*RAIS SAMIA AIMWAGIA MABILIONI YA FEDHA, WAKANDARASI WASAMBAA KILA KONA, MATUMIZI NISHATI JADIDIFU YAPIGIWA CHAPUO
Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM
WAKALA wa Umeme Vijijini (REA), umemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha ili kufanikisha hatua ya usambazaji umeme katika vijiji vyote nchini.
Kutokana na hali hiyo REA imesema kuwa ifikapo Juni 30, mwaka 2023 vijiji vyote 12,318 vitakuwa na umeme sambamba na kuimarisha njia za kusafirisha.
Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari leo Novemba 23, 2023 jijini Dar es Salaam, katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu, amesema kuwa tangua ilipoanzishwa REA walikuwa maeneo ya vijijini yaliyokuwa na umeme ni asilimia mbili.
Kutokana na hali hiyo, Mhandisi Jones Olotu amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati Vijijini kwa Sheria ya Nishati Na 8 ya mwaka 2005 na kuanza kazi rasmi Oktoba 2007 wamekuwa wakifanyakazi ya usambazaji wa umeme vijiji.
Aidha, mpaka sasa jumla ya vitongoji 28,659 vimefikiwa na umeme kati ya vitongoji 64,760 vilivyopo nchini.
“Kutokana na hali hiyo tulijiwekeza lengo la kufanya utafiti alau tufike maeneo ya vijijini kwa asilimia 50 lakini kutokana na utafiti ambao umefanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebaini kwamba sasa wanaopata umeme maeneo ya vijijini ni asilimia 69.9 na sasa tupo mbioni tena kufanya utafiti mwingine ili tuone tumefika asilimia ngapi.
Jambo moja ambalo napenda kueleza hapa kwamba ifikapo Juni 30, mwaka 2024 miradi yote ya umeme katika vijiji vyote Tanzania itakuwa imekamilika na kuunganisha vijiji na baada ya hapo tutaanza kugeukia vitongoji,” amesema
“Wakala wa Nishati Vijijini umeendelea kuhamasisha na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini katika maeneo mbalimbali kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara. Miradi hiyo ni pamoja na kuongeza wigo wa Gridi ya Taifa kufikia kwenye vijiji na vitongoji vyote nchini ili kuwafikishia huduma wananchi wengi zaidi vijijini.
“Miradi ya nje ya gridi inayojumuisha mifumo midogo ya kuzalisha na kusambaza umeme katika maeneo ambayo yna vyanzo vya nishati jadidifu yaani Renewable Enegy Source ikiwamo kufunga mifumo ya umeme jua katika taasisi za Serikalin a maeneo ya huduma ya jamii zilizoko vijijini (Stand alone Solar PV Systems) pamoja na kusambaza nishati safi na salama ya kupikia ambapo wakala umewezesha ujenzi wa mitambo ya biogesi majumbani na katika taasisi za elimu.
“Na katika hili moja kati ya tukio ambalo mwaka 2012 tukiwa Mbiga mkoani Ruvuma wakati mama mjamzito anajifungua mume wake alikuja hospitali na kibatari chake. Alipofika akashangaa kukuta tayari tumefunga Solar yule mzazi aliona ni muujiza na pale yule mtoto akampa jina Solar. Si haya yapo mengi ambayo pia yamesaidia kuleta mapinduzi katika sekta ya nishati hasa maeneo ya vijijini kubwa tunaomba jamii itambue Serikali imedhamiria kuleta maendeleo ya kweli ambayo sasa yanaonekana.
Mhandisi Olotu, amesema kuwa jambo ambalo wanajivunia ni kwamba REA imefanikiwa kubadili maisha ya wananchi maeneo ya vijijini kwa kuruhusu shughuli mbalimbali kiuchumi kufanywa na vijana katika maeneo hayo, ikiwamo suala la uchomeleaji wa madirisha, vinyozi na kuuza vimiminika vya baridi jambo ambalo lilikuwa likifanyika katika maeneo ya mijini pakee.
REA AWAMU YA TATU KUTIKISA NCHI
“Mradi wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III Round II). Mradi huu unahusisha kupeleka umeme kwenye vijiji 4,071 vilivyobaki kati ya vijiji vyote 12,318 pamoja na kujenga njia za umeme wa Msongo wa Kati zenye urefu wa kilomita 23,526, kujenga njia za umeme wa Msongo mdogo zenye urefu wa kilomita 12,159, kufunga mashineumba 4,071 na kuunganisha wateja wa awali wapatao 258,660.
“Mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kwa kiasi cha Shilingi trilioni 1.58. Mradi huu kwa sasa upo katika hatua ya utekelezaji
ambapo unatarajiwa kukamilika Disemba 2023 kwa mikataba 32 na Juni 2024 kwa mikataba saba (7). Utekelezaji wa mradi kwa sasa umefikia wastani wa asilimia 73,” amesema Mhandisi Oloto
MRADI WA KUSAMBAZA UMEME KWENYE VITONGOJI
Mhandisi Olotu, amesema kuwa pia REA ina Mradi wa Kusambaza Umeme katika Vitongoji – (Hamlet Electrification Project – HEP), ambapo baada ya kukamilika kwa mradi wa kupeleka umeme katika Vijiji, Serikali imepanga kufikisha umeme katika vitongoji ili kuhakikisha kuwa umeme unafika na kutumika maeneo ya vijijini Tanzania Bara.
Amesema Serikali kupitia REA ilifanya utambuzi wa wigo wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji vyote Tanzania Bara na kubaini kuwa vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na miundombinu ya umeme nchini ni 36,101 kati ya vitongoji 64,760 vilivyopo Tanzania Bara.
“Aidha, gharama za kufikisha miundombinu ya umeme katika vitongoji hivyo (36,101) ni Shilingi trilioni 6.7 Serikali ilipata mkopo wa gharama nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kupitia dirisha la Extended Credit Facility ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 100 zitatumika kuanza utekelezaji wa mradi huu katika vitongoji 654 katika mikoa ya Songwe na Kigoma na hivyo kufanya vitongoji ambavyo havina umeme kuwa 36,101,” amesema
MRADI WA UJAZILIZI MZUNGUKO WA PILI B
Mhandisi Olotu, ameutaja mradi huo kuwa unalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vitongoji 1,686 katika mikoa ya Arusha, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Lindi, Morogoro, Njombe na Songwe na kuunganisha jumla ya wateja wa awali 95,334. Gharama ya mradi huu ni Shilingi bilioni 234.4.
Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).
MRADI WA UJAZILIZI MZUNGUKO WA PILI C
Amesema mradi huo unalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vitongoji 1,880 katika mikoa ya Manyara, Iringa, Rukwa, Mtwara, Ruvuma, Simiyu na Mara kwa kujenga kilomita 6,562 za msongo mdogo na kufunga mashineumba 1,932 ili kuunganisha wateja wa awali 131,719.
“Gharama ya mradi huu ni Shilingi bilioni 293 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na Serikali za Norway na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Mhandisi Olotu
Pia amesema wana mradi mwingine wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme Ifakara (220/33kV, 1x20MVA) na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji umeme.
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa Kituo cha kupoza Umeme cha Ifakara na Ujenzi wa Njia ya Kusambaza Umeme Vijijini (Wilaya za Kilombero na Ulanga).
“Mradi unalenga kuwezesha na kuimarisha shughuli za kilimo katika eneo la Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania kwa kuwapatia wananchi huduma za umeme. Gharama za mradi ni Shilingi bilioni 23.62 ambazo zinalipwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya.
“Mradi huu utawezesha wateja wapatao 1,853 kuunganishiwa umeme katika vijiji nane na vitongoji saba,” amesema
MRADI WA PERI URBAN AWAMU YA PILI
Amesema mradi huo unahusisha kupeleka umeme katika maeneo 153 yaliyopo katika majiji ya Arusha, Dodoma na Mwanza kwa kujenga miundombinu ya kusambaza umeme yenye urefu wa kilomita 751, kufunga mashineumba 143 na kuunganisha wateja wa awali 16,328. Gharama za mradi ni Shilingi bilioni 31.33.
MRADI WA PERI URBAN AWAMU YA TATU
Mhandisi Olotu, amesema mradi huo unahusisha kupeleka umeme katika maeneo 416 katika mikoa nane ya Geita, Kigoma, Kagera, Mbeya, Mtwara, Singida Tabora na Tanga. Gharama ya mradi huu ni Shilingi bilioni 76.9 ambazo zinatolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwezesha kuunganisha umeme kwa wateja wa awali 22,105.
“Mradi wa Kupeleka Umeme katika Vituo vya Afya na Pampu za Maji ili Kuzuia Magonjwa ya Kuambukiza na UVIKO-19. Mradi huu unahusu kusambaza umeme kwenye Vituo vya Afya 66 na Pampu za Maji 333 vilivyopo vijijini katika mikoa 25 Tanzania Bara. Gharama ya mradi huu ni Shilingi bilioni 34.5. Mradi huu unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya.
“Mradi wa Kupeleka Umeme katika maeneo ya Wachimbaji Wadogo wa Madini, Viwanda na Kilimo, mradi huu unahusu kupeleka umeme katika maeneo 114 ya wachimbaji wadogo wa madini, maeneo 222 ya kilimo na viwanda katika mikoa 25 Tanzania Bara. Mradi unatarajiwa kuunganisha wateja wa awali 19,187 kwa gharama ya Shilingi bilioni 115 ikiwa ni fedha za ndani,” amesema
MWELEKEO WA NISHATI JADIDIFU NCHINI
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage, amesema kuwa REA ni Wakala wa Nishati Vijijini lakini pia kazi yao kubwa waliyofanya inatokana na mkakati wa kutumia nishati mbalimbali.
