*Tembo watajwa kuongoza, 108 wauawa kwenye makazi
*JET, Shirika la Maendeleo la Ki jerumani-Tanzania (GIZ), wajifungia kutafuta suluhu
Na MWANDISHI WETU
-BAGAMOYO
MIGONGANO baina ya binadamu na wanyamapori nchini imetajwa kuwa changaoto kubwa huku Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ikisema ili kukabiliana na migongano kati ya binadamu na wanyamapori ni vema wadau washirikiane kwa pamoja kutoa elimu kwa jamii juu faida za uhifadhi, mazingira na viumbehai waliopo.
Akizungumza hivi karibuni mjini Bagamoyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mapepele katika mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikina na Shirika la Maendeleo la Ki-jerumani-Tanzania (GIZ) kuhusu Miradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori, amesema ni lazima jamii ikubaliane umuhimu wa wanyama pori kama nyenzo muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Mradi huo ambao unatekelezwa katika vijiji 30 vilivyopo wilaya za Liwale mkoani Lindi, Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa kushirikiana na JET pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mapepele amesema hakuna njia mbadala ya kumaliza migongano ya binadamu na wanyamapori tofauti na wadau kushiri kutoa elimu, huku akiwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kwa kuandika habari zenye mtazamo chanya ili jamii iweze kubadilika kwa haraka.
Mkuu wa Kitengo amesema lengo la mradi huo ni kuwajengea uelewa jamii inayoishi karibu na maeneo ya hifadhi, ili wawe na uwezo wa kudhibiti na kutatua changamoto baina yao na wanyamapori, huku wakiamini kuwa wanawajibu wa kuishi nao kwa upendo.
“Migongano baina ya binadamu na wanyamapori ipo na haiwezi kuisha kwa haraka, kinachotakiwa ni sisi serikali, wadau wa uhifadhi kama JET, GIZ na waandishi wa habari kuhakikisha tunatoa elimu kwa jamii inayoishi karibu na hifadhi, shoroba, mapori ya akiba na tengefu kuwa wanapaswa kuishi na wanyamapori kwa upendo, kutokana na ukweli kuwa asilimia kubwa binadamu ndio wameingia kwenye maeneo ya wanyamapori,” amesema.
Mapepele amesema matumaini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni kuwa kupitia mradi huo migangano baina binadamu na wanyamapori itapungua kama sio kuisha kabisa.
Mkuu huyo amesema sekta ya utalii inachangia asilimia 21 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni, hivyo hakuna namna ya kuacha migongano hiyo kuendelea, bali ni wadau wote kushiriki kutoa elimu kwa jamii, hali ambayo itachangia ongezeko la mapato.
Amesema sekta hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa jamii hasa vijana na makundi mengine hivyo elimu ikiendelea kutolewa ni wazi faida zitaongezeka kama ajira na uhifadhi.
Mapelele amesema uhai wa viumbehai vyote unategemea mazingira bora na rafiki, hivyo ili kuwepo na uendelevu ni jukumu la waandishi kuandika bahari za uchechemuzi kuhusu eneo hilo lenye fursa nyingi za kiuchumi.
Mkuu huyo amesema wizara yao inatumia mbinu mbalimbali kutangaza utalii nje na ndani ya nchi, hivyo haitapendeza juhudi hizo zipotee bila kuleta faida kwa jamii.
“Wananchi au jamii inayoishi karibu na hifadhi na misitu wanapaswa kufaidika na rasilimali zilizopo ila kwa utaratibu wa kisheria, lakini hilo watalijua iwapo nyie wandishi mtaamua kuliandika kwa kina na ufasaha,” amesema.
Amesema Tanzania inasifika kwa kuwa na wanayama wengi hali ambayo inavutia watalii, hivyo serikali itahakikisha fursa hiyo inakuwa endelevu, huku wanadamu nao wakipata haki zao.
Amesema kwa sasa sekta hiyo imezidi kupaa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia mwenyewe moja kwa moja kuitangaza, hivyo iwapo kutakuwa na migongano baina ya wanadamu na wanyamapori faida haitakuwepo.
Mshauri kutoka Shirika la GIZ, Anna Kimambo amesema wameamua kushirikiana na serikali kutoa elimu kwenye maeneo yenye migongano baina ya binadamu na wanyamapori, ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na uendelevu.
Amesema changamoto kwenye vijiji 30 vya mradi ni kubwa ila kwa ushirikiano ambao serikali na wadau wengine wakiwemo waandishi wa habari ni imani yao hali itakuwa nzuri na binadamu na wanyamapori wataishi pamoja kwenye hifadhi na shoroba.
“Tunaamini elimu ikitolewa kwa ushirikiano wa wadau wote, ikiwemo waandishi wa habari kuandika habari za ukweli na uhakika, hali itakuwa nzuri, kuna wakati unasikia habari mpaka unakosa amani, lakini msingi wake ni kukosekana taarifa sahihi, ila kupitia JET na nyie tunatarajia kuona na kusoma taarifa zenye tija kwa sekta hii,” amesema.
Kimambo amesema GIZ inatekeleza mradi huu wa mwaka mmoja kwa kutambua faida zilizopo kwenye uhifadhi, hivyo ni matumaini yake kila mdau atashiriki kuhakikisha mafanikio chanya yanapatikana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa JET, John Chikomo amesema chama hicho kimejipanga kikamilifu kuhakikisha waandishi wa habari wanaandika masuala ya uhifadhi, mazingira na shoroba.
Amesema wamechagua waandishi wachache na wameanza kwa kuwapatia mafunzo kuhusu eneo hilo na baadae wataenda kutembelea vijiji 30 kwa makundi ili waweze kuona hali ilivyo kuhusu migongano ya binadamu na wanyamapori.
