*Vifaa vya milioni 12 vyatolewa, umeme wawashwa kwa mara ya kwanza katika Sekondari Ndogowe
Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
KATIKA kuadhimisha Siku ya Mwanamke Duniani, Jumuiya ya Wanawake Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) L wametoa msaada wenye thamani ya shilingi milioni 12 kwa waalimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ndogowe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chimwino.
Msaada huo umegawanyika katika makundi mawili ambapo kiasi cha Shilingi milioni sita zimetumika kununua vifaa vya umeme pamoja na kufanya Wiring (Huduma ya kuunganisha umeme) kwenye vyumba nane vya madarasa katika shule hiyo ambapo kiasi cha Shilingi milioni sita zimetumika kununulia Kompyuta mpakato (Laptop), mashine ya kudurufu (Printer, Photocopy & Scanner) pamoja na kununua wino na shajala kwa waalimu na wanafunzi wa shule hiyo.
Katika hotuba yake; Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema lengo la msaada huo ni kuunga mkono kwa vitendo maelekezo ya Serikali ambayo yanatoa kipaumbele kwa taasisi za Serikali kama shule kuunganishwa na miundombinu ya umeme.
“Mnaweza kuona hii miundombinu ya umeme, imetoka mbali lengo la Serikali ni kujenga mazingira wezeshi kwa waalimu na wanafunzi katika kujifunza na kupata maarifa,” amesema Mhandisi Advera.
“Sisi wanawake wa REA, tuliamua kujichangisha toka mwaka jana (2023), tulichangishana kidogo kidogo na tulikubaliana kuwa katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu wa 2024, tulisema, tutatafuta shule ya sekondari iliyopo Mkoa wa Dodoma ambayo haina miundombinu ya umeme ili tuiunganishe (Wiring) na huduma ya umeme,” amesema
Aidha Mhandisi, Advera ametoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye sekta ya elimu pamoja na kulinda na kutunza miundombinu hiyo kwa kuwa fedha nyingi zimetumika katika kuijenga.
Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Mbadala, ametoa shukran kwa jumuiya ya watumishi wanaume wa REA kwa kuwaunga mkono harakati hizo ambapo imeelezwa kiasi cha Shilingi milioni sita zilizochangwa na wanaume kwa ajili ya kuwaunga mkono wanawake katika kutimiza adhma hiyo.
Kwa pande wake geni rasmi katika hafa hiyo, Afisa Tarafa Sosthenes Chakupanyuka ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Gift Msuya, amewapongeza jumuiya ya watumishi wanawake wa REA kwa kuunga mkono maendeleo ya sekta ya elimu kwa vitendo na kutoa wito kwa makundi mengine katika jamii kufanya vivyo hivyo.
“Umeme utarahisisha masomo, huku vifaa vya TEHAMA vitaongeza ufanisi katika kujifunza na nina uhakika ufaulu utapatikana kwa wanafunzi wetu,” amesema Chakupanyuka.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Ndogowe, Hamis Suleiman amewashukuru wanawake watumishi wa REA kwa kuwa sehemu ya kutatua changamoto na uhitaji wa vifaa katika shule hiyo na kuongeza kuwa yeye na waalimu wenzake watahakikisha vifaa hivyo vinatumika ipasavyo kwa ajili ya kuongeza tija katika ufundishaji pamoja na kuvitunza ili vitumike ipasavyo.