Home KITAIFA SHILINGI TRILIONI 1.4 KUTUMIKA KUKABILIANA NA MALARIA, UKIMWI NA KIFUA KIKUU

SHILINGI TRILIONI 1.4 KUTUMIKA KUKABILIANA NA MALARIA, UKIMWI NA KIFUA KIKUU

Google search engine
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. John Jingu, akifungua Mkutano wa mkakati wa utekelezaji wa fedha hizo kupitia mradi mpya wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa saba leo Machi 21, 2024 jijini Dodoma.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu

Na MWANDISHI WETU

– WAF, DODOMA

SERIKALI imepokea jumla ya dola za kimarekani milioni 602 sawa na trilioni 1.4 za kitanzania kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu na Ukimwi katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. John Jingu leo Machi 21, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa mkakati wa utekelezaji wa fedha hizo kupitia mradi mpya wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa saba.

Dk. Jingu amesema kuwa fedha zilizopokelewa zimetokana na jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya ili ziweze kuwafikia wananchi katika maeneo yao bila kikwazo.

“Mkutano huu umeandaliwa kwa wakati muafaka ili uwe chachu ya kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unakua na ufanisi uliokusudiwa huku lengo letu ni kuangalia na kufanyia kazi mambo muhimu tuliyojiwekea kwenye mikakati itakayoongoza utekelezaji wa mradi huu katika kipindi chote cha utekelezaji,” amesema Dk. Jingu

Aidha amefafanua kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeendelea kutenga rasilimali zinazotumika kugharamia utekelezaji wa afua mbalimbali za kudhibiti Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na Uimarishaji wa Mifumo ya Afya hivyo ameushukuru mfuko wa dunia kuweza kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua zilizopangwa.

“Tunatakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji na kuongeza uwajibikaji kwa lengo la kuboresha hali ya utoaji wa huduma za Afya nchini. Ili kufikia malengo haya, wote tunao wajibu wa kusimamia na kutekeleza ipasavyo mipango tuliyojiwekea na kuwezesha shughuli zote za mradi ambazo zimepangwa kutekelezwa kwa kipindi cha mwaka 2024-2026 zinakamilika kwa asilimia mia moja,” amesema Dk. Jingu.

Akitoa salamu za Serikali ya Marekani, Mwakilishi wa Serikali ya Marekani, Dk. Etruda Temba, ameishukuru Serikali kwa kuandaa mkutano huo na kusema wadau wa Maendeleo wanatambua mchango wa Serikali huku akitoa angalizo wakati wa utekelezaji kuepuka ubadhirifu wa fedha ili kupata matokeo yaliyokusudiwa.

Washiriki wa Mkutano wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. John Jingu (hayupo pichani)
Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here