*YAITAKA TPDC KUONGEZA KASI YA KUUNGANISHA WATEJA, YATOA RAI KUHAKIKISHA WANANCHI WANAFIKIWA MAJUMBANI
Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya ziara katika viwanda mbalimbali Jijini Dar es salaam ili kukagua miundombinu ya usambazaji wa Gesi Asilia inayotumika katika Viwanda vinavyotumia mfumo wa gesi Asilia kama nishati.
Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake Dk.Mathayo David Mathayo, ilitembelea Kiwanda cha MMI STEEL TANPACK kinachojishughulisha na utengenezaji wa Mabati kwa kutumia Teknolojia ya Gesi Asilia kilichopo Jijini Dar es salaam.
Ziara hiyo imefanyika Machi 16, 2024 jijini Dar es salaam kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa hapa nchini, na kujionea ufanisi wa utekelezaji wake,ambapo walisifu uongozi wa kiwanda hicho kwa kutumia Teknolojia ya Gesi Asilia, na kuwataka watanzania kutumia Gesi Asilia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.
“Kamati imetembelea na kuona maendeleo ya matumizi ya gesi asilia inayotumika katika kuzalisha mabati na vitu vingine katika kiwanda hiki cha MMI STEEL TANPACK, hivyo tunawashauri Watanzania kutumia gesi asilia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji,” amesisitiza Mathayo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio amesema kuwa, Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya petrol nchini (TPDC), inaendelea na kazi mbalimbali za kuunganishia wateja wapya gesi asilia ikiwemo viwandani pamoja na hoteli, ili kuendelea kukuza matumizi ya nisha hiyo.
“Gesi Asilia inatumika viwandani na majumbani, hivyo tunawakaribisha wawekezaji wanaohitaji matumizi ya gesi kwa ajili ya uzalishaji na shughuli za kibiashara kujitokeza kwakuwa miundombinu ya gesi ipo tayari,” amesema Mataragio.
Ziara hiyo imehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC, Mussa Makame na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na TPDC.