Home KITAIFA KAMATI YA BUNGE  YAKAGUA VITUO VYA GESI JIJINI DAR ES SALAAM

KAMATI YA BUNGE  YAKAGUA VITUO VYA GESI JIJINI DAR ES SALAAM

Google search engine

*Yashauri vituo vya kujazia gesi kwenye magari visambae mikoani, Naibu Waziri Kapinga akaribisha wawekezaji  kwenye CNG

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imekagua vituo vya gesi iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas – CNG Stations) Kituo cha kujazia gesi kwenye magari cha  Taqa – Dalbit kilichopo Kipawa jijini Dar es Salaam. Wa Saba kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo  na Wa Tano kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.
 
 

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imekagua vituo vya gesi iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas – CNG Stations)katika eneo la Ubungo Maziwa pamoja na Kituo cha Taqa – Dalbit vilivyopo Kipawa jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo iliyoongozwa na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga, Kamati ilipokea taarifa ya uendeshaji wa vituo hivyo iliyowasilishwa na Mhandisi Aristides Katto kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Mhandisi Katto amesema TPDC inatekeleza mpango wa ujenzi wa vituo

vitatu vya CNG katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na Mkoa wa Pwani ambapo vitajengwa pembezoni mwa barabara ya Sam Nujoma eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la wateja wanaohitaji kubadilisha magari yao kutoka kutumia mafuta ya dizeli na petroli na kutumia gesi asilia ambayo ina gharama nafuu ikilinganishwa na nishatiya petroli na dizeli.

Magari yakijaza gesi kwenye kituo cha Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati, David Mathayo aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanya uwekezaji katika sekta ya nishati  kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

 “Tunajua Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kuhakikisha inawekeza katika sekta hii ambayo itawezesha watanzania wengi kupata nishati ya gesi kwa gharama nafuu na kuepukana  na gharama kubwa za mafuta,” amesema

Kamati hiyo iliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya gesi katika mikoa mingine nchini ili kutoa fursa kwa wananchi kunufaika na huduma hiyo ambayo kwa sasa inapatikana katika Jiji la Dar es Salaam pekee.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga aliahidi kuuzingatia ushauri wa Kamati hiyo ili kuendelea kuleta mapinduzi katika sekta ya nishati.

Amesema kwa sasa Serikali ina mkakati wa kushirikiana na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kuongeza karakana kwa ajili ya kubadilisha mifumo ya nishati katika magari ili wananchi wengi waweze kupata huduma hiyo ya gesi.

Ziara hiyo imehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dk. James Mataragio, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC,  Mussa Makame na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na TPDC.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here