Na MWANDISHI WETU
-MWANZA
KAMPUNI ya kizalendo ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG) imeahidi ukarabati wa viwango na kukamilika kwa wakati baada kupewa kazi ya kukarabati meli kongwe ya abiria na mizigo MV. Liemba iliyopo mkoani Kigoma (Ziwa Tanganyika), MV. Ukerewe pamoja na meli ya MT. Nyangumi zinazofanya kazi Ziwa Victoria.
Akizungumza jijini Mwanza mara baada ya kusaini mikataba hiyo mitatu ya ukarabati wa meli hizo na Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL) yenye thamani ya zaidi bilini 48, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG), Rayton Kwembe amesema:
“Tunaaidi ukarabati uliotukuka na wenye viwango ambapo kwenye utekelezaji huu tunafanya kwa ushirikiano na Kampuni ya M/S Brodosplit JSC ya nchini Croatia kwa garama ya Zaidi ya shilingi bilioni 48.”
Mkurugenzi huyo amesema kuwa ukarabati wa meli kongwe ya abiria na mizigo MV. Liemba utatumia gharama ya shilingi bilioni 32 wakati ukarabati wa MV. Ukerewe utafanywa kwa shilingi bilioni 6 wakati ukarabati wa meli ya MT. Nyangumi utafakinishwa kwa gharama ya shilingi bilioni 8.
Kwembe aliongeza: “Kampuni yetu ya DMG inaishukuru sana serikali yetu ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuamini na tunaiahidi Serikali kuwa kamwe hatutawaangusha katika utekelezaji wa miradi hii.”
Alisisitiza kwa kusema, “Tutajitaidi kwa hali na mali kuhakikisha kuwa miradi hii ya ukarabati tunaifanya kwa muda muafaka ili meli hizi ziweze kuendelea kufungua fursa nyingi za ajira binafsi na kupunguza gharama za usafirishaji sambamba na kuongeza tija katika shughuli za biashara hivyo kuwafanya wananchi wengi kunufaika.”
Mkuruenzi huyo wa DMG alidokeza kuwa kampuni yao ina uzoefu wa muda mrefu na utaalam wa kushiriki katika miradi mikubwa inayohusisha matengenezo ya meli na uundaji kwa ujumla kutoka hatua ya awali mpaka kukamilika.
Alibainisha: “Lakini pia Kampuni yetu ya DMG ipo katika mahusiano mazuri na taasisi za fedha ambapo mahusiano haya yanatusaidia kupata fedha stahiki kwa wakati pale zinapoitajika ili kusaidia miradi yetu kwenda na muda ulipangwa.”
Alisisitiza: “Ili kutekeleza vyema miradi ya ujenzi wa meli na matengenezo yake, DMG ilianzisha Idara ya kushughulikia mambo hayo mwanzoni mwaka 2017 kwa nia ya kutatua changamoto zinazoikabili Sekta hii iliyo katika uchumi wa bluu kwa kuleta maendeleo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (Mscl), Eric Hamissi amesema Serikali imeamua kuwekeza katika ukarabati wa meli hizo kutokana na uimara wake na kuokoa gharama ya kujenga au kutengeneza meli mpya.
“Kuna watu walikuwa wananiuliza kwanini Serikali inafanya ukarabati wa meli hii sasa ni wajibu kwamba mbali na meli hizi kuwa na miaka mingi lakini gharama za kutengeneza meli mpya kama hizi moja ni zaidi ya Sh120 bilioni lakini pia baada ya wataalamu kuchunguza meli zilizopo tulibaini bado vyuma vyake vina ubora mkubwa na havina uchakavu ndio maana Serikali ikaamua kuwekeza,” amesema Hamissi.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba mitatu ya ukarabati wa meli uliofanyika katika Bandari ya Kusini jijini Mwanza, Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile ametaka ukarabati huo kuzingatia muda wa mkataba.
“Nitumie fursa hii kuwaomba wananchi jiandaeni kutumia fursa hii ya miradi ambayo inatekelezwa na Serikali na popote pale tunapofanya miradi
naomba wananchi wenyeji wapewe kipaumbele cha kupewa ajira na nitoe rai kwa kwa viongozi wa mikoa kusimamia vyema na kuhakikisha mnalinda na mnapinga uhujumu uchumi katika miradi hii,” amesema Kihenzile.