Na MWANDISHI WETU
-ZANZIBAR
RAIS wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa huduma ya utoaji wa msaada wa kisheria inayotolewa nchini inasaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi wanaohitaji msaada katika kesi za jinai na kiraia.
Rais Samia ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Jumuiya ya Madola, ufunguzi uliofanyika visiwani Zanzibar.
Amesema ili kufikia hilo serikali ilizindua Kampeni kubwa ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign-MSLAC), Kampeni ambayo inahusisha utoaji wa msaada wa kisheria na elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya kikatiba na kisheria, upatikanaji wa haki na masuala mtambuka kama vile ukatili wa kijinsia, ardhi, mirathi, haki za binadamu na utatuzi wa migogoro ikiwemo kuhamasisha utatuzi kwa kutumia njia mbadala.
“Kampeni hii inahamasisha wananchi juu ya haki zao na namna ya kupatikanaji haki hizo hivyo kutokana na hiyo, migogoro mingi ya ardhi, mirathi ya ndoa na GBV imetatuliwa katika ngazi za jami.
“Baada ya kuona uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria serikali ilitoa wito kwa wadau wengine kuchukua jukumu katika kutoa msaada wa kisheria, na tunashukuru sana kwa sababu tuna watu wanaojitolea, watendaji wasio wa serikali, ambao pia hutoa msaada wa kisheria kwa watu, Tunashukuru sana,” amesema ais Samia.