Na MWANDISHI WETU
-ZANZIBAR
MAMENEJA wa matawi ya Benki Zanzibar, wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kutoa huduma bora kwa wafanyakazi na wateja wanaofika katika benki hizo kupata huduma za kifedha.
Kauli hiyo imetolewa na mameneja hao walipotembelewa na Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Jamii kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Henry Mwaibambe, akiwa ameambatana na maofisa wengine ambapo walifanya ziara katika matawi mbalimbali ya benki Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja na kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo kupitia huduma inayotolewa na Jeshi la Polisi
Akizungumza na ujumbe huo Meneja wa Benki ya People’s Bank of Zanzibar (PBZ) Tawi la Malindi Mwalim Mussa Omar amesema askari wanaendelea kutimiza majukumu yao vizuri na kudumisha ushirikiano baina yao na wafanyakazi wa benki hiyo
“Siku moja kuna mteja alikuwa anapiga picha ndani ya benki na alipoonekana alikamatwa na askari, lakini kabla ya kupelekwa kituoni au kutoa taarifa kwa viongozi walinipa taarifa mimi kama Meneja mwenye dhamana na baadae tuligundua kuwa hakuwa na nia mbaya na picha hizo pia alikuwa mteja wetu mkubwa na tunamfahamu, hivyo kwa mazingira hayo yanaonesha namna ushirikiano uliopo,” amesema Mwalim Omar
Hata hivyo, alipongeza Jeshi la Polisi namna lilivyoshirikiana na wafanyakazi wa Benki ya PBZ tawi Forodhani kuokoa fedha Shilingi Bilioni 1.3 baada ya jengo la benki hiyo kuangukiwa na jengo jengine.
Nae Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Darajani, Naima Shaame amesema askari wanafanya majukumu yao kama walivyoelekezwa na inapotokea changamoto ya aina yeyote inatatuliwa kwa kushirikiana na viongozi wao pamoja na askari.
Naibu Kamishna Mwaibambe pia alifanya kikao na Maofisa, Wakaguzi na Askari ambapo aliwapongeza kwa kufanya majukumu yao kwa waledi na kuendelea kujenga heshima na imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi.
Aidha, amewataka kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na kutenda haki bila kumuonea mtu yeyote huku akisisitiza kujenga hazina ya matendo mema kwa jamii wanayoihudumia.
Ziara hiyo ililenga kusikiliza changamoto pamoja na kukagua benki hizo kwa namna gani zinawajibika kutengeneza mazingira salama na rafiki kwa askari.