Na Mwandishi Wetu
Benki ya NMB jana imekabidhi mashuka 500 yenye thamani ya shilingi milioni 9 kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ilikuboresha mazingira kwa wagonjwa wa taasisi hiyo.
Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ilyofanyika katika taasisi hiyo jijini Dar es Salaam jana, Meneja ya Kanda ya Dar es Salaam ya Benki ya NMB Dismas Prosper alisema kuwa msaada huo ni utekelezaji wa mkakati wa benki hiyo wa Uwajibikaji Kwa Jamii (CSI).
“Kwa zaidi ya miaka saba sasa, benki yeku iliridhia kurudisha asilimia moja ya faida yetu kila mwaka katika kuchangia maendeleo ya jamii inayotuzunguka na sekta ya afya ni miongoni mwa vipaumbele vyetu vikuu. Tuna furaha kuwa leo tunakabidhi mashukaa 500 kwa Taasisi ya Jakaya Kikwete na tunaamini kuwa msaada huu utasaida kuboresha mazingira kwa wagonjwa,” alisema Prosper.
Prosper aliahidi kuwa benki yake inatendelea kufanya kazi na Serilaki kwa karibu kwa kutambua kuwa sekta ya afya ni nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Peter Kisenge aliushukuru uongozi wa benki ya NMB kwa msaada huo huku akibainisha kuwa taasisi yake imendelea kuimarika zaidi kutokana na michango mingi inayotolewa na wadau.
“Miongoni mwa wadau hao ni benki ya NMB. Benki hii imekuwa ikitoa kipaumbele katika maendeleo ya taasisi yetu kwa kutoa michango mbalimbali. Nia ya Serikali yetu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora bila kujali ana uwezo gani,” alisema.
Alisema taasisi yake miaka michache ilaanzisha mpango maalum wa ‘Mama Samia Outreach Program’ ambao tayari umeweza kuwafikia watu 12,000 katika mikoa 12 nchini kwa ujumla.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo wakati wa hafla hiyo aliishukuru benki ya NMB kwa kuendelea kuchangia jitihada mbalimbli za maendeleo za Serikali huku akizitaka kampuni na taaisi nyingine kuiga mfano huo.
“Zipo taasisi nyingi zinazopata faida katika mkoa wetu wa Dar es Salaam na zote zingekuwa zinawajibika ipasavyo kama benki ya NMB, basi mkoa wetu ungepiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo,” alisisitiza.
Awali, Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Angela Muhozya ambae pia ni Kiongozi wa Umoja wa Wanawake katika JKCI alibainisha kuwa msaada huo ni utekelezaji wa ombi la umoja wao kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka jana.