*Apokewa na Katibu Mkuu na wafanyakazi wa wizara, aahidi kushirikiana na wadau kumsaidia Rais Samia kufikia malengo
Na MWNDISHI WETU
-DODOMA
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio amewasili rasmi ofisini na kuahidi kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza malengo yake kwa Taifa.
Alipowasili Ofisi za Wizara eneo la Mtumba, jijini Dodoma alipokewa na Katibu Mkuu Wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba, Menejimenti na watumishi wa Wizara ya Nishati.
Akizungumza mara baada ya mapokezi, Dk. Mataragio amesema, ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi ni nyenzo muhimu ya kuyafikia matarajio ya viongozi na Taifa kwa ujumla.
“Mimi nashukuru kwa kuteuliwa kutumika katika nafasi hii, na nitaendeleza ushirikiano na watumishi wenzangu, ili kumsaidia Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutimiza malengo yake,” amesema Dk. Mataragio.