“Tumewachagua nyie kwa kuzingatia mambo mengi, lakini pia hatutasita kumuacha mtu ambaye haendani na kasi yetu, JET tunataka mabadiliko chanya kwenye sekta ya utalii na maliasili, ili iweze kuchangia pato kubwa zaidi kwa nchi,” amesema.
KAULI YA TAWA
Akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa wanyama pori, Afisa Muhifadhi Tawa, ambaye pia ni Mdhibiti wa Wanyamapori Waharibifu, Isaac Chamba, amesema kuwa kwa sasa Tawa inajukumu la kusimamia mapori ya akiba 28, tengefu 23 ambayo yanasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Kutokana na hali hiyo amesemakuwa suala la migongano baina ya binadamu na Wanyamapori inasimamiwa chini ya Sera ya Uhifadhi Wanyamapori ya mwaka 1998 na maboresho yake ya mwaka 2007 kifungu cha 69 cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Sura pamoja na maboresho yake ya mwaka 2022
Amesema uwepo wa migongano baina ya binadau na wanyamapori nchini ni mojawapo ya changamoto za uhifadhi
“Changamoto hii ni ya kihistoria na ilishughulikiwa na Idara ya Wanyamapori hadi mwaka 2016 TAWA ilipoanzishwa. Katika kipindi hicho, tatizo lilikuwa la kiwango cha chini na athari ndogo kwa maisha na mali za watu.
“Mnamo 2018, kulikuwa na ongezeko la matukio ya migogoro ya binadamu na wanyamapori. Ongezeko hilo lilipelekea Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Migogoro ya Watu na Wanyamapori (2020-2024). Mkakati huo ulizinduliwa Oktoba 5, 2020 na unatekelezwa na TAWA, TANAPA, NCAA, TFS na TAWIRI na wadau wengine husika,” amesema Chamba
Amezitaja moja ya changamoto zinazosabaisha kuibuka kwa migongano baina ya binadamu na wanyamapori ikiwmo kuzibwa kwa shoroba za wanyama hao.
“Lakini pia mipango duni ya matumizi ya ardhi, kuingia kwa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, mabadiliko ya tabianchi, kupuuza ushauri unaotolewa na wataalamu kuhusu jinsi ya kuepuka athari za HWC pamoja kuwepo kwa kwa imani potofu katika baadhi ya jamii,” amesema
Chamba amesema kwa yapo malengo mkakati namna bora ya kupambana na hali hiyo ikiwamo kukabiliana na jamii
Mkakati mwingine ni kuhakikisha inatolewa elimu kwa jamii ili iweze kutambua faida kwa Jumuiya za kuishi pamoja kwa binadamu na wanyamapori pamoja na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa migongano ya binadamu na wanyamapori
MATUKIO YA MWAKA 2022/23
Afisa Muhifadhi huyo, amesema kuwa jumla ya matukio 2,817 yameripotiwa kuhusu mauaji ya wanyama wenye matatizo katika kulinda maisha ya binadamu
“Kwa mwaka 2022/2023 jumla ya wanyama pori 108 waliuawa. Lakini pia wanyamapori waiohamishwa kwa mwaka 017/18 hadi 2022/2023: Simba 60 na Fisi wawili walihamishwa kutoka makazi ya watu kwenda kwenye mapori mengine na mwaka huu wa Februari 2024 Simba watatu waliohamishwa,” amesema Chamba
Pamoja na hilo, amesema kuwa katika kukabiliana na hali hiyo, wamefanikiwa kujenga vituo vya katika maeneo ya mapori ya hifadh ambayo pia kuna askari ambao wamekuwa akishirkiana na askari wa jamii.
Amesema kwa mwaka 2021/22 TAWA ilijenga vituo 16 vya PAC katika wilaya zilizoathirika ikiwamo matumizi ya teknolojia
“Pia moja kazi iliyofanyika ni kuweka Kola za Satelaiti za GPS kwa wanyamapori hasa tembo ambapo ni gharama kwa Kola moja hugharimu hadi kiasi cha Shilingi milioni 15 jambo ambalo gharama kubwa kuliko uwezo wa TAWA.
“Novemba 2022 hadi Februari 2023 Kola tano (5) za GPS Satellite ziliwekwa kwenye makundi 5 ya tembo katika wilaya za Liwale, Nachingwea, Lindi vijijini na Tunduru,” amesema Chamba
MATUMIZI YA DRONES
Amesema TAWA imenunua ndege tatu zisizo na rubani nne za Mavic Pro, waliosomea (Tanzania Aviation College Dar es Salaam).
“Marubani wane wa ndege zisizo na rubani (Februari 2023) Marubani 10 wa ndege zisizo na rubani kwa ushirikiano na FZS Desemba 2023,” amesema
HELIKOPTA KUSWAGA TEMBO
Desemba 2022, TAWA iliswaga tembo wapatao 270 kutoka ardhi ya jumuiya kurudi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa katika wilaya za Liwale na Nachingweahuku Julai 2023 Tembo 284 katika wilaya za Same na Bunda.
MTAMBALIKE
Kwa upande wake Mkufunzi na Mwandishi Mkongwe, Pili Mtambalike amewataka waandishi wa habari kuandika habari ambazo zitaleta mabadiliko chanya kwa jamii husika.
“Mnatakiwa muandike habari zenye tija na zinazofuata misingi ya uandishi wa habari, eneo hili ni muhimu sana iwapo litaripotiwa kwa kufuata misingi ya uandishi,” amesema.