NA MWANDISHI WETU, KISARAWE
KATIKA kuendeleza utamaduni wa Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI), Benki ya NMB imekabidhi msaada wa mabati 600 yenye thamani ya Shilingi Milioni 28.2 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Fatma Almasi Nyangassa kwa ajili ya shule tano za msingi za Halmashauri hiyo.
Makabidhiano hayo ymefanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Kisarawe, ambako Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Dismas Prosper, alimkabidhi DC Nyangasa mabati hayo, naye kuyakabidhi kwa Walimu Wakuu wa shule hizo, mbele ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Beatrice Dominic.
Shule zilizonufaika na msaada huo, ambao thamani yake ni sehemu ya asilimia moja ya faida baada ya kodi ya Benki ya NMB kwa mwaka jana, ni Kibasila (bati 200), Titu (bati 100), Panga la Mwingereza (bati 100), Mtunani (bati 100) na Vilabwa (bati 100).
Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Dismas Prosper, alisema thamani ya mabati hayo ya Sh. Mil. 28.2 ni sehemu tu ya kiasi cha Sh. Bil. 6.2 zilizotengwa na benki hiyo kusapoti jitihada za Serikali katika sekta za Elimu, Afya, Majanga na Mazingira kwa mwaka 2023.
“Tuko hapa kukabidhi mabati 200 yenye thamani ya Sh. Mil. 9.4 kwa Shule ya Msingi Kibasila, huku shule za Panga la Mwingereza, Mtutani, Titu na Vilabwa – kila moja tukiikabidhiwa mabati 100 yenye thamani ya Sh. Mil. 4.7, hivyo kufanya jumla kuu kuwa Mil. 28.2.
“Kiasi hiki ni sehemu ya Programu ya Uwekezaji kwa Jamii ambayo NMB tumekuwa tukiifanya kwa zaidi ya miaka saba sasa, ambako kwa mwaka huu peke yake tumetenga Sh. Bil. 6.2 kusaidia utatuzi wa changamoto zinazokwaza sekta za elimu, afya, majanga na mazingira.
“Mheshimiwa mgeni rasmi, elimu ni miongoni mwa sekta za kipaumbele kwa benki yetu na hii ni kutokana na ukweli kwamba ndio ufunguo wa maendeleo ya taifa lolote duniani, na wanafunzi wanaopata elimu mashuleni wanatokana na jamii iliyotufikisha NMB hapa tulipo,” alisema.
Alibainisha kuwa, usaidizi wao katika utatuzi wa changamoto za elimu, unalenga kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo inapambana kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa elimu bora mijini na vijijini na wao kama wadau, hilo ni jukumu lao.
DC Nyangassa kwa upande wake aliishukuru NMB kwa kujitoa kwao katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, na kwamba ingawa kutoa kupitia CSI ni utaratibu wa kawaida kwa taasisi hiyo, lakini kwa Serikali ni jambo kubwa linalopaswa kuungwa mkono na wadau wa elimu.
“Mnalofanya hapa NMB ni jambo kubwa sana kwetu, mnaunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia, ambayo kwa mwaka huu wa fedha, imetupa kiasi cha Sh. Mil. 443.42 kwa ajili ya maboresho mbalimbali ya miundombinu ya elimu Wilaya ya Kisarawe tu.
“Hii sio mara ya kwanza kwenu, mmefanya hivi kwa kutoa madawati mashuleni, vifaa tiba mahospitalini na zaidi ya yote mlikuwa nasi kuwezesha na kushiriki ‘Programu ya Kisarawesha’, inayolenga kuboresha mazingira ya kiuchumi kwa wanawake wa Kisarawe,” alisema DC Nyangassa.
Alisema yote hayo ni uthibitisho wa moyo wa kujali na kuthamini jamii walionao NMB, huku akiwapongeza Walimu wa shule zilizonufaika na msaada huo, kwa kufanya kazi kwa bidii licha ya ugumu wa mazingira ya kufundishia yanayozikabili shule zao.