangamkia fursa zitokanazo na mradi huo, akiutaja utasaidia kuongeza Pato la Taifa pindi utakapokamilika Desemba 2025.

“Mradi huu ukikamilika utasaidia kuongeza Pato la Taifa na ajira, hivyo nitoe rai hasa kwa wakazi wa maeneo ambayo mradi huu unapita wachangamkie fursa zitokanazo na mradi ili waweze kuongeza kipato cha familia zao,” amesema Dk. Mathayo.

Mwenyekiti huyo pia amesisitiza kuwa mradi huo ni muhimu utekeleze miradi ya kijamii katika maeneo yanayopitiwa na mradi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka amesema Wizara ya Nishati imepokea ushauri wa kamati na itasimamia vyema utekelezaji wake.

Amesema hadi kufikia Oktoba 31, 2023, serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ilikuwa imetoa jumla ya Dola za Marekani milioni 207 kama mchango wake kwenye  hisa ya kampuni ya EACOP, Watanzania 4,228 wameajiriwa na mradi, watoa huduma 146 wazawa walinufaika na kulipwa jumla ya Sh bilioni 355 wananchi 9,822 sawa na asilimia 99.2 wamelipwa fidia yenye jumla ya Sh bilioni 35 na kazi inaendelea vizuri.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mbuttuka, pia amesema kazi ya ujenzi wa mradi huo inaendelea kwa kasi. Utakamilika na kuanza kufanya kazi Desemba 2025 

“Mradi huu mpaka sasa umefikia sehemu nzuri na ajira zilizopo zimewapa kipaumbele zaidi wakazi wa maeneo ambayo mradi huu unapita, lakini pia tunatarajia kuona fursa nyingi zaidi zikiendelea kuchangamkiwa na wananchi, mradi huu utakamilika na kuanza kufanya kazi ifikapo Desemba 2025,” amesema Mbuttuka.

Ziara hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk. David Mathayo. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, (aliyemwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.) Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pia walikuwa sehemu ya ziara hiyo katika mradi wa EACOP.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here