Na MWANDISHI WETU
-KILIMANJARO
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Isdor Mpango ameipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maji nchini.
Ametoa pongezi hizo leo Machi 20, 2024 wakati akizindua mradi wa maji wa Kikafu-Bomang’ombe wilayani Hai mkoani Kilimanjaro uliojengwa kwa ustadi mzuri huku chenji ya zaidi ya milioni 577.6 zikiwa zibaki baada ya utekelezaji.
Aidha Mpango amewapongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Kilimanjaro kwa kutekeleza mradi na kubakisha fedha na kuwaagiza fedha hizo zilibaki kwenye mradi huo zitumike kupeleka maji kwa wananchi wa eneo la Matowo Wilayani Hai.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafiwa Mazingira Vijijini Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Weransari Munisi amesema gharama za mradi huo kwa mjibu wa mkataba ilikuwa utekelezwe kwa shilingi 3,392,463,389.08, kutokana na usimamizi mzuri mradi huo umekamilika kwa gharama ya Shilingi 2,814,854,757.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemhakikishia Makamu wa Rais kwamba Wizara ya Maji itaendelea na jitihada za kuhakikisha inasimamia maagizo ili kuhakikisha kila kona ya nchi inafikiwa na huduma ya maji.
Amesema yako mafanikio ambayo wizara imeyapata ndani ya nje ya nchi ikiwemo kuwa ya kwanza katika utekelezaji wa miradi ya maji Duniani kupitia mradi wa Lipa kwa Matokeo (PforR) kwa miaka miwili mfululizo na kwamba mafanikio hayo watayaendeleza.