Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ametoa tamko la chama hicho kulaani na kusikitishwa kwao na vitendo vya ukiukaji wa Utawala Bora unaozingatia Sheria na Haki za Binadamu pamoja na ukandamizaji wa Demokrasia unaofanywa na Serikali ya Chama tawala cha Burundi cha CNDD-FDD dhidi ya vyama vya upinzani nchini humo, hususan Chama Kikuu cha Upinzani cha CNL kinachoongozwa na Agathon Rwassa.
Amesema CUF- Chama Cha Wananchi kina taarifa za karibu kwamba Serikali ya Burundi imeandaa Mkutano Mkuu bandia wa CNL kwa lengo la kumuondoa kimabavu Rais halali wa Chama hicho, Agathon Rwassa.
Mkutano huo wa bandia ulifanyika muda mfupi tu baada ya Serikali ya CNDD-FDD kuendesha kamata kamata ya wabunge na viongozi wanaotokana na CNL na kuwaweka kizuizini kwenye gereza la Ngozi pamoja na jeshini huko Muramvya. Pia kuna mpango wa kumkamata Rwassa na kumbambikizia kesi ya ugaidi.
“Serikali ya Burundi imekuwa kikwazo kikubwa katika Utekelezaji wa Makubaliano ya Arusha kuhusu Amani na Maridhiano Burundi (Arusha Agreement on Peace and Reconciliation in Burundi- AAPRB) na kiongozi yeyote anayejitokeza kuhimiza utekelezaji wa makubaliano hayo anageuka kuwa adui mkubwa kwa Utawala huo. Chini ya Utawala wa CNDD-FDD, kuna mpango wa kulazimisha wananchi wote waunge mkono CNDD-FDD.
“Kwa kutumia kofia ya Uenyekiti wa Kituo Cha Demokrasia (Tanzania Center for Democracy – TCD), Januari mwaka huu, nilikutana na Ujumbe kutoka Burundi ulio ongozwa na Agathon Rwasa, Rais wa CNL, ambapo, pamoja na kuja kujifunza jinsi tunavyoendesha michakato ya maridhiano ya kisiasa bila kupigana, tulipata muda pia wa kujadili namna ya kukwamua utekelezaji wa Makubaliano ya Arusha kuhusu Amani na Maridhiano Burundi ( Arusha Agreement on Peace and Reconciliation in Burundi- AAPRB),” amesema Lipumba kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari
Amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwenye Kikao chake cha Desemba 2021, liliyataja makubaliano ya Arusha kuwa ni muarobaini wa matatizo ya amani nchini Burundi, na kutoa wito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na vyombo vingine ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhakikisha vinasaidia kutekelezwa kwa makubaliano hayo ya AAPRB.
“CUF- Chama Cha Wananchi kinalaani harakati zozote zinazofanywa na Serikali ya Burundi chini ya Chama cha CNDD-FDD katika kukwamisha Demokrasia na kujaribu kuzuia utekelezwaji wa Makubaliano ya AAPRB,” amesema Prof. Lipumba
Licha ya hilo, Profesa Lipumba amesema kuwa wanatoa wito kwa uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na marais wa nchi zote zinazounda Jumuiya hiyo ya EAC na hasa Tanzania, kuingilia kati kidiplomasia kutuliza hali ya kisiasa Burundi kabla haijashuhudiwa nchi hiyo ikirudi tena kwenye mauaji ya wenyewe kwa wenyewe.
“Aidha, mpango wa kumuondoa madarakani Rais wa Chama Cha CNL Mheshimiwa Agathon Rwassa kwa kutumia Mkutano Mkuu ‘bandia’ ni mpango haramu na unastahili kupingwa na kila Mpenda Demokrasia,” amesema