Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
MEYA wa Halmashauri y Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Songoro Mnyonge amelipongeza Shirika la Plan International kwa kutoa msaada wa vifaa saidizi kwa Jumuiya ya Wasioona Tanzania ( TAB) vyenye thamani ya zaidi ya Silingi milioni tisa.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo Machi 21,2024 katika Ofisi za (TAB) Jijini Dar es Salaam, Mnyonge amesema wasioona wanapitia wakati mgumu pindi wanapokosa vifaa saidizi ambavyo vingeweza kuwasaidia kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
“Nimesikia kuna wengine wametokea Buza, Kigamboni, Goba na maeneo mengine ya mbali na kufika hapa ofisini kwao, wamekuwa wakipatiwa msaada na wananchi wa maeneo ya Kinondoni kufika kwenye neoe hili la ofisi, hivyo basi kuna umuhimu wakapata vifaa saidizi,” amesema Meya Mnyonge.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uchechemuzi Shirika la Plan International, Cecilia Bosco amesema vifaa hivyo vitawasaidia kutoka kwenda katika Shughuli zao za kila siku za kujipatia kipato.
Kutokana na na hali hiyo, amesema wameipatia taasisi ya watu wasioona vifaa ambavyo ni fimbo nyeupe 100, Karatasi za kijivu pisi 100 pamoja na A4 fremu pisi 50 ambazo hutumika wanapokuwa wanaandika ambapo itawasaidia katika shughuli zao.
Amesema wataendelea kuimarisha nakuongeza nguvu kuwasaidia watu wasioona pamoja na makundi mbalimbali yenye mahitaji maalumu nchini kwa lengo la kupunguza changamoto wanazozipitia.
Naye Mtunza hazina wa Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania, Seif Hamis amesema vifaa hivyo ni muhimu ambapo itawasaidia kuzifikia fursa mbalimbali.
Aidha ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambapo imefungua milango ya fursa mbalimbali ikiwamo kwa watu wasioona.