Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
BENKIya NMB imetoa zaidi ya shilingi trilioni 1.8 kwa wanawake 168,600 wa Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) katika kipindi cha miezi 10 mwaka huu (kuanzia Januari hadi Oktoba) ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa benki hiyo katika kuchochea ukuaji wa uchumi endelevu.
Pamoja na mambo mengine, mkakati kabambe wa benki hiyo unalenga kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kote nchini.
Akizungumza wakati wa hafla iliyokutanisha baadhi ya viongozi wa benki na na uongozi wa vikundi mbalimbali vya wanawake iliyofanyika na benki hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Huduma Shirikishi wa Benki ya NMB Nenyuata Mejooli alisisitiza dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kusaidia ushirikishwaji wa kifedha kwa wanawake na kuongeza kuwa benki yake inaamini kuwa uwezeshaji wanawake ni chachu ya maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
“Katika benki ya NMB, tumejizatiti kuziba pengo la ushirikishwaji wa fedha na tutaendelea kufanyia kazi azma yetu kwa kufikisha huduma za kibenki kwa wasio na benki nchini kote wakiwemo wanawake kupitia falsafa yetu ya karibu yako. Kufikia sasa mwaka huu, tayari tumefungua akaunti milioni 2.3 mwaka huu,” amesema Mejooli
Mejooli amesema kuwa kama sehemu ya kutimiza dhamira yake ya uwezeshaji wanawake, benki yake mwezi Novemba mwaka 2020, ilizindua hati fungani yake ya ‘NMB Jasiri Bond’, jukwaa ambalo linalenga kuwawezesha na kuhamasisha ushirikishwaji wa kifedha kwa wanawake katika sekta mbalimbali si tu Tanzania bali Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Mchakato huu ulilenga kutoa mikopo nafuu kwa biashara zinazoongozwa na wanawake na biashara ambazo zinaathiri wanawake moja kwa moja,” amengeza.
Mejooli alibainisha kuwa benki yake itaendelea na kampeni za elimu ya masuala ya fedha nchini kote ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kujenga uwezo kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanawake.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Biashara kutika Benki ya NMB Alex Mgeni wakati wa hafla hiyo amebainisha kuwa benki hiyo tayari imeanza mipango ya kuanzisha kanzidata ya kitaifa ya wanawake itakayorahisisha utoaji huduma za kibenki kwa wanawake katika sekta mbalimbali.
Mgeni amesema benki yake tayari imeanza kutafakari upya jinsi ya kuendela kushirikiana na wanawake wajasiriamali ili kuwawezesha kuondokana na changamoto za kibiashara kwa kutoa bidhaa zinazotengenezwa na mahitaji mengine muhimu yasiyo ya kifedha ili kuendeleza ukuaji wao.
“Tayari tumeshatambua baadhi ya sekta muhimu na nia yetu ni kuhakikisha kwamba tunawaleta wanawake wote katika kanzidata yetu. Kanzidata hii itahakikisha kwamba tunatoa huduma za kibenki zilizotengenezwa mahususi na kwa wakati kwa wanawake,” amesema Mgeni .