Amesema moja ya kazi kubwa pia ni kuhakikisha wanapeleka huduma ya nishati ikiwamo mbadala kama mitungi ya gesi ikiwamo katika ya vijijini kama njia ya kuimarisha uchumi kwa jamii.
“Kuna Visiwa 196 pia yapo maeneo ambayo ni Delta yenye majimaji ambapo ni lazima tutafute mbinu mbadala kuhakikisha wanapata huduma ya umeme. Tumefanikiwa kuwa na miradi hiyo katika shule za umma, vituo vya afya na polisi kwa maeneo ya visiwa na Delta kama Rufiji ambapo maeneo mengi yamezungukwa na maji.
“REA haimiliki mrai ila inawezesha kutoa ruzuku, kazi kubwa ambayo tunafanya sasa na kufikia mwaka 2025 vijijini vyote vipate umeme,” amesema Mhandisi Advera
Mbali na hilo pia wamekuwa na miradi kama ya kutengeneza vitofali vya kupikia (charcoal briquettes), kuhamasisha na kusambaza gesi ya kupikia (LPG) na majiko banifu.
“Tuna mradi wa kupeleka umeme katika Shule na Mahakama za Mwanzo Vijijini, mradi huu unahusu kupeleka umeme katika shule 729 na mahakama za mwanzo 292 vijijini ambazo hazina umeme. REA na TANESCO wapo katika hatua za mwisho za kusaini makubaliano ambapo TANESCO itafanya kazi ya kuzipelekea umeme katika shule na mahakama hizo na REA itakua inatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji.
MRADI WA KUPELEKA UMEME VISIWANI
Amesema kuwa mradi huu unajumuisha ujenzi wa mifumo midogo ya kusambaza umeme katika maeneo yenye vyanzo vya nishati jadidifu kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ambapo ambapo mikataba miwili ya miradi wa Ikondo-Matembwe Hydro Power ulisainiwa Februari, 2023 na mkataba wa mradi wa Mwenga Hydro Power ulisainiwa Machi 2023.
“Miradi hii itaunganisha jumla ya wateja wa awali 2,168 katika vijiji 42 kwa gharama ya Shilingi 3.06 bilioni. Aidha, Serikali kupitia REA imewapata waendelezaji watatu ambao ni Jumeme, Volt Africa na Green Leaf Technology wa miradi ya kusambaza umeme kwa kutumia nguvu ya jua, itakayotekelezwa katika visiwa 28 vilivyopo katika mikoa ya Kagera (8), Mwanza (13), Mara (3) na Lindi (4) na hivyo kuunganisha wateja 9,515 kwa gharama ya Shilingi bilioni 11.18.
UTEKELEZAJI WA MRADI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA VIJIJINI
Mhandisi Advera, amesema kuwa mradi wa usambazaji wa Mitungi ya Gesi ya Kupikia (LPG), Wakala umeanza kutekeleza Mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia kwa utaratibu wa utoaji ruzuku kuwezesha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) 71,000 yenye thamani ya shilingi bilioni 3 na mpaka sasa mitungi 42,000 imeshasambazwa.
“Kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 Jumla ya fedha takribani Shilingi bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kusamabaza mitungi ya gesi ya kupikia na kwa sasa Wakala umeshatangaza kwa ajili ya wasambazaji wa mitungi kuomba.
“Mradi wa Kusambaza Gesi Asilia (CNG), kusambaza gesi asilia ya kupikia katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani (Pembezoni mwa Mkuza wa Bomba Kuu la Kusafirisha Gesi Asilia), ambapo utekelezaji wa mradi huu utahusisha REA na TPDC;
“Mradi huu utahusisha ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia (CNG) lenye urefu wa km 44.4 (Mnazi Mmoja – Lindi (km 22.9) na Mkuranga – Pwani (km 21.5) na Jumla ya nyumba/wateja 980 kunufaisha (Mnazi Mmoja – Lindi, wateja 451 na Mkuranga-Pwani, wateja 529), Wakala umeshalipa awamu ya kwanza ya makataba na ununuzi wa vifaa unaendelea
“…kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 Jumla ya TZS bilion 20 zinatarajiwa kutumika katika kuongeza miundombinu ya kusamabaza gesi asilia samba na mradi wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Utaratibu wa Malipo kwa Matokeo (RBF) Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) imetenga Dola za Kimarekani (USD Milioni 6) kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa majiko banifu ya kupikia na takribani majiko 200,000 yanatarajiwa kusambazwa katika maeneo mbali mbali ya vijijini na vijiji miji (Peri Urban) Tanzania Bara,” amesema