Home BIASHARA BENKI YA NMB YAZINDUA RASMI TAWI JIPYA DUMILA

BENKI YA NMB YAZINDUA RASMI TAWI JIPYA DUMILA

Google search engine
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima (wa tatu kulia), akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Tawi jipya la Benki ya NMB Dumila lililopo mkoani Morogoro, wengine katika picha ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka (wa tatu kushoto), Afisa Mkuu wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia), Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya NMB, Rahma Mwapachu (kulia), Meneja Uendeshaji Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Lilian Silaa (kushoto) na wa pili kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango.Kabla ya hapo wananchi wa Dumila walikuwa wakisafiri umbali wa kilometa 30 kwenda Mvomero kufuata huduma za kibenki wakati kwenda Gairo kilometa 50, Kilosa kilometa 69 na Turiani kilometa 70.

Na MWANDISHI WETU

-MOROGORO

WANANCHI wa Mji wa Dumila wilaya ya Kilosa wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kati ya kilometa 30 hadi 70 kufuata huduma za kibenki baada ya benki ya NMB kufungua tawi jipya ambapo adha hiyo wamekuwa wakiipata kwa zaidi ya miaka 10 mkoani Morogoro.

Akizungumza katika uzinduzi wa benki hiyo Mji wa Dumila mkoani hapa, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi amesema wananchi wa Dumila na vijiji vinavyoizunguka walikuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilometa 30 hadi 70 kufuata huduma za kibenki katika matawi ya benki Turiani, Kilosa, Mvomero na Gairo hali iliyopelekea NMB kuwasogezea huduma ya kibenki kwa wananchi hao.

Mponzi amesema wananchi wa Dumila walikuwa wakisafiri umbali wa kilometa 30 kwenda Mvomero kufuata huduma za kibenki wakati kwenda Gairo kilometa 50, Kilosa kilometa 69 na Turiani kilometa 70.

“Hili tawi la Dumila ni tawi letu la tano kufunguliwa kwa mwaka huu na NMB baada ya matawi ya Kwa Mromboo Arusha kufunguliwa yakifuatiwa na tawi la Paje Zanzibar, Makongorosi Chunya Mbeya na Buhigwe Kigoma lengo likiwa kusogezea karibu huduma za kibenki kwa wananchi,”amesema Mponzi.

Ameongeza kufunguliwa kwa matawi hayo inafanya NMB kuwa na matawi 231 nchi mzima na kuendelea kuongoza kwa kuwa na matawi mengi kuliko benki yoyote Tanzania.

Meneja Idara ya Huduma za Kibenki na Sarafu kutoka Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Dodoma Kanda ya Kati, Lilian Silaa amesema kufunguliwa kwa tawi hilo iwe mkombozi kwa wananchi kupata huduma wanashida ya chenji, kubadili noti na sarafu mahali ya kubadilishia noti ni tawi la Dumila ili kusaidia kazi za benki kuu kwa wananchi.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema benki hiyo inawafikia wananchi wengi na kuwaomba wananchi kutumia benki hiyo kwa sababu Dumila ina shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo kilimo na ufugaji.

Malima amesema uwepo wa tawi hilo katika Mji wa Dumila utaongeza tija kwa wakulima kupata mikopo ya kilimo lakini na wafugaji kupata mikopo ya kunenepesha mifugo ili jamii inayoizunguma benki hiyo kunufaika kihuduma na kubadilika kiuchumi kwa mitaji yao kukua kwa sababu Dumila sasa ni Mji wenye shughuli nyingi za kiuchumi kwa kukuza biashara zao.

“Mkoa wa Morogoro tunashukuru uongozi wa benki ya NMB kwa kurejesha sehemu ya faida kwa jamii kwa kutoa zaidi ya sh200milioni katika sekta ya elimu, afya na huu ni wajibu wa kila taasisi kurejesha faida kwa jamii kwa kutoa misaada ya kila aina lakini leo NMB mmetoa tena meza 30 na viti 30 kwa shule ya sekondari ya Sokoine na madawati 53 kwa shule ya msingi Kwadoli vyote vikiwa na thamani ya sh11milioni na NMB mkoa wa Morogoro sh200milioni huduma za kijamii,” amesema Malima

Mkuu wa Mkoa pia aliipongeza lengo la  taasisi hiyo la kukopesha kiasi cha Sh Bilioni moja kwa wajasiriamali, wafanyabiashara, wakulima na wafugaji kwa mwaka wa kwanza, huku akiwataka Wana Dumila, Kilosa na Morogoro kwa ujumla, kuchangamkia fursa za ujio wa tawi hilo alilolitabiria kuwa kinara kimafanikio kuliko matawi yote ya mkoa huo.

RC Malima amesema Dumila ni miongoni mwa miji ya kibiashara inayokua kwa kasi na kwamba ukubwa wa mtandao wa NMB, uimara wake kimapato na huduma rafiki kwa wateja, vinaenda kuneemesha na kuwastawisha kiuchumi wafanyabiashara, wajasiriamali, wakulima na wafugaji wa kada zote watakaotumia fursa hiyo.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here