Na MWANDISHI WETU
-SIMANJIRO
SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imesema inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo wa Madini ya Tanzanite wilayani Simanjiro mkoani Manyara na ina mipango ya muda mrefu na muda mfupi wa kuzitatua changamoto hizo.
Hayo yamebainishwa Novemba 17,2023 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa Madini ya Tanzanite , wafanyabiashara na wamiliki wa vitalu vya uchimbaji madini katika mkutano maalum ulioitishwa na Serikali ili kujadili changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga kutoa taarifa kuhusu kazi inayofanyika katika eneo hilo ikiwamo kuimarisha ulinza kwa wachimbaji hao kama njia ya kurahisha kazi zao.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga, amemtaka Meneja wa TANESCO Wilaya ya Simanjiro ifikapo Jumatatu kupeleka mpango kazi wa usambazaji umeme katika maeneo yanayohitaji huduma hiyo tofauti na ilivyo sasa ambapo sehemu kubwa ya Nishati ya Umeme ipo katika eneo ambalo kwasasa bado hawaitaji huduma hiyo.
Nao wachimbaji na wafanyabiashara ya madini ya Tanzanite walielezea juu ya changamoto walizonazo ikiwa pamoja na ukosefu wa Nishati ya Umeme katika migodi , mitobozano chini ya ardhi , ubovu wa miundombinu ya Barabara, kukosekana kwa minada ya kuuza madini , ukosefu wa maji na vituo vya afya, ukosefu wa mitaji ya kuendeleza uchimbaji na vifaa duni vya uchimbaji.
Akielezea kuhusu mikakati iliyopo ya kutatua changamoto hizo Waziri Mavunde amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kupitia upya kanuni za masoko, uongezaji thamani na kanuni za eneo tengefu la Mererani ili kufanikisha minada ya vito pasipo vikwazo.
Kuhusu suala la mitobozano, Waziri Mavunde amesema hakuna sheria inayoruhusu mitobozano katika uchimbaji madini kisheria leseni zote zina mipaka hivyo kila mchimbaji azingatie mipaka yake iliyopo katika leseni na kumtaka Afisa Madini Mkazi wa Mirerani kuhakiksha anakaa na wadau kutatua changamoto ili kuruhusu shughuli za madini ziendelee pasipo kuleta athari katika ukuaji wa sekta.
Akijibu hoja ya kuwepo kwa zahanati katika mgodi , Waziri Mavunde ameeleza kuwa mpango wa Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ni kujenga zahanati kumi na moja katika wilaya ya Simanjiro na zahanati moja itajengwa ndani ya mgodi ili wachimbaji waweze kupata huduma ya haraka.
Akifafanua kuhusu uwezeshwaji wa mitaji na vifaa vya kufanyia kazi , Waziri Mavunde amesema tayari timu maalum imeishakaa na taasisi za fedha na benki kuangalia namna bora ya kutoa mikopo kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini na kwasasa yapo maeneo ambao wameanza kunufaika na mkopo
Naye, Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea fedha za maendeleo katika sekta ya Afya , miundombinu ya Barabara ambapo sasa kuna mpango wa ujenzi wa zahanati 11 ,ujenzi wa barabara ya kuelekea katika mgodi wa Mirerani yenye urefu kilomita zaidi tano.
Ziara hii ilijumuisha pia Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dk. Suleiman Serera viongozi mbalimbali wa Serikali, kisiasa pamoja na kamati ya Usalama Mkoa wa Manyara.