Na MWANDISHI WETU
-IRINGA
WAKAZI wa Kijiji cha Tungamalenga kilichopo katika Tarafa ya Idodi wilayani Iringa wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwawezesha kiuchumi ambapo wameeleza kunufaika na Shilingi milioni 57 ambazo zimetolewa kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) kama fedha mbegu wanazoweza kukopeshana na kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ambao wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Ruaha wamesema fedha hizo zimewasaidia kuboresha maisha na kuweza kuondokana na hali duni ya maisha kwani hujiunga katika vikundi na kupatiwa fedha mbegu ambazo huzitumia kuanzisha miradi mbalimbali ambayo hukubaliana inayowasaidia kujiingiza kipato.
Katibu wa Kikundi cha Kordun kutoka jamii ya Kimaasai Janeth Matambile, ambacho ni kimojawapo kinachonufaika na mradi huo amesema fedha mbegu wanazopatiwa zimewasaida kukopeshana na kuendeleza miradi mbalimbali waliyoianzisha ikiwemo unenepeshaji wa ng’ombe.
“Tulipatiwa fedha mbegu ambazo zimetusaidia kujenga mabanda ya ng’ombe ya kisasa kwa lengo la kuwanenepesha, mradi wa REGROW pia umetusaidia kuondokana na dhana potofu kuwa wanawake ni wa kukaa nyumbani tu na kwa sasa wanawake wanajishughulisha katika usindikaji wa maziwa na kutengeneza Sanaa,” amesema Janeth.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Tungamlenga, Linus Mheluka amesema kuwa mradi huo ulianza kwa mafunzo yaliyotolewa kwa vikundi ambayo yamechagiza kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatumika ipasavyo.
“Mradi wa REGROW katika Kijiji changu cha Tungamalenga ulianza katika mwaka wa fedha 2021/22 na ulianza kutoa mafunzo kwa vikundi alafu wakatoa mikopo. Sasahivi nina vikundi saba ambavyo vimeshapatiwa fedha mbegu takribani Shilingi milioni 57 kwa lengo la kukopeshana na kumekuwa na mabadiliko ya kiuchumi kwao,” amesema Mheluka.
Mheluka ameongeza kuwa mradi wa REGROW umetoa mafunzo kwa vijana wa kijiji hicho kupitia ngazi mbalimbali za vyuo ambapo Shilingi milioni 113 zimetolewa kufadhili masomo kwa wanafunzi 29 katika Kijiji hicho huku pia askari 10 wa Wanyamapori ngazi ya kijiji wakisomeshwa .