Na MWANDISHI WETU
-KONDOA
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imehoji Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kuhusu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alizozotoa wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa hospitali wa wilaya hiyo.
Kamati imehoji hayo wakati wa ziara ya kamati hiyo wilayani humo iliyofanyika Machi 15, 2024, ambapo hoja zilizohojiwa na LAAC kuhusiana na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Kondoa ni pamoja vifaa vyenye thamani ya Shilingi milioni 3.6 kutoomekana stoo, PVC, sakafu katika jengo la uzazi kuvimba na kubanduka, nyufa kwenye ukuta na nyongeza ya Sh milioni 260 ya kukamilisha mradi huku watendaji wa halmashauri hiyo kupata ugumu wa kujibu hoja.
Mwenyekiti wa LAAC, Halima Mdee alihoji uongozi wa halmashauri kushindwa kumwonyesha CAG udhibitisho wa mahitaji fedha hizo Shilingi milioni 250 zilizotajwa kwa ili kukamilisha mradi huo.
“Tupatieni uhalali wa nyongeza mnayoitaka katika kukamilisha mradi huu. Sisi nia yetu ni kuona jamii inawajibika katika kutunza na kulinda fedha za nchi hii,” amesema Mdee
Naye Mjumbe wa kamati wa hiyo, Esther Bulaya amehoji nini kimesababisha hoja za CAG ikiwemo kutouonekana kwa vifaa vyenye thamani ya Shilingi milioni 3.6, sakafu kubanduka, PVC kubanduka na nyufa.
Akifafanua kuhusu hoja hizo Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (anayeshughulikia Elimu) Dk. Charles Msonde amesema uadilifu mdogo na usimamizi usio makini umekuwa ukikwamisha utekelezaji wa miradi katika serikali za mitaa.
Amesema msingi mzima wa miradi ya Serikali ya Mitaa kutokamilika katika maeneo mengi ni kukosekana kwa uadilifu mdogo na usimamizi usio makini.
Awali, Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Joshua Mnyangale alisema Shilingi bilioni 1.8 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ulioanza Juni 20, 2020 na zilipokelewa kwa awamu tatu.
Amesema kulikuwa na changamoto kadhaa katika kutekeleza mradi huo ikiwemo ya muinuko mkubwa wa eneo la ujenzi kwenye jengo la mama na mtoto, kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi na kutofautiana kwa gharama ya vifaa vya ujenzi ukilinganisha na uhalisia katika utekelezaji wa mradi.